The Chant of Savant

Wednesday 4 July 2012

Tuagize matabibu na rais nje kutatua tatizo


BAADA ya kugudua kuwa kumbe lisirikali halina mpango wa kushughulikia mgomo wa matabibu, kijiwe kimekutana kutoa shinikizo kutokana na mambo makuu mawili: Mosi ni kutekwa kuumizwa na hata kujaribu kuuawa kwa kiongozi wa matabibu Dk. Steve Walimboka. Huu ni uhuni wa aina yake hasa kutendwa na wale waliokabidhiwa dhamana na umma wa walevi. Kwanini wapuuzi hawa walipwe njuluku zetu na watumie neema hii kutishia haki na maisha ya watu? Pili tunashinikiza wahusika wawajibike maana wameshindwa.
Dk. Msomi Mkatatamaa analianzisha:“Jamani, nimekuwa nikisema kuwa kaya hii imewashinda watuwala wetu. Sasa wakati wa kuwakashafi naona kama umewadia. Maandishi sasa yako ukutani. ni kazi kwa walevi kujitambua na kuwapa kibano kama walichompa Dk. Walimboka.”
Dk. Mgosi Machungi kama, kawa, hakawii kunyaka mic, “Mimi naona tianzishe haakati za kurejesha heshima ya kaya yetu hasa baada hii mijitu kuanza kutichokoza. Badaa ya kushughuikia madai ya matibabu mnawateka na kuwapiga! Je, hio ni jibu?”
Dk. Mipawa naye hakawii. anakwanyua mic, “Nyie mnashangaa kutekwa na kuteswa kwa Dk. mwenzetu Walimboka? Mbona huu umekuwa ndiyo utamaduni wa manyang’au hawa? Nani mara hii kasahau kina Kolimba, Sokoine, Kombe na wengine waliowahi kufanyiwa huu ubazazi kutokana na misimamo yao?”
Leo kila mtu ana hasira. Dk. Mpemba hakawii, “Yakhe naona sasa kitaumana na kueleweka kama kweli walevi wataka ukombozi. Nashangaa kuona jamaa apendaye enda hospitalini na kwenye maziko hata hakwendamjulia hali Dk. Walimboka.”
Dk. Mbwa Mwitu hakawii, anatia guu kinamna. “Ami ulidhani jamaa wa sanaa angeenda. Aende wakati hii ni aibu yake jamaa wangemtoa macho kama si kucha kama jamaa zake walivyomfanyia Walimboka. Kipindi hiki imekula kwake. Hakuna kifo cha msanii maarufu yeyote wa kutumiwa kukwepa aibu na madhara ya mgomo huu unaoangamiza maisha ya watu wasio na hatia ukiachia mbali kupata ujiko wa dezo.”
Naye Dk. Maneno anakwanyua mic huku akitupa kipisi chake cha sigara kali, “Yote tisa, kumi eti nasikia lisirikali lina mpango wa kuagiza matabibu baada ya wale waliochoka na ushenzi wake kugoma. Hii ni ajabu na kweli kaya hii ni ya ajabu! Haingii akilini eti unashindwa kuwalisha wanao eti unakwenda kujifanya unatoa msaada kwa watoto wa jirani. Wapiga chaki wakigoma, mnaagiza nje. Wake zenu wakigoma mnaangiza, waume zenu wakigoma mnaagiza nje. Nchi ikigoma mnaagiza nje. Kama kuangiza matabibu toka nje si tusi kwa matabibu wetu basi agizeni na rais anayeweza kuzuia upuuzi huu unaoitwa kuagiza matabibu nje.”
Kila mtu hana mbavu kwa jinsi alivyopanga migomo hadi kwenye bedroom. Anaendelea huku akiwa anajifuta kijasho tokana na kijua kuzidi kutuwakia, “Mie naona kama umma ungeshirikishwa nadhani ungeshauri kuagiza wanasiasa nje hasa Uchina wanakonyonga mafisadi kabla ya madaktari ili wapatikane watu wanaoweza kusimamia kaya yetu vizuri au siyo?”
