How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 26 November 2013

CHADEMA: Kwenye msafara wa mamba kenge wamo


KWA wenye kufuatilia siasa zetu za ulaji, urushi, unafiki na ubangaizaji, hawakushangaa kilichotokea kwenye chama kikuu cha upinzani Chadema. Baada ya Chadema kuwachukulia hatua za kinidhamu “waasi” ndani ya chama, mitandao ya kijamii ilifurika maoni. Yalikuwamo maoni ya aina mbili, yale ya wanaoipongeza Chadema kuondoa kansa na wale wanaoiponda kwa kuizushia kila aina ya uchafu hata usioingia kwenye akili hata ya njiwa.
Wahenga walisema; Kwenye msafara wa Mamba na Kenge wamo. Ama kweli hawakukosea wahenga kwa vile tumekuwa tukishuhudia wanasiasa uchwara na nyemelezi wakihama vyama lakini bado wakibaki wakimtumikia baba yao ambaye kila mmoja anamfahamu.
Tuliwaona akina Shibu—da, Mre—ma, Mba—tia, Che—yo na wengine wengi wakijiacha uchi kutokana na kutumikia mabwana wawili. Hata hivyo, wahusika walisahau kitu kimoja cha msingi, za mwizi siku zote ni arobaini.
Ukiangalia walichokuwa wakijaribu kufanya waasi wa Chadema, unagundua utoto na ukosefu wa mikakati hasa ikizingatiwa wakati walipokuja na mkakati wao. Huwezi kuanzisha mabadiliko ya uongozi ndani ya chama kwa njia ya mlango wa nyuma ukafanikiwa.
Hata kama una hoja na sababu ya kufanya hivyo utakwama kutokana na uharamu wa njia uliyotumia. Waingereza husema, the end justifies the means lakini huwezi ukahalalisha mbinu iliyogunduliwa na bazazi na nyemelezi Macchiavelli alipokuwa akitumikia usomi na utawala wa Kirumi ili kuishi.
Leo hii tutasikia mengi kuhusiana na Chadema. Hata hivyo, haya yanayotumiwa na wachovu na wabaya wa Chadema kuipaka matope si mapya. Usishangae kusikia uchaga, udini, ukanda na hata u-dot.com kwenye uchafu huu wa rejareja.
Huwezi kuwashutumu wenzako udini, ukabila na ukanda wewe usiwe nao. Unatumia vigezo gani kufikia hitimisho hili kama si kuwa muathirika mkubwa wa mabalaa?  Kwa wanaojua maana ya kukinzana na siasa huru, wana ushauri mmoja wa muhimu, ukiona wenzio hawakutaki si unakitoa na kwenda kule unakopendwa? Kwani chama ni baba au mama yako? Kwani lazima wewe na wenzako tu?
Ingawa ni mapema kusema, kinachoendelea ndani ya Chadema, ni matokeo ya kazi chafu ya ibilisi mwenyewe aliyewatuma wajumbe wake kwenda kuvurugu upinzani. Hamna kingine. Haiwezekani kuanze vurugu na miparurano wakati wa kujiandaa kuelekea uchaguzi. Hili si jipya. Tumewaona watoto wa yule mwovu wakivihama vyama wakati kama huu. Akina Steve Wassi—ra wanajua ninachosema hapa. Akina  Nsanzu—gwanko pia wanafahamu hili. Je watashinda?
 Wakati umefika kuwaambia wapinzani wa kweli kuwa muwe makini kwenye msafara wenu. Hamna tofauti na msafara wa Mamba ambao hujazana Kenge. Hivyo, kila mnapomgundua Kenge muonyeshe njia arejee huko kwa wenzake.
Situmii mfano wa Kenge kutaka kutukana au kudhalilishana. La hasha. Hii ni hekima ya wahenga ambayo tuliirithi wote. Kwanini Kenge aandamwe hivi? Nani hajui kuwa Kenge akiona mvua inaanza kunyesha hukimbilia majini? Akili au matope? Anyway, Kenge ni hayawani. Ila ni kujinyang’anya tunu ya ubinadamu kwa binadamu kutenda kama Kenge.
Kwa waliofuatilia sekeseke na mshike mshike kwenye Chama cha Chadema, walishangaa uvumilivu uliokuwa umechaguliwa na chama kama njia ya kujijenga. Huwezi kujijenga kwa kukumbatia Kenge ndani ya msafara wa Mamba.
Hakuna sehemu tulibaki kinywa wazi kama kwenye uchaguzi uliopita ambapo chama kilimsimamisha mwanachama wake kiliyeona amekidhi viwango vyake lakini mmoja wa viongozi tena wa juu wa chama akaamua kukisaliti na kumuunga mkono mgombea wa chama kingine. Hata kama chama kingekuwa kilikosea, kuna taratibu lakini siyo kukomoana na kusalitiana.
Wakati mwingine ni pale chama kilipotoa msimamo kama chama lakini baadhi ya viongozi wake wakakataa kusimamia msimamo wa chama. Kwa hili hata angekuwa mwalimu Nyerere asingevumilia kama walivyofanya Chadema.
Kwa vile siku zote huwa tunajifunza kutokana na makosa, wakati wa Chadema kutowaangalia nyani usoni umefika. Siasa za vyama ni kile wanachoita Waingereza to toe the line. If you can’t toe the line your political carrier in the party is on the line. Huwezi kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja.
Haiwezekani na kama ikiwezekana ni kwa muda tu. Ukigundulika unaadhibiwa bila kujali kuwa unajulikana au kukubalika. Kuwa na mawazo mbadala hata mkinzano si dhambi katika siasa za vyama. Kinachotakiwa ni kufuata utaratibu uliowekwa hata kama kinachodhamiriwa ni kubadili baadhi ya mambo chamani. Lazima kufuata utaratibu uliopo kichama na kisheria.
Kwa vile Chadema wameamua kuweka chama kwenye mstari, mengi yatasemwa. Wanapaswa kujiandaa kuyasikia haya na kukabiliana nayo vilivyo kama taasisi. Wabaya wao watawapakazia kila baya.
Watawakaribisha waasi kwenda kufanya nao biashara waliyokuwa wakiifanyia nyuma ya pazia kama njia ya kulipiza kisasa na kufanikisha kile walichokuwa wamekula njama kukifanya, kuwazuia kuingia madarakani.  Je watafanikiwa?
Itategemea na Chadema itakavyocheza karata zake hasa kuwaeleza wapiga kura nini kilikuwa kikiendelea ili waamue wenyewe. Je kupakaziana mabaya kutaondoa yale mabaya yanayojulikana kutendwa na wapinzani wa Chadema?
Je Watanzania ni majuha na wasahaulifu kiasi cha kuambiwa kuona tofauti ya ukweli wanaouona? Je nani huyu anayeweza kuwa mkubwa kuliko chama bado akaendelea kuwa kwenye chama hicho akitaka kitende atakavyo badala ya inavyotakiwa? Kuna haja ya kutafakari.
Wabaya wa Chadema wameishaandaa mabaya tena mengi tu. Lazima Chadema wajiandae kulisikia na kuliona hili kila siku hadi uchaguzi. Wabaya wa Chadema pamoja na mawakala na makuwadi wao waliojazana kwenye upinzani wataanza kutangaza injili ya udini na ukabila. Je wataweza kuzificha na kuzifunika zile za ubakaji, ufisadi, ujambazi, utoroshaji pesa na nyingine nyingi kama zinavyowaandama wapinzani na wabaya wao?
Tuhitimishe kwa kuwashauri Chadema kusimama kidete, kutenda haki na kuhakikisha demokrasia, kanuni na taratibu vinafuatwa ili kuepuka kutoa silaha kwa maadui ili wawamalize kirahisi. Ama kweli, kwenye msafara wa Mamba na Kenge wamo. 

Chanzo: Dira Novemba 26, 2013.

2 comments:

Anonymous said...

Huu ni mtazamo wangu mfumo wa siasa za afrika unatakiwa uendane na utamaduni wa watu tangu asili kabla kuja mkoloni halafu ufanyiwe marekebisho na watalaam wa wenye -maarifa ya kiafrika ya kisomi siyo wasoma wa vyeti ku-copy na ku-paste doctorate degress....

Baada yahapo tunaweza kuwa na mfumo kamili wa kisiasa hivi sasa naoa tunapamiapamia tuu hizi siasa za mifumo isiyokuwa ya kwetu. uthibitisho tangu mfumo vyama kuingia afrika.

Kikubwa kilichobadilika kuongeza ubadhirifu na rushwa pekee katika kiwango cha juu kabisa watalawa wakijigawia fedha za wizi bila aibu.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon nakubaliana na mawazo yako, tunahitaji mabadiliko ya kweli kweli kweli.