How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 18 February 2014

Suluhu ya ujangili iko Ikulu si London

JAPO ni jambo jema kwa dunia kupambana kama kijiji kimoja kutokana na utandawazi, bado si kila jambo linahitaji utandawazi.
Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alikuwa mjini London kuhudhuria mkutano wa kujadili namna ya kuokoa faru na tembo wanaoangamizwa na ujangili wa kimfumo barani Afrika.
Wapo waliosifia ushiriki na hotuba yake wasijue maneno matupu hayavunji mifupa. Waswahili wana busara. Husema: ‘Simbuliko halisimbuliki hadi kwa mikukuliko.’
Busara hii inaweza kuwa kweli kwa Rais Kikwete na harakati zake za ‘kupambana’ na ujangili kwa njia ya kuupamba.

Wanaojua jinai, wanajua fika. Suluhu si kwenda London wala si shinikizo la Wazungu bali uzalendo na hiari ya watawala wetu.
Kwa mujibu wa gazeti la The Mail on Sunday la Uingereza la Februari 8, tembo zaidi ya 10,000 waliuawa nchini.
Gazeti liliandika: “Utawala wa Rais Kikwete umetawaliwa na mauaji ya tembo … wahifadhi wanasisitiza kuwa, ndani ya serikali kuna viongozi wanaoshiriki biashara hiyo… miongoni mwao ni matajiri wakubwa nchini, wafadhili na wanachama wa CCM na ndugu wa karibu wa Rais Kikwete.
Lakini vyombo vya dola, majaji, waendesha mashtaka na polisi hurubuniwa kwa urahisi.” Lisemwalo? Wengi hawaoni mantiki ya Kikwete kutangaza ‘vita’ dhidi ya ujangili kama anaishiriki.
Mbunge Peter Msigwa (Iringa Mjini) ameliona hili alipokaririwa akisema: “Inakuwaje mtu anayevunja sheria za nchi hakamatwi? Waziri Lazaro Nyalandu amekuwa mlalamikaji badala ya kutafuta suluhu, majibu yake na ya Serikali ya CCM yanadhihirisha kuwa mtandao huu unaoogopwa unaihusisha Ikulu, wanasiasa, polisi, maofisa wanyamapori na wanajeshi."
Je, Msigwa ni mzushi au doomsayer au maneno yake yana ukweli?