Dk. Msomi amepata mwanya, anakatua mic, “Je madaktari wa nje ni suluhu? Kwa nini watu wanapenda sana kutumia masaburi badala ya vichwa kwenye mambo nyeti kama haya? Kama kuangiza matibabu toka nje ni suluhu, tutaona. Ni tabibu gani atakuwa tayari kufanya kazi jehanamu ambako umeme, vitendea kazi, usalama, maslahi na mambo mengine ni ndoto?”
Anampungia mkono rafiki yake mmoja anayepita kijiweni na kuendelea, “Hivi hawa wanaotuma mbwa wao kuwateka na kuwaumiza matibabu wangekuwa wanatibia humu kayani wangefanya hivyo? Wanajali nini iwapo wao wanatibia Apollo? Laiti hata huko Apollo wangewagomea wakaona cha mtema kuni.”
Dk. Machungi anarejea dimbani tena,“Hii kaya imekuwa ya hovyo sana. Mabiioni mnaweka nje. Akiii nayo naona imewekwa nje. Tianze kutumia akii badaaa ya masabui. Asemayo Dk. Mfiosofe ni kweli. Wao wanatibiwa nje kwa njuuku yetu haafu wanataka watumaize sisi. Hawana akii hawa. Hii ni sawa na kumkamua ng’ombe haafu unamchinja ukitegemea kupata maziwa baadaye. Hivi nani anawashaui hawa viaza?”
Dk. Mchunguliaji ambaye alikuwa ameshika shavu muda wote anaamua kujitosa kutoa dukuduku, “Kaya ina uhaba wa madaktari eti wapuuzi fulani wanafukuza matabibu! Ni ajabu. Hii ni sawa na mtu asiye na chakula cha kutosha akaanza kumwaga kidogo alicho nacho. Kwa pesa ipi mnatishia kuleta watu toka nje wakati kila kitu ni kopakopa na ombaomba? Kaya yenyewe hata matabibu wa kutosha haina eti mnafukuza kazi madaktari?”
Dk. Kidevu anakwanyua mic, “Lazima matabibu wafukuzwe kwa sababu wao wanatibiwa Apollo . Isitoshe wakipata chansi ya kuagiza matabibu wengine watatumia nafasi hiyo kupiga dili zao za kutoroshea njuluku nje kwa kisingizio cha kutuma pesa ya kusafirisha matabibu. Mpo hapo washirika?”
Dk. Mpemba anarejea tena naye kumwaga wizidom, “Yakhe mwanchekesha. mwadhani hawa jamaa wana utu? Hamkuwasikia hao wezi na wambea waTakokuru wakisema eti watahakikisha hiyo fedha iliofichwa huko Uswisi itarejeshwa kayani? Mie naona hawa Takokuru sijui Takokubwa wataka nao wapewe chao kama walivozoea halafu nchezo uishe.”
“Kweli kama walivyosema waliotangulia kaya hii ni ya ajabu. Leo watu wanakufa, wenzao wanaendelea kupiga siasa za kitoto tena zilizojaa fikra za kimasaburisaburi. Mie nadhani wagonjwa hawataki kusikia ngonjera na hadithi za tutaleta matabibu wengine. Kwa pesa ipi iwapo pesa yenyewe ni ya kuombaomba na kuibiwa ibiwa hovyo?” Aling’aka Dk. Mipawa.
“Ingawa mgomo huu si jambo la kushangilia, umenifurahisha kwa sababu utatusaidia kuona matatizo ya watu wetu kwa ukaribu zaidi ili tutafute suluhu kama wenzetu wa Masri, Libia na hata Tunisiya. Mpo hapa waheshimiwa? Huu nidyo wakati. maana hawa jamaa walivyo hamnazo, ama utasikia Mtalii katimkia nje au mmoja wao amepelekwa Apollo kama si Ujerumani kucheki mafua. Wanatudharau hawa hatuna haja ya kuwaogopa wala kuwaheshimu.” Dk. Msomi alipigilia msumari wa mwisho.
“Du! Kila mmoja anajisemea.
Tukiwa tunaendelea si likapita gari la Daktari fweki, Hossni Muinyi! Tuliamua kulikimbiza ili timtie adabu.
Chanzo:Tanzania Daima Julai 4, 2012.

No comments: