Sikuwa nimepanga kuandika makala nyingine juu ya Samuel Sitta. Ila kwa vile ametokea kuwa msemaji wa Katiba Mpya kuliko hata rais Jakaya Kikwete aliyeunda tume ya kuhariri maoni, nimelazimika kurejea uwanjani kumuelimisha mtu yule yule ili angalau jamii imjue, kumtahadhari, kumzuia asiende zaidi na kukataa hujuma anayolitendea taifa kwa sababu binafsi na zisizo na tija kwa taifa. Hivi karibuni mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba (BMK), Samuel Sitta linaloendelea kinyume cha matakwa ya watanzania Samuel Sitta alikaririwa akilalamika kuwa amekuwa akitumiwa meseji za matusi kupitia simu yake ya kiganjani. Kwa wanaojua maana sahihi ya matusi, watakubaliana nasi kuwa na Sitta pamoja na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) rais Jakaya Kikwete wamewatukana watanzania tena matusi ya nguoni. Haiwezekani watanzania wapoteze muda na fedha kutoa maoni halafu watu wawili, kwa woga na sababu binafsi, wakayapuuzia na kuwabambikia utashi na mipango yao wasiwatukane matusi ya nguoni. Licha ya matusi ya nguoni, wamewapuuzia na kuwageuza watanzania hamnazo bila stahiki wala sababu za msingi. Hata hivyo, nao watakuja kugundua kuwa wamejitukana ingawa ni mapema. Kwani nao ni watanzania hata kama wana madaraka na ushawishi. Hata kitendo cha hivi karibuni kwa Sitta kutumiwa meseji za matusi ni ushahidi kuwa “amelianzisha” na anapewa vipande vyake japo hakuna anayeuunga mkono ustaarabu wa matusi yawe ya kisiasa kama kuchakachua katiba mpya au ya nguoni kama kuwapuuzia watanzania. Mkuki kwa nguruwe!
Sitta amekuwa wa kwanza kulalamikia matusi asijue aliyaanzisha yeye. Hatujui mwenzake naye ametumiwa kiasi gani. Sitta alikaririwa kisema, “Mimi napokea matusi kila siku. Meseji zisizopungua 50 viongozi wa Chadema wameweka namba zangu katika tovuti nitukanwe kila siku hilo mimi niko tayari na mnaniona niko safi tu wala sihangaiki nalo.” Kama uhangaiki, unalalamika nini; au kulalamika si kuhangaika? Uko safi vipi wakati unafanya kazi chafu ya kuchakachua katiba ya wananchi? Hivi ukipanda mbigiri unategemea nini? Eti huyu ndiye anayetaka kuwa rais wa Tanzania! Anadai ni viongozi wa chadema? Rais wa namna gani anayeweza kujizushia mambo na kudanganya wazi wazi? Je hii ndiyo maana wameondoa ibara inayozuia wabunge kudanganya bungeni? Uko wapi ushahidi wa kuthibitisha madai yake? Kila kinachofanyika, CHADEMA! Itafikia mahali hata mvua ikiacha kunyesha au kuleta mafuriko mtasema ni CHADEMA, Mnamgeuza nani juha?
Sitta na wenzake wamesahau kuwa matusi yao kwa watanzania yananaza kujibiwa kwa matusi hayo hayo. Aliongeza, “Kwa hiyo wale wanaoendeleza hayo mapambano tuendelee na tutaendelea kupambana, lakini kazi ya Bunge Maalumu itaendelea na ndugu zangu Watanzania mjue tunaandaa Katiba safi na rafiki kwa wananchi na itapatikana.” Hivi katiba safi ya watanzania inaweza kuandikwa kwa kudharau maoni yao? Katiba ya wananchi safi na rafiki inaweza kuandikwa na chama kimoja pamoja na vibaraka wake? Katiba ya wananchi inaweza kuandikwa kwa kuchakachua mawazo yao? Kweli katiba ya wananchi inaweza kuandikwa na mafisadi wanaolinda maslahi binafsi kwa kuyasulubu ya taifa? Licha ya kuwa utani mbaya, haya ni matusi ya nguoni yanayopaswa kuwakera na kuwakereketa watanzania kiasi cha kuyakemea kwa nguvu na nyenzo zote, tena si kwa maneno bali matendo mitaani.
Je Sitta hajagundua kuwa anachosimamia ni dhuluma ya aina yake?
Anasema kuna vyombo vya habari vinamchukia! Nani ampende wakati amehujumu kila mtu? Kwanini sasa baada ya kuingiza nchi kwenye mtafaruko wa tararatibu au amesahau alivyoenguliwa kugombea uspika vyombo hivyo hivyo anavyolaumu vilivyokemea jinai aliyotendewa? Kumbe Sitta ni mwepesi wa kusahau hivi! Alikaririwa akisema, “Kuna baadhi ya vyombo vya habari wananichukia mimi binafsi. Wasichanganye chuki hizo na mchakato wa Bunge Maalumu.” Ingeleta maana kama angetaja hivi vyombo vya habari na hayo mambo binafsi. Je kuna jambo ambalo vyombo vya habari vinajua na umma haulijui kuhusu ugomvi wake na Sitta au anaweweseka baada ya kuonyesha wazi ambavyo hafai kiasi cha kupingwa na baadhi yetu kuwa hafai hata hata kugombea wenyekiti wa kijiji achia mbali urais? Rais gani asiye na huruma na wale anaotaka kuwaongoza? Rais gani anayeshiriki kuhujumu umma maskini kwa kujilipa na kuwalipa wenzake kutenda jinai ya kuchakachua katiba? Rais gani asiyesikia hata baada ya wakuu wake kujaribu kusikia? Rais gani asiyeheshimu mawazo ya wale anaotaka kuwatawala? Rais gani asiyejua hali ya nchi yake kiasi cha kuruhusu fedha ya maskini itumike kwenye mazingaombwe yanayoitwa Bunge Maalum la Katiba?
Hakuna kinachokera kama Sitta kuyaita haya mazingaombwe eti katiba safi na rafiki kwa wananchi. Wananchi wapi iwapo maoni yao mliyazika na kuweka yenu? Je kuna matusi zaidi ya hayo? Nadhani Sitta na wenzake hawajatukanwa vilivyo. Tusi lililowafaa si jingine bali kuwafuata huko waliko na kusitisha jinai wanayotenda huku wakitupwa nje ya ofisi za umma wanazotumia kuuhujumu. Wakati wa kuzuia jinai ya akina Sitta ni sasa. Watanzania amkeni. Wakati ni sasa.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 1, 2014.
No comments:
Post a Comment