How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 3 March 2015

Kijiwe Chagundua Waliomtumia Wahuni Warioba

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiSEmCq3EQgqIVAUtDBJwGJM0s74U2BvOulklGwh8ZeI5teZVdNWSZerrQyeGX9M76fJOFi55oRg9rJoGHoptnnj_FsOT6poq7ph61ZSHV9yaZefdO8OCGjL91fVsAN1B8956Ny2MrCEk8/s1600/0L7C0742.JPG
          Baada ya wengi kuwa wanamtafuta mchawi wa gwiji la Katiba ya wananchi mzee Jose Shinda Waryuba bila mafanikio, Kijiwe kimemuibua hivi karibni baada ya kupewa malipo ya uhuni na usaliti wake. Anayeleta hoja leo ni Mgosi Machungi.
          Anaanza, “Wagosi mmesikia na kushuhudia uhuni tuliofanyiwa hasa wilaya ya Kinondo? Waahi sikuamini macho na masikio yangu kuona mhuni Makondakonda akipewa ukubwa wa wilaya hii.”
          Mijjinga anakula mic, “Kenge huzaa kenge usitegemee azae mamba. Sisi tulijua waliomtumia wahuni mzee Jose Shinda Waryuba baada ya kukomalia Katiba ya wananchi dhidi ya wala nchi. Naamani nimkamate huyu mhuni Makondakonda na kumfanyia kitu mbaya ili liwe somo kwa wengine. We ngoja nitakuja kufanya kweli mie.”
          Mpemba anamwangalia Kapende na kunong’ona tokana mkwara uliochimbwa na Mijjinga ambaye huwa anaziweza ngumi si haba. Anakwanyua mic na kusema, “Yakhe hata mimi nina maya na huyu mkuda. Kama ingekuwa Pemba wallahi asingekalia hicho kiti ili akichafue.”
          Kapende anarukia mic na kuzoza, “Ipo siku yake wala asiwahangaishe. Hakuna lisilo na mwisho. Hata hao wahuni wakubwa waliomtuma na hatimaye kumpa ulaji kwa kazi ya unepi na utaulo wataondoka naye ataondoka tu. Tuliwaona wangapi tena wenye vifua na maarifa?”
          Msomi aliyekuwa akiweka vizuri tablet yake mezani anakamua mic, “Mie sishangai. Kama ulivyosema mheshimiwa Mijjinga,” anageuka na kumwangalia Mijjinga na kuendelea, “Kenge hawezi kuzaa mamba wala mbwa kuzaa samba. Huyu bwege ni kielelezo cha uhuni wa wakubwa wanaojifanya wastaarabu wakati ni washenzi na wezi wakubwa. Huoni walivyomshindwa Rugemalayer na ponjoro Seti Singsong? Hata hivyo, tunapaswa kujilaumu kwa kubariki huu  uhuni wa mchana na wa kitoto. Wanadhani wakiwalipa fadhili wahuni wao watamtisha mzee Waryuba au kutunyazisha tusidai Katiba yetu? They won’t succeed in this nonsense so to speak.”
          Kabla ya kuendelea mzee Maneno anamuonya, “Msomi angalia hiyo lugha ya Kikameruni. Au unataka tumfanyie mpango huyu Makondakonda tumkameruni na kumpiga picha ili wote wajue alivyo bwabwa?”
          Kijiwe hakina mbavu kwa jinsi mzee Maneno anavyomwaga usongo na ngoa.
          Mipawa anakwanyua mic na kudanda, “Tukubaliane kuwa kaya yetu imebakwa vilivyo. Wanaiba njuluku zetu wanavyotaka. Wanataka kuwatisha na kuwanyamazisha watetezi wa wachovu kwa kuwatumia wahuni kwa malipo ya ulaji tena ulaji wenyewe wetu. Kwanini tusiamue tukaandamana toka hapa hadi kwenye afisi ya mkubwa wa wilaya kupinga kuingiliwa na wahuni waliohongwa ulaji baada ya kufanya uhuni wa kitoto?”
          “Mie nawalaumu ndata kwa kuhangaisha wanuka njaa huku wakiwaogopa wahuni kama Makondakonda . yaani walishindwa hata kumwita wakamhoji lau wasionekane wanamgwaya. Hili jeshi au geresha? Kitendo chao cha kumgwaya mhuni tena msaka tonge kimewaondolea udhu wa kuwa walinzi wa usalama wa kaya na wa wachovu,” anazoza mheshimiwa Bwege huku akiweka vizuri msuli wake.
          Sofia Lion aka Kanungaembe ameguswa pabaya. Anakwanyua mic na kuronga, “Kuna haja ya watu hapa kuchunga ndimi zenu. Mnawatuhumu watu bila kuleta ushahidi mnadhani mtampata nani?”
          Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anajibu kihuni, “Tutakupata wewe na tukupate mara ngapi?” Anamgeukia Kanji na kusema, “Mshirika sikunyang’anyi mshirika wako natania.”
          Kanji anapoka mci, “Veve dugu yangu acha hiyo bwana. Mimi iko na memsahib vangu Kasturibhai atosa mimi yeye. Acha leta chonganishi na bibi yangu dugu yangu.”
          Kijiwe kinaangua kicheko kwa jinsi Kanji anavyojitetea utadhani bi Mkubwa wake yupo akisikia asiende akamvisha gagulo.
          Msomi anakamua mic, “Dada yangu Sofi unataka ushahidi gani wakai kila kitu kiko wazi? Ninachokumbuka ni maneno ya gwiji Mchonga.” Kabla ya kuendelea anasema, “Mzee Maneno nisameheni nitarudia maneno ya gwiji Mchonga kwa Kikameruni kama alivyoyatamka. Alisema, “I can let my country go the dogs. Sasa angekuwa hai huenda angebadili maneno yake hasa baada ya wahuni tena wakubwa kuliko Makondakonda kupewa ulaji. Mara hii msahau wahuni kama Abdi Kinamna jangili wa kutupwa, Mwehujuu Michemba ambaye sasa anatanua kwenye wizara ya njuluku huku akiwasingizia wapingaji ugaidi wakati yeye ndiye gaidi nambari wani?”
          Mijjinga anaamua kumpoka Msomi mic na kudema, “Umewasahau wahuni wengine kama huyu Nipe Ninaye wa chata la mafisadi? Umeasahau akina Bill Lukuviii na Lazio Nyalanduuu ambao wako wananema wakati si chochote si lolote?”
          Mgosi anarejea, “Sasa tikubaiane kuwa sasa tinatawaiwa na genge la wezi majambazi na wahuni. Maana nkiangaia safu nzima napata kichefuchefu waahi. Hapa bado hujawagusa wahuni kama wajina wake Sofi Lion, Hawa wana Ghasia na akina Makorongo Muhanga na Mery Nyagu walioghushi. Ama kwei kaya hii imekwenda kwa mbwa kama alivyosema gwiji Nchonga!
          Mheshimiwa Bwege anaamua kula mic, “Dawa ya moto ni moto. Kwanini tusiende wilayani na kumfanyia uhuni huyu mhuni ajue kuwa hata kama tu wastaarabu bado tunaujua uhuni? Hatuwezi kuendelea kutawaliwa na wahuni na makandokando na makondakonda yake.”
          Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si likapita shangingi la Makondakonda akikagua himaya yake. Acha tulifukuze huku tukilimwagia kahawa na kulitupia viatu kabla ya kutokomea. Ana bahati. Kama tungemnyaka tungemfanyia kitu mbaya hadi nkewe amwache.
Chanzo: Tanzania Daima Feb.,4, 2015.

No comments: