The Chant of Savant

Wednesday 2 January 2013

Wao wanakuza uchumaji sisi uchumi!


MTAALAM mmoja wa uchuma na uongo zii aitwaye Denjaman Chinga Mkapa alisema kuwa ukitaka kujua kuwa kaya yenu imeendelea angalia jinsi wachukuaji waitwao wawekezaji wanavyomiminika kwenye kaya yako na kuchuma na kuondoka.
Denjaman aliongeza kuwa kigezo kingine cha kukua kwa uchumi ni kwa kaya kuwa na uwezo wa kukopesheka na kusifiwa ujuha. Kwa misingi ya falasafa ya Chinga ni kwamba uchumi wa kaya yetu umekuwa kwa vile tumeweza kuongeza ukubwa wa uchumaji wetu kiasi cha deni la kaya kukua kama vile limelishwa hamira.
Taarifa za hivi karibuni za waziri wa Fedheha na Uchumaji, Willy Mgimwe zinasema kuwa deni la kaya limeongezeka toka dolari bilioni tatu mwaka 2007 hadi dolari bilioni 14.
Hili ni ongezeko la kujivunia la asilimia 400.
Hii ni kwa mujibu wa wataalamu wenzake kama vile Mzito Kabwela na Profwesa Harry Malipumba.
Mgimwe aliendelea kuwaambia walevi kuwa wasiwe na wasi wasi wala haraka ya kuhoji uongezekaji wa uchumaji kwa vile sirikali inawekeza kwenye miradi ya kiabunwasi ya maji, maziwa na nishati.
Kwa mujibu wa tafsiri yangu ya maneno ya Mgimwe ni kwamba, walevi wategemee mabomba yao ya maji kuanza kutoa maziwa huku nishati ikiendelea kupatikana hata kwenye miti.
Kwa maana hii, ndugu zangu chingas walistuka wakahoji kwanini wao waendelee kuuza nnazi wakati kule Bwagamoyo kwa wauza mnazi wao wauze wese toka Mnazi Bay? Wao wanataka wauze wese na jamaa zangu waendelee kujiuzia mnazi ilahi mkulu anatoka kwao. Jamani hii ni haki? Hayo tuyaache.
Ndoto ya Mgimwe ni nzuri sana hata kama ni ya kihekaya hekaya za Alfu Leila Uleila. Kinachofurahisha ni kwamba kweli walevi hawatahoji kwa vile wamelelewa kwenye misingi ya kuwaamini wakubwa wao hata kama wanajua wanachosema ni upuuzi na uongo ambao hata kuku hawezi kuukubali.
Kwa wanakaya wanaoona mbali, haya ni maendeleo makubwa ukiachia mbali yale tuliyofikia mwaka huu ambapo wanakaya wenzetu walitengeneza mishiko kiasi cha kufurisha mabenki yetu. Hivyo kulazimika kupeleka mafweza mengine kule Uswisi kwenye nchi ya vibaka inayotunza pesa ya kila kibaka duniani.
Wabongolala wanapaswa kumpongeza mkulu Njaa Kaya kwa kuwezesha mafanikio haya ambaayo ni ushahidi kuwa maisha bora kwa wao wote yanawezekana.
Viashiria vingine vya kukua kwa uchuma ni kudumaza uchumi na kukuza uchumaji. Ili kufanikisha hili, kaya lazima itumie sana ili kufanya pesa izunguke kaya na dunia nzima. Hivyo, wanaolalamika kuona bei za vitu vikipanda wanapaswa kukumbushwa kuwa hiki ni kiashiria cha maendeleo na kukuwa kwa uchuma.
Wasiojua kanuni za kukuza uchumaji na uchuma utawasikia wakimlaumu mkuu kwa kusema eti anazurura yeye na bibi yake wasijue hiyo ndiyo sera yake. Kama yeye na kibeti chake wanazurura kwani wamefunga barabara na viwanja vya ndege. Nanyi chumeni mkazurure ili mjue raha ya kufanya hivyo.
Mkulu amekuwa mbele pamoja na bi mkubwa wake kutembelea kaya zote duniani ili kutangaza mafanikio ya kukua kwa uchuma na uchumaji.
Juzi mzee mzima nilijaribu kuzurura kama mkulu. Nilikwenda zangu kule Ntwara nikalala Nanguruwe, asubuhi nikaenda zangu Nanyumbu, kabla ya kuelekea Tunduru maeneo ambako nilikula chakula changu cha mchana Nakapanya.
Nikiwa nakamata chamaki nchanga mjini Mtwara si wakaibuka mamia ya watu wakipinga eti gesi yao kuibiwa na kwenda kuuziwa Bwagamoyo. Walikuwa na kila aina ya vipeperushi. Nilivutiwa na kimoja kilichosema, “Njaa Kaya tafuta gesi ya Wakuere hii ya Ntwara ni ya wamakonde,”
Ukisikia kukua kwa uchuma na uchumaji chini ya sera ya Uhujumaa na Kujimegea ndiyo huku. Hawa wanachuma. Wale wanachumwa. Hawa wanakula. Wale wanaliwa. Na amani inaendelea kuwapo kila mtu akijiridhisha kuwa amefanya jambo la maana na la kimaendeleo.
Ingawa haipendezi kuwaeleza hivi walevi, ukweli ni kwamba watake wasitake wataliwa tu. Vinginevyo kama wanaweza nao waanze kuwala wale wanaowala wao. Bila kuamua kupambana wapo watakaoliwa milele na watakaokula milele.
Hivi nitumie lugha gani mnielewe enyi walevi wapumbavu? Mna macho lakini hamuoni, mna masikio lakini hamsikii. Hivi hamuoni wanene wanavvyoendelea kurithisha ulaji na unene kwa vitegemezi vyao? Mbona vimejazana kwenye mjengo na asasi nono nono nanyi bado mnakalia kulalamika?
Kwani hamuoni kinachoendelea kuwa kinalenga kuwala na kuwachuma maisha yenu yote nyinyi na vizazi vyenu? Haya shauri yenu. Ila kuna siku mtanikumbuka ingawa sitakuwapo.
Hakuna kitu kilinifurahisha kama kushuhudia matunda haya ya uchumaji na uchuma. Maana kila mtu anataka kuchuma hata kuchuma kwenyewe kama ni matokeo ya kumchuma mwenzie. Zaainzibaa walianza wakidai wese lao halifaidiwi na bara. Wao wanaona kufaidi vinono vya bara kama ulinzi, usalama, vyakula na hata kupata mahali pa kuzaliana kirahisi na kifahari kuliko wese lao kutumiwa na wabara.
Hapa kitaalamu tunatumia kanuni ya changu kichungu chako kitamu na changu changu na chako chetu. Chini ya kanuni kama hii,ufisi na ufisadi huzaliwa kiasi cha kaya kugawanyika vipande vipande kama ile mitandao maslahi ya chama cha Mitandao.
Turejee kwenye kukuza uchuma na kudumaza uchumi. Ili kukuza uchuma lazima uchumi uuawe au kutelekezwa. Katika kufanya hivyo mhusika huwekeza kwenye viini macho kama barabara ambazo hazifikii viwango na madudu mengine kama kukopa hovyo hovyo ili aweze ku-survive.
Essentially, this is the venue of lunatics and megalomaniacs who sees nothing except their tummies and massaburis. Such merry-andrews see no tomorrow and tomorrow for them is dangerous. Samahani, nimechonga kikameruni kuonyesha kuwa nimesoma kama yule waziri wa wanyama aliyehojiwa na kachangu fulani akamwaga uswangilishi ili kuficha uovu wake wa kufanya biashara ya utalii wakati ni waziri wa wizara hiyo. Nadhani brother Lazarus Nyalandudu unanipata pata kama siyo kunideku.
Kama tulivyoanza, tumalize na falsafa ya Denjaman itekelezwayo na Njaa Kaya. Gwiji Denja alisema kuwa ili kufanikisha kukua kwa uchuma na uchumaji, lazima kila maskini atumie mtaji wake ambao ni nguvu yake.
Hivyo, mnachopaswa kufanya maskini hapa, ni kuunganisha nguvu yenu na kuwakabili wale ambao nguvu yao ni yenu watuwala wanaowala na kuwatawala. Mmenielewa?
Du! Kumbe sijaaenda kuchuma ili nikuze uchuma! Leo bi mkubwa atanitambua lazima nichume kwake!
Chanzo; Tanzania Daima Januari 2, 2013

No comments: