Baada ya kugundua kuwa walazimishi fulani waliopora madaraka ya wachovu na kuamua kutenda jinai kwa kuwabambikizia mkataba mpya wa namna ya kutawaliwa, wana kijiwe wanaonekana kukomaa pamoja na kulidurusu suala hili karibu kwa mwezi mzima na ushei.
Leo Msomi Mkatatamaa ndiye analianzisha pindi tu baada ya kukaa, kuamkua, kuagiza na kubwia kahawa yake. Anasema, “ Jamani mmeona jeuri ya Sam Sixx na Njaa Kaya kutubambika mkenge mwingine wanaouita Katiba Mpya?”
Mpemba anajibu, “Yakhe usinchefue. Kwani wallahi natamani niende nishike ntu na kuntia adabu kama si kumfanyia kitu mbaya.”
Kabla ya Mpemba kuendelea, Msomi anaendelea, “Hatuwezi kuwa mashahidi wa maangamizi yetu yaliyotengenezwa na mahabithi hawa kwa upogo na njaa zao bila kuangalia wakati ujao. Sisi tunaangalia miaka zaidi ya elfu moja toka sasa ambapo hatutakuwepo ingawa tuliyofaya yatakuwepo.”
Mgosi Machungi akiwa anampasia kipisi Mbwa Mwitu anakula mic, “Unadhani tifanye nini? Maana timepiga keee wee mahabithi hawa hawasiki na kama wanasikia wanajifanya hawatisikii hata kidogo.”
Mijjinga aliyekuwa amemaliza kuagiza kahawa yake anakatua mic, “Mie nadhani, kwa vile wamejifanya hamnazo, nasi tungoje wapitishe upuuzi wao kwenye vigwena vyao halafu nasi tuuchanilie mbali ima kwa kwenda kule na kutia mtu adabu au kugomea kura ya kuupitisha.”
“Mkigoma wenzenu wala. Kama mtafana kosa la kugoma, tutaendelea na upigaji kura na itapita kwa kishindo cha kisunami. Mkishiriki, pia lazima ipite tumtake mistake.” Anajibu Sofia Lion aka Kanungaembe huku akibeua midogo akiwa amemtazama Mijjinga.
Kapende hangoji. Anakwea mic, “Da Sofi hebu tujuze. Una uhakika gani kuwa itapita au ni kwa vile unajua kuwa mtachakachua kama kawaida yenu?”
Kabla ya Sofi kujibu, Mchunguliaji anasema, “Kama ni kupita itapita kwako mwenye mapenzi nayo.”
“Unasemaje? Eti itapitia kwake? Ni nini hiyo jamani mbona siwaelewi?” Anachomekea Mbwa Mwitu.
Kanji anaamua kula mic, “Sasa Mbwamwitu taka tukana vatu. Veve naambia katiba. Sasa unaleta tusi ya nini sema eti Sofi iko penzi nayo na tapita kwake. Kana naongelea kitu ingine nashauri veve koma na acha tani.”
Kijiwe hakina mbavu jinsi Kanji anavyojifanya kutojua Kiswazi wakati anakijua fika kuliko hata kigabacholi.
Mipawa, baada ya kugundua kuwa utani unaweza kuharibu mada, anakula mic, “Tuache utani. Uchoyo, ubinafsi, roho mbaya na uroho vitaangamiza kaya tusipochukua hatua mujarabu. Nakubaliana na wazo la kuchanachana hiyo kitu. Hakuna cha kungoja ichakachuliwe. Maana wakifanikiwa wataweka rehani vizazi vyetu au siyo?
“Hivi mmesikia kuwa uchakachuaji wa sirikali za mitaa utafanyika chini ya daftari la zamani?” Anauliza mzee Maneno huku akipokea kipisi toka kwa Mijjinga.
“Ukisikia uchakachuaji kuanza kabla ya mechi ndiyo huu. Iweje tutumia daftari la zamani wakati walaji fulani wameishajipatia mabilioni kwa kuandika jipya? Hili nalo halikubaliki.” Anazoza Kapende.
“Yakhe mie nshasema mara nyingi. Tusipowatoa hawa matwahuti tutajauzwa wazima wallahi.” Anadema Mpemba huku akimuashiria muuza amuongezee kahawa.
Mheshimiwa Bwege aliyekuwa kimya muda mrefu anatia daruga, “Sitaki kusikia lugha ya kuuzwa. Tulishauza zamani kwa kila aina ya majizi kuanzia Kagodamn, Richmonduli, EPA, IpTL, ESCROW na kadhalika. Sema tutakuja fanyiwa kitu mbaya tunajiona.”
“Subutu! Mgosi hii ya kufanyia kitu mbaya siafiki. Tifanyiwe kitu mbaya kwani sisi hatina hizo zana za kuwafanyia kitu mbaya? Nadhani titakuja kupiga mtu zongo haafu timfanyie kitu mbaya mchana kweupe ili iwe somo kwa wengine.”
Kijiwe hakina mbavu kwa jinsi Mgosi anavyotishia kupiga mtu zongo na kumfanyia kitu mbaya.
Msomi anarejea, “Japo unaweza kuchukuliwa kama utani, naona kuwafanyia kitu mbaya inaweza kufikisha ujumbe kama siyo kuondoa mzizi wa fitina. Maana dawa ya moto ni moto. Tumevumilia kuuzwa lakini siyo kufanyiwa mchezo mbaya kama huu unaoendeshwa na Sam Sixx na bwana wake Njaa Kaya ambaye ametimkia kwa Joji Kichaka kukwepa ripoti ya rushwa ya Escrew ya watu wake. Aende ajue atarudi na zigo atalikuta tu kama alivyopayuka Annae Makidamakida kuwa lazima ripoti iondowe watu.”
“Mnaona? Kama tungekuwa na katiba mpya ya wachovu bila shaka uchafu kama huu usingendekezwa na kukingiwa kifua kama ambavyo imekuwa siku zote kutokana na hii iliyopo kubariki ujambazi.”
Akiwa anatikisa kichwa kwa hasira, Mipawa anakula mic, “Sasa tuazimie na kutuma ujumbe kwa hao matwahuti wanaojidanganya kuwa wanaweza kutugeuza majuha kila mwaka kwa kutuchezea mahepe. Katiba yenu ya uchakachuaji na ufisadi haipiti come rain come shine.”
Kapende anakula mic, “Naona tuanze kukusanya saini za kupinga katiba kupigiwa kura. Pia tuombe wachovu waturuhusu tuwafungulie mashtaka wale wote waliobariki na kushiriki ujambazi huu.” Anaamka na kwenda kununua daftari ili tusaini.
Anarejea na daftari kubwa jeusi.
Tukiwa tunajiandaa kuweka saini si Sofi akalipoka na kukimbia nalo! Acha tumkimbize ili kumtia adabu!
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 1, 2014.
No comments:
Post a Comment