Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Wednesday 21 December 2011

Kijiwe chagawa nishani kama njugu

JUZI kijiweni kwetu kulikuwa na shughuli bab kubwa. Dk, profesa, Al Haj, Mwalimu, Field mashall, shehe, ulamaa,maulana, Man and a half, askofu, Mpayukaji mkuu wa kijiwe niliamua kutoa nishani kwa washirika zangu kwa uvumilivu na kufumba macho niendelee kuhomola na kina Mbwa Mwitu.

Mtu wa kwanza kupewa nishani alikuwa ni mgosi Machungi kwa ikiwa ni shukrani yangu kwa kujikomba vilivyo na kuhakikisha mzee mzima siguswi hata ninapofanya mazabe. Amehakikisha anawanyamazisha vidomodomo wanaotaka kugusa ulaji wangu. Machungi ambaye wanakijiwe humtania kuwa ni spika wa kijiwe al maarufu Baba Makidamakida kutokana na lugha yake ya kucheza makidamakida. Mgosi alichukua nafasi ya msomi Sam Sixx Mkatatamaa. Kupewa nishaku kulizua utata ni kwanini alipewa nishani huku nikimnyima Sam Sixx.

Watu wengine wagonjwa kweli kweli. Wakiniona nachekacheka wanadhani kicheko changu na tabasamu ni vya kweli. Kwa taarifa ya msionijua, mimi ni bingwa wa kulipiza visasi hasa kwa viherehere wanaotishia ulaji wangu.

Juzi niliwaambia jinsi Eddie alivyoniadhiri kwenye sakata la kuvuana gamba kijiweni. Adhabu yake ya kwanza kama utangulizi ni kumnyima nishani ili baadaye nimtoe nishai. Anadhani nilishindwa kumpa nishani kama ningeamua?

Najua ananilaumu kwa sasa bila kujua kuwa anapaswa alaumu domo lake na woga wake. Hata kama kwenye kashfa ya Richmonduli ya wizi wa pesa ya mkaa kwa kumpa gabacholi tenda ya upendeleo wakati ni tapeli tulikuwa wote kwanini asije nyumbani tukayamaliza badala ya kwenda kunianika? Hopeless kabisa.

Halafu mpuuzi huyu eti ana mpango wa kutaka kurithi nafasi yangu nitakapoachia ukanda wa kuibia kijiwe!

Aliyefuata kwa kupewa nishani ni loh! Nimesahau jina lake! Anyways, majina ya waliopata nishani si muhimu zaidi ya wale walionyimwa. Maana waliopewa hawalalamiki ingawa wanalalamikiwa.

Aliyenyimwa nishani si Eddie Ewassa tu bali hata brother Johhnnie Sam Mali-sera ambaye kijiweni hujulikana kama mzee Maneno kutokana na maneno yake ya kufyatua na lafudhi yake ya ki-Idodomya.

Huyu bwana nilimnyima nishani kutokana, kwanza, kutaka kushindana nami kwenye uchaguzi wangu wa kwanza wa kuwa mkuu wa kijiwe miaka kama nane sita iliyopita.

Pia mke wake bi mkubwa Hana Mali-sera ana tabia ya kunikosoa kosoa hasa akimuunga mkono Sam Sixx na wenzake wanaposhambulia utawala wangu kijiweni. Huyu mama ametokea kuwa mwiba kiasi cha kunifanya nikose usingizi. Hata hivyo kwa kumnyima mshirika wake wa bedroom nishani, nadhani message sent. Atachagua kusuka au kunyoa.

Ukiachia mbali niliowanyima nishani kutokana na kuwalipizia visasi na kuwapa taarifa kuwa mie siye yule wamtaniaye, kuna wengine niliwasahau kiasi cha kujisikia vibaya ingawa hapo baadaye nitawapa nishani.

Hawa ni Endelea Chenga na Rosti Tamu Laazizi ambao nitawapa nishani kutokana na kufanikisha mikakati yangu ya kuukwaa ukuu. Pia ndugu yangu Petero Nonyi wa Noni naye nitamkumbuka kipindi hiki. Hivyo, nawataarifu wasikate tamaa.

Kipindi hiki nikiwapa nishani nitahakikisha na mshirika wangu wa bedroom mama Kidume Riziki anapata pamoja na kidume chenyewe Riziki. Hawa watapata nishani kutokana na kufanikisha ulaji kwenye familia yetu hasa mke wangu mpendwa mwalimu Salima ambaye pia ni rais wa wanawake wote kijiweni chini ya chata lake la MAWAWA, yaani Wake za Wakubwa na Maulaji.

Rizi nitampa kutokana na kufanikisha kuwagawanya vijana kijiweni pale wanapotaka kuingilia ulaji wa mshua. Ikumbukwe kuwa yeye pia ni rais wa vijana kama ambavyo Halfa ni rais wa chipukizi.

Pia nitahakikisha nasuka mpango na vyuo vikuu vya kule Ulaya nilikosomea kuhakikisha naye anapewa shahada ya Udaktari tena wa Uchumi na Sheria.

Pia napanga kutoa nishani kwa mgambo wa kijiwe al maarufu Polishi wa kijiwe. Hawa wamefanikiwa kuwatia adabu wote wanaopinga ulaji wangu. Wamekuwa wakifanya kazi kubwa hasa kuwapiga wanywa kahawa wanaotaka kuanzisha mada za kunipinga au kuandamana kwa midomo kupinga maulaji yangu.

Nisiwachoshe na zoezi la kutoa nishani. Baada ya kuhitimisha zoezi hili niliteua wawakilishi wa wanywa kahawa kwenye vijiwe marafiki huko nje ya nchi.

Pale kwenye kijiwe cha River Road Nairobi nilimteua shoga wa mke wangu, Batinda Kwaherini kuwawakilisha walevi na wanywa kahawa pale Nairobi.

Pia nimemteua daktari mwenye shahada kwenye kuzuia jinai ya kughushi (PhD in faking) Dolorous Kamaliza kuwa mwakilishi wetu kwenye kijiwe cha kahawa cha Udachini ambako nasikia kahawa inanywewa sana.

Sikuishia hapo, kwa mamlaka niliyopewa na kijiwe, nimemteua bwana Phil Zilipendwa Mammie kuwa mwakilishi wetu kwenye kijiwe cha kwa akina Huaa Guo Feng ambako nako kutokana na baridi nasikia kahawa inanyweka vilivyo.

Kimsingi hawa washirika wangu nilitaka kuwapa nishani. Lakini baada ya kusikia minong’ono kuwa kama wanakijiwe waliwapiga teke wanapewa nishani za nini.

Kwa hasira niliamua kuwaudhi hawa waliowapiga teke kwa kuwapa ulaji mkubwa tu. Waende kule waniwakilishe na si wanakijiwe wambea wasio na shukrani hata ukiwapa takrima wakakuchagua bado wanataka eti uwakomboe wakati hukuchaguliwa kuwakomboa bali kurejesha takrima yako.

Leo sitasema mengi kutokana na kuwahi kwenda kupanda pipa kwenda kutanua na bi mkubwa baada ya kujihakikishia kuwa tumeshinda zoezi la kuvuliwa magamba. Najua hapa wasomaji wameishaanza kutoa mimacho wakidhani nimechanganyikiwa kupanda pipa wakati hata nauli ya dala dala yenywe ni mbango.

Ninaposema kupanda pipa namaanisha kupata lift kwenye shangingi la fisadi fulani ambaye anataka kunitumia kumsafisha. Upo hapo mshirika?

Kabla sijasahau. You know what? Msianze kuchanganyikiwa kwa maulaji niliyoelezea pale juu mkadhani nimewatosa baadhi ya washirika zangu wa karibu.

Kwa ufupi huo hapo juu ni mhutasari wa mipango yangu ya mambo nitakayofanya siku nikigombea urais nikaupata. Hivyo, msihangaike kwenda kwa vigagula bure kuniroga. Pia muelewe kuwa haya yaliyoandikwa yaliandikwa nikiwa kitandani naota.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 21, 2011.

1 comment:

Malkiory Matiya said...

Njugu zinaendelea kugawanywa. Akina Lubuva nao wamo, ulaji kwa kwenda mbele kama wasemavyo wabongo!