Kwanza, baada ya kutolewa shutuma, serikali haikuhangaika kutoa maelezo au kukanusha. Hii inaweza kuchukuliwa kuwa shutuma zina ukweli ambao serikali ikijidai kupinga unaweza kufichua mengi.
Msigwa si mwendawazimu wala mzushi. Ilichofanya serikali ni kunyamaza ili shutuma za Msigwa zijifie. Hii mbinu ilitumika kwenye shutuma za kuhujumu viwanda, madini, EPA, Richmond, UDA, Meremeta, Mwananchi Gold, IPTL na jinai nyingine.
Pili, waliofuatilia ‘vita’ dhidi ya ujangili chini ya Operesheni Tokomeza Ujangili, wanaweza kukubaliana na madai ya Msigwa kuwa serikali inawajua majangili wakubwa ambao wengi wamo serikalini humo humo.
Kimsingi, kilichofanyika wakati wa ‘Operesheni’ hii ni kuivuruga ili kupata kisingizio cha kuachana nayo kutokana na kuelekea kuwaumbua wakubwa wanaofaidika na jinai hii.
Hivyo, badala ya kufuata taratibu, polisi na jeshi walioamriwa kutekeleza operesheni hii walivuruga na kuvunja haki za binadamu makusudi ili itokee sababu ya kusitisha zoezi ambalo lilikuwa linaelekea kuwaumbua wengi.
Hata hivyo, wengi walishangaa kuona eti mawaziri wanne wanawajibishwa kutokana na kuvunja haki za binadamu wakati Tanzania haina rekodi ya kujali wala kusimamia haki za binadamu.
Nani mara hii kasahau, mfano, jeshi hilo hilo la polisi linalosifika kwa kuua watu wasio na hatia kila mwaka hakuna mkuu wala polisi aliyewahi kuwajibishwa?
Nani amesahau matukio ya juzi juzi ambako mwandishi wa habari, Daud Mwangosi, aliuawa na polisi na Mkuu wa Polisi wa Mkoa, Michael Kamuhanda, aliyesimamia mauaji haya alipandishwa cheo na si kuwajibishwa? Haya mapenzi ya haki za binadamu yameanza lini kama si kutaka kukwepa kuwaumbua vigogo?
Tatu, wanaojua tabia ya Rais Kikwete na serikali yake ya kulinda na kushiriki ufisadi, hawashangai kusikia shutuma za Msigwa. Rejea alivyowaaminisha Watanzania kuwa anazo orodha za majina ya wauza unga, wala rushwa, majambazi hata vidokozi bandarini na asiwachukulie hatua.
Hivyo, kwa wanaomjua Kikwete na jinsi alivyoingia madarakani akishutumiwa kutumia pesa iliyokwapuliwa kwenye fuko la madeni ya nje la EPA, hawashangai kuona anavyofumbia macho jinai hii kwa vile anaweza kuwa mnufaika kama si yeye basi watu wake.
Msigwa anasema wazi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amekuwa mlalamikaji. Ni kweli. Kwanini asilalamike iwapo ameshuhudia yaliyompata aliyemtangulia, Khamis Kagasheki, ambaye alikuwa bosi wake?
Kwanini asigwaye iwapo yeye amenusurika kutokana na ukaribu wake na Kikwete? Kwanini asigwaye iwapo anajua fika kuwa ukigusa masilahi ya wasioguswa unaondoka wewe?
Kwanini asigwaye na hii “none sense, crap and malicious” kwa kuazima maneno ya Salva Rweyemamu, mpambe wa Kikwete, iwapo wanaopaswa kuhusika wanafanya nonsense, crap and malicious politics kwenye masilahi ya taifa?
Wengi wanashangaa upotezaji wa muda na fedha ya wananchi kwenda eti London kuhudhuria mkutano wa kuzuia ujangili wakati ujangili anaufuga yeye.
Hebu muulize Kikwete wale waliosafirisha wanyama hai kupitia Uwanja wa Ndege wa Kia Novemba 24, 2010 ambapo ndege ya kijeshi ya Qatar ilifanikiwa kutorosha wanyama mbalimbali 130 tena wengi wao wakiwa hai na wakubwa kama vile twiga wamefanywa nini?
Wengi wanashangaa serikali yenye vyombo vya ulinzi na upelelezi kutoweza kugundua wala kushughulikia jinai hii. Hii maana yake ni kwamba serikali ama haipo au inahusika.
Ukiachana na hili la kutorosha wanyama hai mchana kweupe, hivi karibuni kumetokea matukio ambapo raia wa kigeni hasa kutoka Uchina walikamatwa na pembe za ndovu nyingi tu.
Ajabu majangili hawa wanaingia nchini kama wawekezaji kumbe lengo si uwekezaji bali ujangili na bado wanalindwa na serikali hii inayosifika kulala kitanda kimoja na wahalifu.
Nani mara hii amesahau jinsi wawekezaji wanavyoiba madini yetu na serikali isifanye lolote kutokana na wale aliowataja Msigwa kuwa nyuma ya jinai hii?
Baada ya pembe za faru na ndovu kuwa na soko sawa na madini, wahalifu hawa wameamua wajiongezee kipato kwa kumaliza wanyama wetu.
Tukiondoa utegemezi kwa wakoloni ambao hata hivyo wana sifa moja kuwa walikuja wakatuibia lakini wakatubakishia kile ambacho tunajiibia na kukimaliza, suluhu ya kupambana na ujangili iko Ikulu na si London.
Tembo na faru hawawezi kuuawa Tanzania suluhu ikapatikana London. Wanaotaka kuokoa faru na tembo wamwambie Kikwete aache kuwalinda wale aliowataja Mchungaji Msigwa vinginevyo kinachoendelea ni danganya toto na usanii kama kupambana na mihadarati na ufisadi. Ujangili ni aina fulani ya ufisadi pia.
Chanzo: Tanzania Daima Feb. 19, 2014. 

2 comments:

Jaribu said...

Bwana Mkubwa kama kawaida yake, badala ya kuelezea hatua atakazochukua, anasema ana "orodha" ya majina 40. Naona kabati lake litakuwa limejaa orodha za kila namna. Labda itabidi amwite Ms Business Study amfanyie filing.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Huyu bwana si vibaya tukisema ana ugonjwa wa kujisahau na kuongopa. Maana kabla na hata baada ya kutuingiza mkenge akaukwaa hajawaahi kusema ukweli hata siku moja. Ni balaa ambalo litaingia kwenhye vitabu vya historia chafu ya taifa letu so to speak.