Ingawa kila mtu ana vigezo vyake vya
rais anayemtaka, kuna haja ya sisi –kama taifa – kuwa na vigezo vya pamoja –hasa
tukiangalia matatizo yanayolikabili taifa –vya kumpata rais ajaye ili asafishe
uchafu unaonuka na kutamalaki nchini ambako jinai na ubabaishaji vimegeuka sera
hivi hivi. Kwa upande wangu ningependa rais ajaye awe na uchungu na nchi kwanza
kabla ya mambo mengine. Maana, ukiwa na rais asiye na uchungu na nchi matokeo
yake ni kuendeleza na kuzidi kushamiri
kwa ufisadi na matumizi mabaya ya fedha na raslimali za umma ambayo sasa ni
tatizo na janga la kitaifa. Tumeendekeza
kuombaomba na kukopa kopa huku hata kidogo kinachopatikana tunaruhusu wezi
wakubwa wakiibe na kutuacha maskini zaidi.
Kitu kingine ningependa rais ajaye
athamini elimu sawa na anavyothamini uhai wake. Maana, taifa lisiloelimika
litaangamia, hali ilivyo sasa inatisha na kukatisha tamaa. Lazima apatikane mtu
wa kutukwamua na jinai hii itokanayo na matumizi mabaya ya ubongo ambapo mambo
ya kijinga yamefanywa mambo ya maana na ya maana kufanywa ya kijinga kiasi cha
kugeuka taifa la kigodoro. Nikiangalia hali ilivyo sasa –ambapo ubabaishaji
umeingia karibu kila nyanja ikiwamo elimu – najikuta nikichanganyikiwa na
kupatwa na hofu sana juu ya mstakabali wa taifa hasa vizazi vijavyo. Maana, kwa
namna mambo yanavyofanyika, ni kama vile hakuna kesho wala maisha baada ya hawa
walaji waliopo kuondoka wakiacha nyuma nchi iliyopaganyika karibu na kuwa taifa
lililofeli yaani failed state. Kwa ufupi ni kwamba bila kuwa na rais anayeona mbele
na mbali na badala yake tukawa na mtu anayeangalia tumbo lake na jamaa zake
waliomzunguka, taifa letu litaingia kwenye machafuko kwa sababu kuu nne yaani ulafi,
upofu, ujinga na ufisadi.
Mwalimu Julius Nyerere – rais wa
kwanza – alituachia urathi mkubwa hasa kwenye elimu. Licha ya kutoa elimu ya
bure kwa watanzania wote toka mwaka 1967 hadi 1990, alisoma na kutunga vitabu.
Alikuwa gwiji wa kutoa na kushiriki mihadhara chuoni (wakati ule tulikuwa na
chuo kikuu kimoja tu cha Dar Es Salaam kikisifika kwa fikra za kimapinduzi). Alipenda
wakati mwingine kuitisha mikutano na waandishi wa habari mara nyingi akijibu
hoja mbali mbali za wananchi. Alikuwa akiongoza nchi kwa mfano na si kwa mdomo.
Alisema alichotekeleza na kutekeleza alichosema. Alikuwa mtu wa vitendo zaidi
ya maneno. Baada ya kung’atuka, taratibu nchi yetu ilikwenda kwa mbwa kam
alivyowahi kusema, “I can let my country go to the dogs” asijue itakwenda baada
ya yeye kutoweka hasa wale aliowakataa kupewa ukanda.
Baada ya kuondoka Nyerere –ambaye kitaaluma
alikuwa mwalimu – tulipata mwalimu mwingine, Ali HassanMwinyi ambaye –hata
hivyo –hakuonyesha mapenzi kwa elimu wala umahiri wa kushiriki na kutoa
mihadhara kama mtangulizi wake. Kwa upande fulani alionekana kupenda kuhudhuria
shughuli za kidini kuliko mihadhara ya kitaaluma. Hii, huenda inatokana na
ukweli kuwa alikuwa shehe na msomi mkubwa wa dini ya kiislamu.
Baada ya Mwinyi aliingia Benjamin
Mkapa, mwandishi wa habari ambaye alionyesha kupenda kuandika na kusoma hotuba
ndefu. Alipenda sana kusafiri na kushiriki makongamano ya kimataifa hadi
kufikia kusema kuwa huwa anajisikia raha akihojiwa na waandishi wa habari wa
nje kuliko wa nyumbani. Alikuwa akiwakandia waandishi wa habari wa ndani si kwa
sababu walikuwa mbumbumbu kama alivyotaka waonekane bali kutokana na kujua
ufisadi kibao na kumusulubu kwa masuala ambayo wageni hawakujua.
Baada ya Mkapa aliingia Jakaya Kikwete
mwanajeshi ambaye alipenda sana michezo na kusafiri kuliko mihadhara na
makongamano ya kitaaluma. Tofauti na wenzake, rais Kikwete ataingia kwenye
vitabu vya historia kama rais aliyehudhuria misiba mingi kuliko matamasha
vyuoni na mashuleni ukiachia mbali kuizunguka dunia hadi watani wake
wakambatiza jina la Vasco da Gama yule habithi wa kireno aliyeizunguka dunia
akitafuta makoloni na nchi za kupora. Ataingia vitabuni kama rais aliyepiga
picha na wasanii wengi kuliko wasomi. Pia ataingia kwenye vitabu vya historia kama
rais ambaye chini yake elimu ilivurugika sana. Lawama nyingi bila shaka
zitakwenda kwa rafiki na mshirika wake toka jimbo la rais, Dk Shukuru Kawamba
ambaye utawala wake uliua kabisa elimu ya Tanzania.
Kwa kuangalia mdudu yaliyopo kwa sasa,
rais ajaye asipokuwa na uchungu na taifa na elimu basi tumekwisha. Maana kwa
sasa elimu haina maana tena kiasi cha kusahaulika na kuhujumiwa na kila ajaye.
Imefikia mahali watu wanaghushi vyeti na wanaendelea na nyadhifa tena za juu
serikali kama vile uwaziri. Je kama tumeweza kuvumilia mawaziri walioghushi,
tutapata wapi motisha na uhalali wa kuwashughulikia makatibu muhtasi, walimu,
wakunga, polisi na wengine tutaweza kuwashughulikia? Hakuna kitu kinachoendelea kuwachanganya wengi
kama mzaha uliotolewa hivi karibuni kama kupendekeza kuwa kuwa Kiswahili
kitumike kama lugha ya kufundishia kuanzia shule za vidudu hadi vyuo vikuu. Bila
kubatilisha uamuzi huu nchi itaingia matatani kitaaluma hata kimkakati.
Tumalizie kwa kusema wazi kuwa rais
ajaye lazima awe ni mpenda elimu kweli kweli.
Awe na uchungu wa hali ya juu na taifa vinginevyo miaka si mingi,
tutaambulia kilio hata vurugu tokana na madudu yanayofanywa kwa sasa. Angalia
ufisadi, wizi wa fedha za umma, ujambazi, biashara haramu ya mihadarati na
uzembe na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Chanzo: Dira.
No comments:
Post a Comment