WIKI iliyopita Kijiwe kilimkumbuka nguli mwalimu Julius Mchonga. Japo wale waliowatengeneza, kuwatengenezea na kuwaachia ulaji walimtosa baada ya kuwa wakimsanifu kila mwaka, sisi tulimkumbuka kwa dhati na kweli. Kwa kuendeleza mapambano ya kuleta haki na usawa aliyoanzisha mzee Mchonga, Kijiwe kimepanga kutoshiriki kwenye uchakachuaji wa kupitisha katiba feki iliyoacha maswali mengi kuliko majibu.Kama wamechakachua Idodomya watashindwa nini kuendelea na ujambazi huu?
Leo Msomi amewahi kijiweni kuliko wote. Inaonekana ana jambo linalomkera. Maana hata usoni hana bashasha kama kawaida.
Baada ya kujiridhisha kuwa ni wakati muafaka wa kuanza mada, anajiweka vizuri kwenye benchi na kusema, “Mwenzenu usiku sikulala vizuri. Maana nilikuwa nawaza jinsi ya kuepusha kaya yetu kuingizwa mifukoni mwa mafisadi hasa kwa kuwapa kibali cha kuendelea kutugeuza mabunga na kitoweo chao kupitia kushiriki kinachoitwa kura ya kupitisha katiba mpya ambayo si mpya chochote bali kiini macho na maigizo ya kitoto na kishenzi. Sijui wenzangu mnasemaje?”
Mijjinga anakuwa wa kwanza kula mic, “Msomi una hoja na umefanya vizuri kuweka jambo hili hapa mezani. Nadhani kabla ya kuamua kushiriki hiki kiini macho, tungepewa kwanza maelezo ya escrow na namna watakavyoziba pengo la fedha waliyogomea wafadhili.”
Anapiga chafya na kuendelea, “Unaona hata chafya inakataa! Hata wafadhili wamegoma kugeuzwa shamba la bibi kwa kutoa njuluku zinazoishia kuliwa huku wanaofanya hivyo wakiendelea kujitia hamnazo, wakiomba waongezewe waibe zaidi.”
Kapende anakwea mic, “Nangoja kumsikia yule kihiyo Masele akiwabwatukia kama alivyosema kwenye skandali ya Escrew. Pia nangoja kusika kauli ya mjivuni Mura Werema kuhusiana na kuumbuliwa huku. Nakumbuka alivyomtishia balozi wa Uswazi kuhusu njuluku zilizofichwa kule. Sijui nazo zimeishia wapi. Ajabu hata Njaa Kaya anajifanya kutosikia joto ya jiwe!”
Msomi anadakia, “Asisikie joto ya jiwe yeye nani? Nadhani anachofanya ni kungoja mambo yapoe aende kuwaramba miguu wamsamehe japo amalize ngwe yake. Tena kabla sijasahau, mmesikia skandali yake ya kuhongwa saa ya Rolex na tapeli aliyempa ubalozi wa heshima wakati si chochote wala lolote bali mwizi wa kawaida?”
Mgosi Machungi anajibu, “Tangu jamaa ahongwe suti tilimzalau. Usishangae kashfa hii ikafutikwa chini ya busati kwa kuleta sanaa nyingine. Wako wapi waiokwepa njuuku Uswazi? Nani anajai?”
Mipawa ameng’ang’ania rasimu ya Waryuba. Anakula mic, “ Kukata mzizi wa fitina lazima turejeshewe rasimu orijino ya jaji Waryuba vinginevyo kushiriki huu upuuzi ni sawa na kujitia kitanzi kwa hiari ya kura zetu ambazo bila shaka zitachakachuliwa na kudharauliwa kama ilivyotokea Idodomya walikododomya demokrasia na rasimu orijino ya wadanganyika.”
Mgosi Machungi anapoka mic, “Waioihujumu na kuhaibu fedha yetu wafungwe maisha. Hatiwezi kupoteza mabiioni ya kuwapa hao waliokutana kutuibia na kudharau na kuchakachua mawazo na haki yetu haafu watu wakaendelea kuturingia mitaani baada ya kuwapa kura zetu. Mimi sishiriki hata kama ni kwa kutiwa kitanzi.”
Mpemba anakwanyua mic, “Waliohusika wote wasiruhusiwe kushiriki na wajiuzulu ili watu safi wachukue nafasi zao. Maana twachezewa mahepe nchana kweupe. Tukataeni jamani.”
Kapende anakwanyua mic, “Hawa wajivuni na mafisadi wanaodhani yamekwisha wajue ndiyo yanaanza. Tusishiriki zoezi la kuhalalisha haramu yao huku tukiweka saini hati ya kifo cha kaya yetu na vizazi vijavyo. Tunataka katiba kweli lakini iwe mpya na itokanayo na utashi wetu na si nguvu na hila za mafisadi na wezi wa mchana. Katiba lazima iongelee ufisadi kwanza maana haya mambo ya kuhongana kila upuuzi na kuuza kaya hayavumiliki.”
Mbwamwitu anakula mic na kusema, “Acha nikuongezee. Katiba lazima itangaze kuwa na kaya moja na si vipande vipande kama ilivyo. Hivi kusingekuwa na kipande cha zenj huu ujambazi wa kura ungefanikiwa vipi?”
Mpemba anaguna na kusema, “Wallahi heri kila mtu aende kivyake ati kama mwataka tuwe kaya moja.”
Bi Sofia Lion aka Kanungaembe kapata upenyo! Anazoza, “Nanyi mkienda kivyenu mtasambaratika. Hapa najua ami anataka Pembe iende kivyake na Zenj hivyo hivyo.”
Kanji anakamua, “Kama vunja ungano tapata tabu sana. Mimi iko ona India na Pakistan. Ilipovunja ungano lianza gombania witu howo howo. Hiwo mimi sema hapana tengana. Kama nataka amani basi fanya kaya moja yote iwe sawa.”
Mpemba haridhiki, “Wafahamu? Hata hawa mahabithi walochakachua rasimu walitaka epuka hili wasijue ndo walipa nguvu. Kama tungekuwa na sirikali tatu maana yake kila upande ungepata nguvu na uchaguzi wa kuendelea au la. Sie twataka sirikali tatu ili kila mmoja aheshimu mwenzie ati.”
Mheshimiwa Bwege alikuwa kimya kitambo. Anaamua kutia timu, “Mie naona wote hamjakosea. Kinachopaswa kufanyika ni maridhiano na makubaliano. Kama wachovu wangetaka hata sirikali mia nyie yawahusu nini. Ajabu eti wale wanaowaibia wanawadanganya kuwa sirikali tatu zitaongeza gharama. Mbona wanapochora michoro kama EPA, Escrew na mingine hawaoni huu uchungu kama siyo urongo na woga wa kawaida? Warejeshe rasimu ya Waryuba ndipo kieleweke vinginevyo kuna kila sababu ya kugomea hiki kiini macho kama alivyokiita Msomi. Tukatae katakata kushiriki jinai hii kwetu na vizazi vijavyo.”
Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si lakipita shangingi la Sam Sixx. Wacha tumtoe mkuku ili kumfanyia kitu mbaya. Bahati yake. Kama si ndata kurusha mibomu ya michozi angepatikana!
Chanzo: Tanzannia Daima Oktoba 22, 2014.
4 comments:
Ni sahihi kutopiga kura maana kura yenyewe imeishapigwa kwa katiba kupita hata kama kutakuwa na kura ya hapana inabadilika kuwa hapana katiba zaidi ya hii sisi watu wachache
Anon umenena. Dawa ya huu mzengwe ni kugomea kushiriki na si kushiriki kwa kutegemea kupiga kura ya hapana ambayo itachakachuliwa na kuwa ya ndiyo na kuupitisha.
Nasikia kutapika nikiona sura hizi
Huna haya ya kutapika bali kuhakikisha unahamasisha wengine kuzira huu uhuni unaoitwa kura ya kupitisha katiba.
Post a Comment