The Chant of Savant

Friday 27 March 2015

Kinana: Hapana, kufichua mafisadi kiama cha CCM


          Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahaman Kinana ni mtu asiyeishiwa vituko. Ni bingwa wa kutoa matamko yanayosuta chama chake huku akijionyesha kama mkosoaji na mwana mageuzi mzuri lakini hatoki CCM.  Kama anamaanisha anachosema basi hapaswi kuendelea kuwa CCM tena kwenye madaraka makubwa kama hayo. Heri atoke nje akosoe kwa dhati kama akina Joseph Warioba na Joseph Butiku wanavyofanya. Vinginevyo hataeleweka zaidi ya kupiga kelele na kufanya maigizo na ngonjera tupu. Mara nyingi Kinana huongea kama mtu asiyeishi Tanzania wala asiyejua ima anachosema au chanzo cha anacholalamikia.
 Hivi karibuni Kinana alikaririwa akisema, “Tatizo lenu (wanachama wa CCM) mnakuwa wapole na mnajenga tabia ya kulindana. Kwa njia hiyo hamtaweza kukisaidia chama chenu. Mtu akikosea hakuna bahati mbaya, ondoa huyo na apelekwe jela mara moja ili kazi nyingine zisonge.” Kwanza, Kinana anaongea kama si mwanachama wa CCM tena mwenye nafasi ya kufanya hayo anayowahadaa watu wa chini yake. Pili, ukimuuliza ametaja wangapi au ameonyesha ukali wake lini wapi na katika lipi, nadhani hatapata jibu la maana. Tatu, Kinana anaongea kana kwamba hajui ni wapi pa kutoa malalamiko au ushauri wake huo “mzuri”. Kila siku anaongea na mwenyekiti wa chama rais Jakaya Kikwete. Anashindwa nini kumwambia hayo mawazo yake mazuri ya kukijenga chama kama siyo hadaa za kisiasa na maneno mazuri ya majukwaani? Nne, Kinana anapaswa awe mkweli akifahamu kuwa watanzania wa sasa siyo wa mwaka 47. Wanajua fika anavyowadanganya na kuwageuza majuha. Siku hizi anaonekana kwenye picha akifanya kazi hii na ile huku na kule kama kiongozi mchapa kazi na wa mfano. Ukimuuliza siku za nyuma alikuwa wapi kama siyo gea ya kusakia kura hakupi jibu la maana. Hata hivyo, kujenga kibanda sehemu fulani au kumwagilia bustani kwa siku moja kunaweza kuondoa matatizo ya wananchi kama siyo kuwahadaa ili watoe kura wakipate kingine cha moto?
Kinana anapiga mdomo hasa wakati huu tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu kana kwamba anaongea na mataahira. Muulize Kinana; Ilikuwaje yeye akatuhumiwa kusafirisha nyara za taifa na bado akateuliwa kuwa katibu mkuu wa chama anachowalaumu wanachama wake? Au ni yale ya nahodha kuongoza kwa kukaa nyuma badala ya kukaa mbele? Je Kinana hajui matatizo ya taifa letu hasa ufisadi, wizi, ujambazi, kujuana, kulindana na jinai nyingine nyingi zilizolifikisha taifa hapa msambweni? Kama hajui au anajua lakini anajifanya hajui si bora anyamaze tu kuliko kuwakebehi maskini wa taifa hili waliosikinishwa na sera mbovu za chama chake. Anachofanya Kinana ni utani na matusi kwa watanzania tena maskini wanaonyonywa na mali na fedha zao kuibiwa kila uchao chini ya uongozi wa CCM na akina Kinana.
Kuonyesha anavyoishi ndotoni kwenye nchi ya Kusadikika, Kinana aliongeza, “Nasema kwa wanachama wa CCM nchi nzima, mpango wa kuhamisha mtu kutoka eneo moja na kupelekwa sehemu nyingine huo usiwepo, mtu akituhumiwa lazima aachie ngazi akisubiri uchunguzi.” Muulize, nani anahamisha hawa wavurugaji kama siyo chama chake? Hata hivyo, Kinana anaonyesha kitu kimoja dhahiri kuwa viongozi wa CCM wako mbali na wananchi kiasi cha kujisemea bila kufikiri madhara ya wayasemayo. Kama Kinana angekuwa anasoma alama za nyakati, basi angemshauri bosi wake abatilishe baadhi ya uteuzi wa hivi karibuni wa wakuu wa mikoa na wilaya hata mawaziri. Hivi Kinana hajui kwa mfano, mawaziri waliovurunda wakaendelea kubakizwa serikalini mfano waziri wa Elimu, Jinsia Wanawake na Watoto, Fedha, Kilimo, Serikali za mitaa na wengine wanaojulikana kuvurunda lakini tokana na ukada na ukaribu wao kwa wakubwa wakaendelea kubakizwa ili wavurunde zaidi? Kama hawajui tumempa wizara zao. Aende akamwambie bosi wake awafute kazi badala ya kuwakingia kifua.
 Hakuna kauli iliyowachefua na kuwaacha wengi hoi kama Kinana kusema, “Wakati wa kuiba wezi hawafuati utawala bora, lakini wanapotakiwa kuondoka ndipo masuala ya utawala bora yanapoanza kusimama, naona suala la utawala bora litazamwe upya maana wengine hawafanyi kama tulivyowatuma.”  Kinana aambiwe wazi kuwa Tanzania hakuna utawala bora bali bora utawala. Kungekuwa na utawala bora kusingekuwa  na mauaji ya kila mara ya walemavu wa ngozi, wizi wa fedha za umma, uzururaji wa wakubwa, uuzaji mihadarati, utoroshaji nyara aliohusishwa nao na madhambi mengine mengi ambayo yanafanywa na kulindwa na chama chake anachojitahidi kuonyesha kuwa hakihusiki wakati kinahusika fika. Kinana huyu huyu alikuwa mshauri na mkuu wa kampeni wa rais Kikwete wakati wa kampeni za uchaguzi. Anataka kusema kuwa hajui hata walioiba fedha ya EPA wakaitumia kuwahongea wapiga kura na kuupata ukubwa wakaendeleza mchezo huo hadi kuja na Richmond na Escrow? Kama hajui haya au anayajua lakini anajifanya hajui basi hafai na ajinyamazie angaojee hukumu ya wananchi hapo mwezi wa kumi. Hata hivyo, Kinana ana wasi wasi gani wakati mchezo wa kuchakachua kura unajulikana?
Yatosha kumwambia bwana Kinana: Tafadhali acha kebehi na matusi ya nguoni wakati umma unaumizwa na chama chako hicho hicho unachopigia debe. Kama una uchungu na taifa hili wajibika wewe kwanza lau utoe maelezo kuhusiana na shutuma zinazokukabili badala ya kushupalia ya wengine wakati yako bado hujayamaliza. Ni vizuri Kinana akafahamu kuwa watanzania si majuha na mataahira wa kudanganya kila baada ya miaka mitano. Wahenga walisema, ada ya mja kunena muungwana vitendo. Watanzania wanataka vitendo na si ngonjera tenzi na maigizo ya majukwaani mbele ya kamera.
Chanzo: Dira ya Mtanzania

No comments: