How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 17 March 2015

Kijiwe Chamstukia na Kumbeep Kinamna


  • katibu mkuu wa ccm abdulrahman kinana akifunga skrubu wakati akiweka
Baada ya katibu mkubwa wa Chama cha Maulaji (CcM) Amduli Kinamna kuwa akionyesha kama mchapa mzigo wakati ni mchapa picha, Kijiwe kimeamua kumtolea uvivu na kumtumia salamu aache usanii.
Leo linaanzishwa na Mpemba, “Yakhe mmemuona mjivuni aitwaye Anduli Kinamna anavyojionyesha kama nchapa kazi wakati ni nchapapicha? Hivi huyu ataka kundanganya nani wakati wote wanjua?”
Kapende anadandia, “Huyu hana jipya. Angekuwa nalo si angejitetea lau kuhusiana na kashfa ya kusafirisha vipusa vyetu Asia? Hawa jamaa kwa usanii sina hamu.”
Mgosi Machungi anadandia mic, “Tishimishangae Kinamna hasa ikizingatiwa kuwa chama chao ni cha maigizo. Baada ya kutoka mgosi mwenzangu akaja huyu ai shabbaab na ngonjera na sanaa zie zie. Sijui kwanini hawachoki waa kubadii mbinu yao ya kufanya utapei wa kisiasa!”
Sofia Lion aka Kanungaembe leo hangoji. Anakamua mic, “Tafadhali achene kutukana watu bila ushahidi. Mnaodai alisafirisha vipusa vyenu mnao ushahidi au vijiba vya roho na wivu?”
“Malizia wivu wa kike Sofi tafadhali,” Mbwamwitu anamchomekea Sofi.
Mijjinga hangoji. Anakwea mic, “Ama kweli siku hizi da Sofi umegeuka mwanasheria. Kila kitu unataka ushahidi. Je wewe una ushahidi gani kuwa Sofi ni jina lako? Kuna vitu vingine havitaki ushahidi. Kwa mfano, jamaa anavyofanya usanii wa wazi akijionyesha kama mchapakazi na mkereketwa wa wachovu nalo linataka ushahidi dadangu?”
Mheshimiwa Bwege anakwanyua mic, “Kutaka ushahidi si vibaya. Kama Kinamna angepinga au kutoa maelezo ya tuhuma zake hapo ndipo ushahidi ungehitajika. Mtu hajajitetea tutoe ushahidi wa nini? Unataka tuue kesi kabla haijaanza siyo?”
Msomi Mkatatamaa anaamua kutia guu, “Mheshimiwa hujakosea. Mimi nimesoma sheria kweli kweli siyo kama akina mzee wa Vijisenti wanaotumia taaluma kuibia wachovu. Kisheria, yanapotolewa madai au tuhuma, mtuhumiwa hupaswa kujibu ndiyo aukukanusha ndipo ushahidi huitishwa. Hili halihitaji kuwa na shahada nyingi za sheria kama mimi.” Anajisifu kidogo kama mtume Paulo kwa Wakorinto na kuendelea, “Nami nakubaliana na wanaomuona Kinamna kama msanii. Hata matamshi yake yanaonyesha hili. Mfano juzi aliwataka wanachama chake wawafukuze wavurugaji utadhani wanachama ndiyo wanaowateua. Kimsingi, alimchokonoa na kumsuta bosi wake Njaa Kaya ima bila kujua au kudhani waliokuwa wakimsikiliza ni mabunga na wasanii kama yeye.”
Kanji anakatua mic, “Somi sema kweli bana. Hii na Nana iko sema neno kama hii? Hapana amini kama ongozi ya CcM naweza nyonga menyeve kwa neno yake kama haina akili zuri.”
Mipawa anaamua kutia daruga, “Kanji unauliza swali au jibu. Kwa taarifa yako mimi nilirejea jana toka Idodomya alikopayukia mjivuni na jangili huyu. Ni kweli aliyasema na wenye akili walishangaa na kudhani bosi wake angemnyofoa kwenye ulaji ili akawinde vipusa vizuri. Hata hivyo, nani amfukuze nani wakati wote lao moja? Majogoo yote hunya ndani ati.” Kijiwe kinaangusha kicheko isipokuwa da Sofi aliyenuna utadhani atapasuka.
Mzee Maneno anaamua kula mic, “Mimi sishangai huyu Kinamna kukufuru mbele ya umma. Mara hii mmesahau alivyowaita walaji wenzake mawaziri mizigo akaishia kuwa mzigo mwenyewe! Kawaida ya mbwa abwekaye hang’ati. Hata aliyemfuga anajua hili ndiyo maana ahangaiki kumfuta kibarua.”
Kapende anarejea, “Hebu tuwe wakweli. Pamoja na kutokubaliana na yote abwabwajayo Kinamna, hili la mizigo nakubaliana naye. Nampinga kwa kuogopa kusema kuwa hata bosi wake ni zigo kubwa lilileta mizigo midogo aliyokuwa akiiandama.
Mpemba anakatua mic, “Mie naona kilomsukuma wivu wa kike. Kama wote nzigo yeye nani kuwasema mizigo wenzake kama siyo nnafiki? Kama angekuwa amaanisha asemacho si angejiondoa kwenye hilo genge au kujivua ulaji akosoe vizuri kama wakosoaji wengine?”
Msomi anakatua mic tena, “Nadhani nyie hamuwajui hawa wasanii. Hamjui kuwa huu ni wakati wa kuelekea kwenye uchakachuaji ambapo kila msanii huja na sanaa zake ilmradi genge lao lipite waendelee kula kwa mikono na miguu bila kunawa hata kuomba? Naona wapingaji wamewabana kiasi cha kupumulia mpira. Hivyo, watafanya kila liwalo liwezekanalo na lilisolowezekana lau wapate kula. Hivyo, haya yote afanyayo jamaa ni harakati za mfa maji. Nashangaa anapigwa picha yeye kana kwamba chama hakina watendaji wengine! Au ni kwa vile jamaa hakujaliwa kujisuta wala kuona aibu?”
Mijjinga anakatua mic, “Kweli wengi hawamuelewi Kinamna na Njaa Kaya. Baada ya Njaa Kaya kugunduliwa na lile gonjwa, nadhani alimpa kazi ya kuzurura ndani ya kaya wakati yeye akizurura nje kusaka matibabu na matanuzi ili lau chama kionekane kiko karibu na wachovu wakati ukaribu wenyewe ni wa mrija na chupa. Nadhani kuna haja ya kuwahamasisha wachovu tuwapige chini msimu huu ili lau tujikomboe au vipi?
Mpemba anakula mic, “Yakhe mie niko nyuma yako.”
Kabla ya kuendelea Mijjinga anang’ak, “Yakhe sitaki upopobawa ati. Nyuma yangu ukae unafanya nini? Kama kukaa nyuma kama Kinamna anavyofanya basi nenda kakae nyuma yake ati. Maana ukiona anavyowalaumu wanachama kuwa wanawavumilia wanaovurunda au kuwahamisha unashangaa kwanini yeye asiwe mstari wa mbele kuonyesha mfano lau kwa kumwambia bosi wake. Wote wanakaa nyuma na kutaka wanachama wafanye vitu. Haifai ati.”
Mpemba anajibu, “Waona nadhani waongoza kama nahodha wa mashua ati.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si tukasikia mlio. Tulidhani al shabaab wameshambulia. Tulitimka hao!
Chanzo: Tanzania Daima Machi 18, 2015.

No comments: