Juzi
nilifurahi sambamba na kuchukia. Ni pale runinga ya Afrika Kusini ilipoonyesha
kuwa uchumi wa Tanzania utakuwa kwa kasi kuliko chumi zote duniani miaka
michache ijayo. Baada ya kuona hili nilianza kuangalia uzuri na ubaya wa kukua uchumi
kwa kasi kwenye taifa linaloongozwa kifisadi. Je uchumi wetu utakapokuwa nani
atafaidi kati ya wananchi na makuwadi wa wawekezaji ambao wamehakikisha kila
kitu kinawanufaisha wao na mabwana zao? Rejea kugundulia utitiri wa madini
ambao matokeo yake ni utitiri wa mashimo na kashfa kiasi cha kuwaacha watu wetu
maskini na wakimbizi kwenye nchi yao. Nani amesahau mauaji ya watu wasio na
hatia kule Mara kwa kosa la kukatisha kwenye mgodi? Nani amesahau magonjwa ya
hatari yanayowasumbua wakazi wa huko huko Mara ambao kemikali zimenyiririshwa
kwenye vyanzo vyao vya maji?
Je
kuna haya ya walalahoi kushangilia habari hii au kuomboleza kwani kukua kwa
uchumi wa Tanzania kwao ni chachu ya kukua kwa umaskini? Hivi unategemea nini
toka kwenye nchi inayogawa raslimali zake bure au kuharibu mali za umma kama
vile kuuza mashirika ya umma kwa bei ya kutupwa kama ilivyotokea kwenye uuzaji
wa iliyo kuwa Kampuni ya Usafiri Dar es salaam (UDA), NBC na mashirika mengi?
Taarifa za ukuaji wa uchumi wa Tanzania zilizotolewa
mwaka 2012 na Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu,
Morrice Oyuke zilionyesha kuwa uchumi wa Tanzania ungekuwa kwa asilimia 7.1.
Hili ni jambo la kujivunia. Kinachogomba ni kwamba huyu mtakwimu hakueleza ni
kiasi gani umaskini utakuwa. Wapo waliosema kuwa umaskini ungeongezeka kwa
asilimia 5 na ushei sambamba na ukuaji huu. Je hii inatoa picha gani? Wapo
wanaoona kama takwimu tunazoletewa ni za ungo wa kawaida. Na hii inaweza kuwa
kweli hasa tukizingatia jinsi takwimu zinavyoweza kuficha ukweli kama
alivyowahi kusema, Joel Best kwenye kitabu chake cha Damned lies and statistics, “Mujumuisho ni hatua muhimu katika
kufikiri kitakwimu. Mara chache twaweza kuhesabu matukio haya yote ya kijamii. Badala
yake, tunakusanya baadhi ya ushahidi kutokana na sampli na kutoa hitimisho la
jumla,” (uk.6). Sambamba na hili Benjamin Disraeli (1804–1881) waziri mkuu wa Uingiereza
aliwahi kusema, “There are three kinds of lies: lies, damned lies, and
statistics.” Hatuna tafsiri ya nukuu hii. Pamoja na kwamba si takwimu zote zinaficha
uongo, kuna haja ya kuwa makini na takwimu hasa katika kuzilinganisha na ukweli
halisi. Kwa wanaojua udhaifu wa takwimu,
wanajua ninachoongelea hapa. Takwimu zinaweza kuonyesha picha tofauti na hali
halisi kama ilivyo kwenye suala la kukua uchumi wa taifa. Ukitaka kujua uongo
wa takwimu hebu nenda vijiji uangalie aina ya maisha wananchi wanayoishi. Huwezi
kukuza uchumi kwa takwimu bali uzalishaji na matumizi bora na nidhamu ya pesa
na raslimali za umma jambo ambalo ni msamiati mgeni nchini. Huwezi kukuza uchumi kwa midomo au kisiasa au
kwa kupika takwimu. Mwandishi wa makala hii ni muumini wa dhana tofauti na
takwimu. Anaamini kuwa ukuaji wa kweli wa uchumi hauelezeki kwa takwimu tu bali
unaweza kuelezewa vizuri na wakati maskini wa vijijini au mabandani mijini. Hali
za maisha ya makundi haya ya wasio nacho zinaweza kutupa picha nzuri na ya
kweli kuhusiana na kukua kwa uchumi. je wanapata huduma bora? Je wanaridhika na
mambo yanavyokwenda? je wanashirikishwa kikamilifu? Je wanawezeshwa? je
wanapewa taarifa muhimu? je wana welewa wa taarifa husika kiasi cha kuzichambua
na kuzifanyia kazi ikiwamo na kuzikubali au kuzikataa? Haya ndiyo mambo ya
kuzingatia katika kutoa tafsiri ya kukua kwa uchumi. Je waliotoa taarifa za
ukuaji wa uchumi wetu wameyazingatia haya? Jibu ni hapana tena kubwa tu.
Kwa
wanaojua udhaifu wa uwekezaji nchini, bila shaka wanategemea ongezeko la
wamachinga wanaojiita wawekezaji toka India, Pakstani, Bangladesh, China na
kwingineko. Pia wanategemea utoroshaji wa mtaji na raslimali kuongezeka
kutokana na mamlaka zilizopo kupoteza muda kwenye kusaka rushwa badili ya
kukusanya mapato na kubana mianya ya kutorosha mitaji na mali za umma. Uliza
madini kama Tanzanite yameisaidia nini Tanzania zaidi ya kuwa laana na msaada
kwa nchi jirani ya Kenya na India?
Je
uchumi wetu utakuwa kiuchumi au kisiasa? Kwa wanaojua ukuaji wa uchumi wa
kisiasa ambao ulielezewa na rais Jakaya Kikwete aliposema kuwa ukiona mitaa
yetu finyu imejaa misongamano ujue uchumi umekuwa kiasi cha watanzania wengi
kuwa na mikangafu. Tofauti, ukuaji wa kisayansi ni ule unaowezesha nchi
kuongeza pato lake na kupunguza utegemezi katika misaada au kuagiza zaidi ya
unavyouza. Je Tanzania nchi iliyojaa bidhaa zilizo chini ya viwango kutoka India
na China kweli inaweza kuwa na ukuaji wa kujivunia kwa watanzania?
Tujalie kuwa uchumi wetu
kweli utakua, je utafua dafu kwenye matumizi mabaya ya kisiasa ambapo
tumezalisha mikoa na wilaya nyingi kukidhi mahitaji ya kisiasa badala ya
matakwa ya wananchi? Je ukuaji huu
uliotabiriwa utaondoa au kupunguza uombaomba wa nchi yetu ambapo bajeti yetu
hutegemea michango ya wafadhili kana kwamba hatukujaliwa raslimali?
Tukifie mahali tuuangalie
ukweli kama ulivyo kwa kujitenga na kujipigia debe kisiasa ili wahusika
wachaguliwe tena wafanya madudu tena. Swali linalopaswa kuulizwa na kujibia kwa
utuo ni: Je uchumi wa Tanzania unapimwa na nani na nini katika ukuaji wake? Je
ukuaji, kama upo, unamnufaisha nani na vipi?
Ukuaji wa uchumi
unaowaacha nje maskini ambao wanaona umaskini na uduni wa huduma vikiongezeka
hauna maana. Watawala wetu wanapaswa kufikiri kabla ya kutuletea takwimu za
ajabu ajabu zilizokaa kikampeni zaidi ya sayansi. Je inakuwaje uchumi wa Tanzania
unakuwa sambamba na umaskini?
Chanzo: Dira Feb., 2014.
2 comments:
Miaka kumi iliyopita £1.00 ya Uingereza ilikuwa na sawa na thamani Tsh 1450.00.. Leo hii £1.00 ni sawa na Tsh 2700.00.
Je unahitaji kuwa Professor au ma-Dokota(Dr) kutafsiri hizo takwimu zinatolewa kuhusu maendeleo ya uchumi wa Tanzania...!
Mimi katika familia yangu miaka nane iliyopita ilikuwa angalau kulikuwa na watu nne wakiwa na ajira ya kudumu. Leo hii hakuna hata mmoja kwenye ajira ya kudumu.
Kama unavyojua ile kamati yetu iliyoundwa na Mr ambaye mara nyingi anawasema watanzania ni wavivu wa kufikiri ambapo yeye amekuwa madarakani katika ngazi tofauti na kupanda vyeo mpaka kufikiwa kuwa Rais.
Hivyo udhaifu wa kufikiri ninapozungumzia unaanzia wapi kama si kwake yeye mwenyewe na kuendelea hadi ngazi ya chini. Ushahidi yeye alikuwa madarakani kipindi kirefu tuu na nchi imeendelea kuwa maskini na huduma duni za kijamii siku hadi siku. Hata kamati yake aliyounda ni uthibitisho kuwa naye yeye ni mvivu wa kufikiri
Kamati iliundwa kwa jina la kurekebisha/ubinafsishaji mashirika umma lakini kilichokuwa kinafanyika ni uvivu wa kufikiria kama ambavyo Mr msataafu Rais anavyofikiri kuhusu uvivu wa kufikiri kwa sisi Watanzania...yaani kuuza kila shirika badala ya kurekebisha tena kwa bei chee au buree wakti mwingine.
Kifupi hizo takwimu za maendeleo ya uchumi ni sawa kupakwa mafuta kwa mgongo wa chupa! Mpaka sasa Wagonjwa wanalazwa sakafuni au kutimia kitanda kimoja wagonjwa wawili...Vyoo vya umma au hospitali imekuwa sehemu ya kuweka uchafu badala kupitisha uchafu
Au Kama Bwana JK aliposema hivi karibuni akutukanaye akuchagulii tusi(ingawa yeye alikuwa akijaribu kubishana na ukweli) kuubalisha kimaoni kuwa ni uwongo ingawa kila kitu kilikuwa katika video kuhusiana na mahuaji wanyama pori hasa tembo na faru na wahusika katika hiyo biashara
Anon,
Wasomaji wangu wakifumba mimi hufumbua. Bila shaka huyu unayemaanisha si mwingine ila Benjamin Mkapa rais wa hovyo aliyesifika kwa majivuno, kupayuka na kutawaliwa na kutumiwa na mkewe. Ni Mkapa huyu huyu aliyetuuza kwa wawekezaji hata mafisadi alipoasisi wizi wa EPA uliomuwezesha Dr Zero kuukwaa urais ambao ameugeuza urahisi wa kufanya ufisadi. Nakubaliana nawe kuwa huyu bwana ni bingwa katika uvivu wa kufikiri na alichosema ni kama alikuwa akijipiga kijembe bila kujua. Ila kwa vile yu mvivu wa kufikiri hakujua kuwa alikuwa akijisimanga mwenywe.
Post a Comment