How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Saturday, 2 November 2013
Utabiri wa kifo cha CcM: Mlevi azimia
Hivi karibuni mlevi alikimbizwa hospitali. Ilibakia kiduchu angepumulia mashine kama Mandela. Hii ilitokana na kuwa na furaha kiasi cha kupita kiasi na kuanguka na kuzimia.
Baada ya munene JK kutoa utabiri wa kiama cha Chama cha Maulaji (CcM) ambao wakameruni huita self-fulfilling prophecy, yaani utabiri unaotimilika, nilikimbikia kupata kanywaji kujipongeza. Hata hivyo, nilishatabiri hili anguko takatifu na Nabukadnezza na Firauni.
Baada ya kunyaka nyuzi nilipiga kanywaji kama sina akili nzuri. Nani ambaye hangeshangilia kiama cha waliotusababishia kiama? Ukichanganya na mibangi si nikazimia kiasi cha kujikuta niko uso kwa uso na daktari.
Nani alinilipia fweza za kumdeku daktari na makandokando mengine ya walaji kama vile kumnywesha chai nesi au mtu wa mapokezi? Usiniulize. Huenda ningepelekwa Mwanamanyala pengine ningededi kwenye lango la hospitali ambayo imepata sifa ya kuwa mahali pa mauti badala ya uhai.
Hebu kwanza niwamegee kitu ambacho kilitaka kumnyotoa roho mlevi. Si munene JK baada ya kuona wenzake hawaelewi soma akaamua kupayuka. Ama kweli alaliaye kitanda ndiye anajua kunguni wake! Alipaaza sauti kama mtu aliyeko nyikani na kutabiri, “Kama (sisi walaji) hatutabadilika katika suala la rushwa mwaka 2015 tutakuwa na wakati mgumu sana na kama mwaka huo tutafanikiwa kuishika Sirikali, basi mwaka 2020 hatutarudi tena maulajini.”
Nasikia wakati akitoa utabiri huu mithili ya swahiba yake Shehena Yaya walaji wengi walikuwa wakitoa mimacho kama panya aliyenaswa mtegoni. Nasikia wapo waliozimia na kuzimika kutokana na kutoamini kuwa kumbe siku zao za kuwageuza walevi mabwege zinahesabiwa. Sijui munene JK alitembelewa na mzimu wa mzee Mchonga or what. Don’t ask me please.
Baada ya kuona somo halieleweki kutokana na kutumia lugha ya kinabii, munene Njaa Kaya sorry JK aliamua kuongea kwa lugha ya rahisi na moja kwa moja ili vihiyo na wagumu waipate. Alipaaza sauti tena akisema, “Amini amini nawambieni na mwenye akili atie akilini asiye nazo akaandae majili yake.
Viongozi wa chama ndiyo mmekuwa mawakala wa kusambaza rushwa bila hata aibu. Nawaombeni tubadilike, kama tutaendelea hivi hali yetu itakuwa ngumu sana katika chaguzi mbalimbali, nawaambieni.” Baada ya kusema maneno haya ya kishujaa viongozi wote walishusha macho yao kwa aibu huku wengine wakinong’ona, “Huyu jamaa mnoma. Kumbe ametugeuka! Tutakuwa wageni wa nani kama ulaji utatuponyoka?”
Munene alichukua glasi ya maji akanywa na kuendelea kunena, “Amini nawambieni na mwenye busara ayashike maneno yangu. Tukipoteza urais ndiyo tumekwisha na chama kinaweza kufa.” Hapa mlevi namuunga mkono mlevi mwenzangu munene. Maana urais ndilo rungu ambalo limekuwa likitumiwa na mwenyekiti wa chama kufanya madudu na kuruhusu ujambazi kuku na upuuzi mwingine kufanyika.
Nadhani hili likitokea hata wauza bwimbwi ambao munene aliwaminyia wataijua siri ya kuku kukosa haja ndogo. Nikikumbuka majambazi wa EPA, Richmonduli, Meremeta, SUKITA, Deep Green Finance, ANBEN, Kagoda na wengine bila kutumia rungu hili kuna watu wangekuwa Keko au Ukonga wakinyea debe kama siyo kuwa waliishanyongwa.
Alitikisa kichwa na kutoa mpya ambayo ilimuacha mlevi akilia kwa kuugulia hadi alipotishiwa kuwa bi mkubwa alikuwa anakuja ndipo akanyamaza. munene alisema, “Kuna watu wanapoingia mikataba sijui wanakuwa wamelewa...kwanza unashindwa hata kuelewa...kwa mfano utakuta mtu alipangishwa jengo la CcM kwa miaka 264 sasa unawaza huu mkataba wa aina gani kwa sisi tuliopo hapa, miaka 50 ijayo hakuna atakayekuwapo duniani, sasa mmiliki wa lile jengo atakuwa nani?”
Laiti angeelekeza akili zake kwenye mikataba ya madini na madude mengine yanayoingiza fweza kama mvua kama IPTL, Songas mbona angesababisha mlevi arejeshe namba kwa aliyemchonga kabla ya wakati wake! Baada ya munene kutamka mambo haya mazito nasikia kuna wanoko walianza kunong’ona, “Huyu hatunaye tena. Lazima aishie Chakudema vinginevyo tujiandae kushuhudia yale ambayo hayajawahi kushuhudiwa.”
Nasikia mlevi mmoja aliyekuwa akipita kwenye mkutano wakati munene akinena alisema, “Toboa baba japo umechelewa. Kwanini hayo hukuyaona miaka ya mwanzo ya ulaji wako na kuwatia adabu wenzio au kamba? Mbona unaongelea rushwa lakini si ujambazi na wizi kama EPA?” Nasikia kabla ya kuendelea kupayuka ndata walikuja wakamziba mdomo (asiwaumbue wakubwa) na kwenda kumbambikizia kesi.
Baada ya kuona somo linazidi kuwa gumu munene aliamua kuchukua maji na kunawa mikono kama alivyofanya Pilato akisema, “Wapo watu ambao wanadai kuwa chama kitafia mikononi mwangu, nataka niseme kuwa hakifii mikononi mwangu, kitafia mikononi mwenu.” hapa kilichowazi ni kwamba chama lazima kusulubiwe bila huruma kwani hakina maana wala mtetezi. Nafikiria ile siku chama kitapokuwa kimewekwa msalabani kikilia Munene Munene mbona waniacha? Tazama naiweka roho yangu chafu mifukoni mwako.”
Hebu tuseme ukweli kidogo. Munene alivyokula hakumaliza waliomaliza ni wale walioiweka kaya mifukoni mwa mafisadi ingawa naye alishiriki karamu hii haramu. Sasa ukisikia wakati wa kuchimbika bila jembe na kutotosha ndiyo huu. Walevi kaeni mkao wa kula maana mmeliwa sana. Wametula lazima nao waliwe bila huruma.
Munene ameamua kutubu tena kwa kutoboa. Je upande wa pili unaotuaminisha kuwa unaweza kupewa ulaji wasile wao tule sisi mbona nasikia wengine wana hata mahekalu huko kulikoungua shoka ukabaki mpini? Nadhani wale jamaa zangu wenye mahekalu Dubai, akaunti Uswazi na Jersey mnanideku. Mlevi sina chama wala ushabiki. Nakata huku na kule kama msumeno.
Laiti wanene wa Chakudema nao wangekuja na kitubio chao tungewaelewa. Wale wenye NGOs wanazoita vyama sina haja nao. Waje tupige kanywaji na mibangi waachane na mateso kama alivyosema munene tujipe raha wenyewe. Hakuna haja ya kuishi kwa matumaini ya kukamata dola wakati hata Dola za wafadhili mkizipata mwakimbizia Uswazi.
Wale walevi wanaosema eti watagombea ulaji hadi wafe wakigombea au watimliwe kwa mawe na walevi sina haja nao. Walishapigika. Hawana sera. Wanaganga njaa. Joni Cheo, August Lyatongolwa, Maalimu Nonihii na wasasi wengine wa ngawira mpo?
Kifo cha CcM kinakumbusha mbwa wangu wenye majina ya kizungu Tamba, Jerome, Stanley na Ray ambao niliwanunua Kimbush. Baada ya kugundua wananiibia si niliwapiga nyundo.
Mlevi anashauri walevi wasingoje CcM ijifie bali waidedishe as soon as possible ili wakombolewe. Uliwaambia wajiandae kisaikolojia wakagoma. Sasa wamalize kisaikoloji. Such spiffy prophecy makes me feel like flying with joy and relief. RIP CcM.
Chanzo: Nipashe Jumamosi Nov. 2, 2013.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment