HIVI karibuni mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe ameonyesha njia kwa kushikilia bango mabilioni ya shilingi yaliyofichwa kwenye mabenki ya Uswiss wakati Serikali ikijifanya haihusiki.
Kama jamii na wananchi waathirika tunapaswa kuunga mkono juhudi za kufichua, kuumbua na kushughulikia walioiba pesa yetu na kuificha nje ya nchi. Hii pesa ni yetu hata kama hatutaki kuliona hili hivyo.
Wizi wa namna hii ndicho chanzo cha umaskini wetu. Kwani wezi wahusika wanaiba kodi na misaada yetu na kutufanya maskini. Bila wananchi kuamka na kutaka hatua zichukuliwe, tutaishia kwenye siasa kama zile tunazoshuhudia kuhusiana na wauza unga, mafisadi na sasa majambazi wa kimataifa.
Tuliambiwa kuwa bunge liliunda kikosi cha kuchunguza tuhuma hizi na kuleta majibu kwa bunge. Muda uliowekwa umepita na hakuna anayeuliza wala kuudhika kuwa bunge limedanganywa, taifa limedanganywa na uongo unaendelea. Je nini mantiki ya kuwa na serikali? Serikali ipo madarakani si kwa sababu inapenda kuwa madarakani. Ipo madarakani kwa ridhaa na uwakilishi wa wananchi.
Pia inashangaza kusikia kuwa tumeshikia bango kwa pesa iliyofichwa Uswiss wakati kuna nchi nyingine pia ambazo ni kimbilio la wezi wetu. je ina maana serikali pamoja na asasi zake za kiusalama haikujua wizi huu hadi waswizi wataje?
Je nchi ambazo hazijataja zitanyamaziwa ili pesa yetu iendelee kuhamishwa toka Uswiss kwenda kule? Nchi zinazotajwa ni Dubai, Mauritius, Uingereza, Cayman Island. Siamini kama ni hizi nchi pekee. Kuna uwezekano zikawapo nyingine nyingi. Hili ni jukumu la vyombo vyetu vya usalama kulishughulikia na kutuletea taarifa sahihi na za uhakika.
Kwa upande mwingine wananchi ndiyo wenye nchi na hata serikali ingawa wamejigeuza watazamaji huku pesa na mali zao vikiteketea kana kwamba hawaathiriki. Je tatizo ni ujinga au woga? Kwa faida ya nani?
Je serikali isiyowajibika wala kuwatumikia wananchi kweli ina mamlaka na uhalali wa kuendelea kuwa madarakani? Je hayo mabilioni ya shilingi yangejenga viwanda vingapi au kujenga barabara na shule na hospitali ngapi? Je kweli sisi ni maskini au ni maskini wa kujitakia kutokana na ukimya wa wananchi kujifanya wizi wa pesa yao hauwahusu?
Hivi karibuni Kabwe alikaririwa akisema kuwa mamlaka za Uswiss zimebadili hata sheria ili kusaidia nchi athirika ziweze kurejesha pesa iliyoibiwa. Ajabu pamoja na nchi tajiri kama Uswizi kutuonea huruma kama nchi maskini, viongozi na serikali zetu zimekataa kutumia sheria hii iliyorekebishwa kurejesha pesa hii. Kwanini? Je wahusika ni miongoni mwa walioficha pesa nje?
Ingawa hajaionei huruma, huwa namuonea rais wetu kwenda kila uchao nje kapu mkononi akiomba jambo ambalo ni aibu kwake na kwa taifa lenye kuweza kuwa mshipa wa kunyamazia pesa iliyoibwa kwa mabilioni na kufichwa nje. Je rais ananufaika vipi na kadhia hii? Ni hiyo per diem anayolipwa anapokwenda kuomba wakati akipuuzia pesa kwa mabilioni iliyofichwa nje ikiwasaidia watu wa nje tena matajiri?
Kwanini rais hatambui kuwa hii pesa inayoibiwa ni kodi ya muuza vitumbua, karanga, machinga, mkulima na mfanyakazi mdogo ambaye amepigika kimaisha. Je huyu rais yupo kweli kwa maslahi ya huyu mwananchi wa chini au mafisadi?
Sambamba na Kabwe, Kila mara serikali kupitia waziri wa fedha wamekuwa wakitwambia kuwa kurejesha fedha zilizofichwa nje kunawezekana kutokana na kuwepo sheria za kufanya hivyo.
Je tatizo ni nini kama sheria hazitumiki? Hivi karibuni waziri wa fedha Dk William Mgimwa alikaririwa akisema, “Lengo la sheria hizi za kimataifa ni kuhakikisha kuwa fedha za wizi zinazoibwa nchi fulani, haziwezi kuhifadhiwa katika nchi nyingine.”
Kumbe waziri anajua kila kitu ila anakosa utashi wa kuzitumia sheria husika kurejesha pesa yetu? Sijui kama nafsi yake haimsuti kusema haya aliyosema na kutenda tofauti na inavyopaswa kuwa. Naye rais wa Uswiss Maya Graf alisema, “Serikali ya Tanzania inatakiwa kuweka mkakati wa kisheria utakaotengeneza mazingira ya kubadilishana taarifa za fedha na mataifa mengine. Kwa jambo hilo hata Serikali ya Uswisi inaweza kusaidia katika kupatikana kwa fedha zilizofichwa.”
Kwanini kuwaangusha wananchi wetu ambao licha ya kujifunga mikanda wanachapa kazi kwa moyo wote ili wajikwamue?
Je wataweza kujikwamua wakati serikali yao inawaangusha kwa kuwanyamazia majambazi walioficha pesa nje? Kuna haja ya wananchi kutoka kwenye usingizi na kuamka na kuibana serikali iwatendee haki kwa kupambana na ujambazi na ufisadi ambavyo vimeweka mazingira mazuri kwa kikundi kidogo cha wezi kutugeuza shamba la bibi.
Kuna kipindi mtu akiangalia yanayotendwa na mamlaka zetu hasa wizara ya fedha anakosa mantiki ya kuwa na wizara na mamlaka husika. Nikikumbuka sakata la Richmond, EPA, Kagoda na kashfa nyingine zilivyomalizwa kijinai na benki, nakosa mantiki ya kuwa na wizara hii. Utakuta pesa hiyo pesa kwenye kashfa tajwa hapo juu iko inawanufaisha wazungu matajiri kule Uswiss huku walioizalisha yaani wakulima na watu hohehahe wanateseka.
Kama haitoshi likija suala la misamaha ya kodi kwa makampuni matajiri utaigusa hiyo hiyo wizara ya fedha. Kwanini tusiifute tukaumia na kujua kuwa hakuna wizara husika? Kuendelea kuwa na mamlaka zinazosaidiana na wezi ni sawa na kisa cha mfugaji wa kuku aliyefunga mbwa kupambana na vicheche waliokuwa wakimwibia kuku.
Mkulima aliamua kumnyonga yule mbwa baada ya kugundua kuwa kumbe kazi yake ilikuwa ni kula vifaranga na kuwaacha vicheche wakamate vifaranga watakavyo. Kwanini wananchi wanajiruhusu kuwa kama huyu mkulima mpumbavu wasiitwe wapumbavu? Je wananchi hawajui kuwa pesa inayoibiwa na madaraka yanayotumika kuwalinda na kuwapuuzia wezi wao ni yao waliyokasimu kwa serikali?
Tuhitimishe kwa kusema kuwa wananchi wanapaswa kulaumiwa sambamba na serikali na wezi wa pesa iliyofichwa Uswiss tokana na ukimya wao na kujifanya hayawahusu. Pia tunamshauri waziri wa fedha na asasi husika zijaribu kusoma alama za nyakati.
Hatuwezi kuendelea na business as usual kwenye uhujumu wa taifa. Wahusika wafikishwe mahakamani na pesa yetu irejeshwe vinginevyo tuiwajibishe serikali bila kusikia visingizio vyovyote.
Chanzo: Dira Nov., 11,2013.
2 comments:
Kurejesha pesa ni sahihi, Je kuna juhudi gani kuzuia pesa kutoroshwa tena!
Sidhani kama kuna juhudi zozote zaidi ya watawala kuzidi kutorosha nyingi zaidi. Ni balaa. We will soon become a failed state economically.
Post a Comment