The Chant of Savant

Wednesday 21 March 2012

Maskini Benjamin Mkapa!

“Kwa nguvu zangu zote wakati nina uhai, nitatetea haki za wananchi wa Tanzania pamoja na kumilki ardhi na kuitumia kwa maendeleo yao,” Hiyo ni nukuu ya aliyosema rais mstaafu Benjamin Mkapa alipokwenda kumnadi mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki.

Kwanza, kwa wengi, hiki kimeonekana kuwa kichekesho cha aina yake kinachomvua Mkapa nguo kiasi cha kuonekana kuishiwa mbele ya jamii. Kwani wengi wanauliza: Mbona hakufanya hivyo yaani kulinda haki za watanzania kwa nguvu zake zote wakati akiwa madarakani zaidi ya kujinyakulia mali za umma? hata hivyo, hapa kuna somo kuwa kila chenye mwanzo kina mwisho na ukipewa dhamana ukaifuja unaishia kuishi kwa aibu, kutegemea kulindwa na hata ghilba na hadaa. Kwa mtu wa hadhi ya Mkapa, kupayuka si saizi yake achia mbali kuongopa mchana kweupe. Maskini Mkapa!

Wakosoaji wanahoji: Mkapa anataka kumdanganya nani wakati siri zake ziko ugani kwa miaka nenda rudi? Hivi Mkapa anadhani watanzania ni wasahaulifu na mataahira kiasi hicho? Je hapa nani anajidanganya ukiachia mbali kudanganya? Mkapa hawezi kusameheka bila kuleta utetezi wake tena unaoingia akilini. Hakuna shaka kuwa sasa Mkapa anahaha kujua nani atamrithi Jakaya Kikwete ili amhakikishie ulinzi asishitakiwe kwa kashfa zake na familia yake. akitaka msamaha siyo ajitetee tu bali arejeshe mali za umma na kuomba msamaha kwa watanzania akikiri kuwa alikosea na kushawishika kiasi cha kuchafua ofisi waliomwamini kuiendesha kwa niaba yao.

Wengi wanashangaa kama kweli wananchi wa Arumeru Mashariki watakubali kugeuzwa wajinga na wapumbavu ambao wanaweza kuipigia kura CCM kwa kubariki kile kinachoonekana kwa wachambuzi wengi kama uongo wa Mkapa. Wengi wanahoji: Je Mkapa anaishi dunia gani ambaye hajui kuwa wananchi hao hao anaowahadaa kuwa atapigania haki zao kwa nguvu zake zote hadi kufa wanaendelea kukumbwa na matatizo yatokanayo na uhaba wa ardhi baada ya ardhi yao kubinafsishwa kwa marafiki na washirika wa Mkapa tena chini ya utawala wa Mkapa huyo huyo. Amenikumbusha kisa cha Alikwina yaani alikuwa wapi? Mkapa ulikwina ? Badala ya kujibu hoja vilivyo alikimbilia kujifanya mwanafamilia ya marehemu baba wa taifa kiasi cha kuwatoa wengine walioamua kumpasulia bomu ambalo limemuacha hoi.
Inashangaza kwa mtu mwenye hadhi ya Mkapa kukosa kumbukumbu kiasi hiki ukiachia mbali kusema vitu visivyoingia akilini kama vile. Kwa walioshuhudia au kusikia aibu iliyomkuta rais mstaafu Benjamin Mkapa wanajiuliza kulikoni.
CCM iliomba kuwepo na kampeni za kistaarabu na si matusi na uongo. Ajabu CCM hiyo hiyo ndiyo ilikuwa ya kwanza kuvurumisha matusi ukiachia mbali kusema uongo. Matusi yasiyo na lazima wala saizi ya Mkap, hata hivyo si kosa la Mkapa. Kwani CCM sasa ni chama kilichoishiwa kuliko wakati wowote wa historia ya kuanzishwa kwake.

Watu wanajua ukweliNBC, EPA IPTL Kiwira Tanesco-Net Group Problems ambazo zilikuwa dhana za utawala wa Mkapa kujikusanyia pesa binafsi nyuma ya pazia. Nani mara hii Mkapa alivyotishia kila aliyejaribu kumpa ushauri kwa mfano asiuze NBC? Ni juzi siri ya siri ilifichuka kiasi cha Mkapa kutuhumiwa kuwa nyuma ya kifo cha baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere kama ilivyodaiwa na mwanae ambaye naye hajajibiwa na Mkapa.
Kimsingi, ujio, na maneno na uwepo wa Mkapa Arumeru Mashariki haukuisaidia CCM bali kuiangamiza. Maana watu si wapumbavu wala wajinga kama anavyodhani. huwezi kwenda jukwaani ukahubiri matusi na uongo chama chako kikapewa kura hata kama wapiga kura wanakupenda au kukipenda chama chako. hapa hapendwi mtu bali haki na maendeleo ambavyo CCM imeshindwa kutimiza kwa miongo iliyokuwa madarakani zaidi ya kundi dogo la watu kujihudumia kwa kuwanyonya walio wengi ambao sasa linawahadaa na kuwafya vipofu na mataahira.
Hivi Mkapa anadhani watanzania wanasahau athari za kufanyia biashara ikulu ambapo wachukuaji wanaoitwa wawekezaji walifanikiwa kuiweka nchi yetu mifukoni mwao kwa kuwahonga wakubwa huku raslimali zetu zikigeuka laana kwetu? Kama amesahau aende Mara, Mwanza, Shinyanga hata arudi huko Arumeru aone madhara ya sera na uroho wake. Aende aone watu wake wanavyowanyanyasa watanzania huku wakipora raslimali zao na kuacha madhara makubwa kiikolojia. Maskini Mkapa hayaoni haya yote. Bado anaotea siasa za kibabe na urushi za wakati wake ambapo alidai kuwa sera yake ilikuwa uwazi na ukweli kumbe akimaanisha kinyume kama ilivyokuja kubainika kuwa sera yake ilikuwa ni uchukuaji, usiri na uongo.

Mkapa anapaswa kuambiwa kuwa aache kudhani kuwa watanzania ni kama mawe ambayo huwa hayabadiliki wazi wazi ingawa yanabadilika. Maskini Mkapa. Aibu! Wahenga waliasa kuwa asiyejua maana haambiwi maana na asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Heri Mkapa angejiendea Moshi, Lushoto au Mtwara akajipumzikia kama siyo kulowea Upanga kuliko kuzidi kuwachokoza watanzania aliowadhulumu yeye familia yake na marafiki zake alioshirikiana nao kwenye makampuni yao ya kuiba Kiwira.

Tumalizie makala hii kw a kumtaka Mkapa akumbuke maneno haya wakati akitafakari nafasi yake kama rais mstaafu. “Ndugu zangu msidanyanyike na kuendelea kuwasikiliza CCM miaka yote wameshindwa kurejesha ardhi ya Meru sasa wanaibuka…..huyo Mkapa alishindwa akiwa rais sasa amekaa nyumbani akisubiri posho ataweza kumshauri rais awarudishie ardhi yetu?” Mbunge Israel Natse (CHADEMA) jimbo la Karatu. Mnaweza kuongeza kuwa: Kwanini Mkapa kama ni jabali kweli hataki kujibu tuhuma za uchafu aliofanya akiwa ikulu?
Chanzo: Tanzania Daima Machi 21, 2012.

No comments: