The Chant of Savant

Tuesday 10 March 2015

Prof Tibaijuka na mboga ya milioni kumi!


 
  • SHEREHE YA KUMBUKUMBU YA MIAKA 14 YA HAYATI BALOZI WILSON TIBAIJUKA
          Wakati mwingine inakuwa vigumu kuelewa busara ya baadhi ya ndugu zetu. Inakuwa vigumu sana hasa unapokuta mtu anayechukuliwa kama msomi wa kupigiwa mfano akifanya vitu ambavyo hata mjinga wa kawaida hawezi kufanya. Hivi karibuni waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendele ya Makazi profesa Anna Tibaijuka alitoa mpya kiasi cha kuacha wengi wakishangaa hata huo usomi na busara yake.
          Tibaijuka alikaririwa na vyombo vya habari akisema, “Nilitoa kiasi hicho kwenda kununua mboga, kwani kuna kosa gani.” Hapa anachomaanisha Tibaijuka ni shilingi za kitanzania milioni kumi. Hata kama alimaanisha kitu kingine, kwa mtu msomi ngazi ya Tibaijuka alipaswa kujua madhara ya kauli kama hii ambayo waingereza huita irresponsible. Huwezi kuita milioni kumi pesa ya mboga wakati watanzania wengine maskini wanakufa bila kuipata fedha kama hii. Huwezi kusema milioni kumi ni fedha ya mboga wakati watu wanalala njaa kwa kukosa hata hiyo elfu moja. Kwa lugha rahisi ni kwamba Tibaijuka alijitahidi kuonyesha alivyo tajiri anayeweza kutumia mamilioni ya fedha kwa ajili ya kununulia mboga. Sijui hiyo mboga ni ya aina gani? Bila shaka ina viungo vya almas, dhahabu na rubi.
          Hata hivyo, Tibaijuka si msomi wa kwanza kutoa nyodo kama hizi ili kuwakera makapuku. Nani mara hii kasahau jinsi mwenzie Andrew Chenge alivyowahi kuita dola za kimarekani alizosemekana kupokea kama rushwa na kuzificha kwenye visiwa vya Jersey kuwa ni vijisenti? Kama haitoshi, bingwa wa kuhonga na mtuhumiwa mkuu wa wizi wa escrow James Rugemalira aliita dola milioni 75 vijisenti vya ugolo. Sijui ni aina gani hii ya ugolo anayobwia Rugemalira. Kimsingi, wahusika waliamua bila huruma wala aibu kuwakoga watanzania maskini waliowaamini ofisi zao wakazitumia kama kijiko cha kuchotea utajiri. Ajabu ya maajabu, Chenge na Tibaijuka bado ni wabunge. Hawa hawafanani na watanzania. Hivyo, hawafai kuwawakilisha bungeni ambako wanakwenda kupiga dili na kuzika maadili utu na huruma ukiachia mbali kushiba hadi wakalewa na kuondokewa busara.
          Ukiangalia tambo za kijinga za namna hii unagundua kitu kimoja. Wanatoa motisha kwa maskini kutafuta fedha kwa njia yoyote ile ili mradi nao waukate kama wakubwa hawa mabingwa wa kusema bila kufikiri wala kuchelea nini inaweza kuwa tafsiri ya kufuru zao. Unashangaa mantiki ya mtu kama Chenge kuwa mwanasheria mwenye shahada ya Uzamili lakini akatenda kama mtoto wa darasa la tatu. Kimsingi, taifa letu linatawaliwa na watu wasio na utu wala huruma; waroho na wenye roho mbaya wasiowajali wenzao.
          Sidhani kama wamarekani wanaosifika kwa utajiri wanaweza kusema maneno kama haya tena mbele ya vyombo vya habari. Kilichofanywa na wajivuni hawa ni kuonyesha kuwa tumegeuka taifa la kifisadi na kijivuni ambapo kila mtu anaweza kujipayukia atakavyo ilmradi afurahishe roho yake kama alivyowahi kusema rais Jakaya Kikwete kuwa furaha ujipe mwenyewe usingoje kupewa. Hata hivyo, ni kuumiza wengine kwa kujipa furaha kwa kuwaibia au kuwaudhi wengine.
           Ukifuatilia matamshi ya viongozi wetu, unabaki kuhuzunika. Nani amesahau maneno ya Kikwete kuwa wasichana wa shule za msingi na sekondari wanapata mimba kwa kiherehere chao bila kuangalia chanzo hasa cha jinai hii ambayo imetokana na kukithiri kwa ufisadi na wizi kiasi cha wenye fedha kuzitumia kuwahonga watoto wa shule na mahakimu wanapofikishwa mahakamani?
          Hivi shilingi milioni kumi ni mshahara wa miaka mingapi wa mwalimu, karani au mkunga? Hata hao matajiri wenye biashara zao tena zenye kusifika na halali hawawezi kuita shilingi milioni kumi fedha ya mboga. Hata hivyo, Tibaijuka alikuwa na uchungu gani na fedha husika kama anaweza kutumiwa mabilioni bila kueleza alichofanya? Sijui kama huyu analipa kodi vilivyo. Na ni ajabu kuwa pamoja na kuonyesha jeuri ya utajiri serikali haijambana arejeshe fedha hiyo kwa vile hawezi kuitolea maelezo ya ni kwanini alilipwa na kama alilipwa ni kwa kazi ipi wakati alikuwa mtumishi wa umma! Je mamlaka zinashindwa kuwashughulikia wajivuni kama hawa kutokana na kufanana na wakubwa wake wengi waliojificha nyuma ya vyeo? Nyodo hizi zinanikumbusha giriki aliyewahi kudai kuwa alikuwa ameiweka serikali ya awamu ya kwanza mfukoni mwake. Rais wa kwanza marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere aliposikia kufuru hizi aling’aka, “Hilo fuko linaloweza kuweka serikalina ukubwa kiasi gani?”  Punde si punde, Nyerere alimtimua mjivuni huyu bila kujali nini wala nini. Huu ndiyo uongozi wenye kuona mbali na uliotukuka. Kwani Nyerere alijua madhara ya kauli ile kama asingechukua hatua haraka. Baada ya madaraka kuwa ulaji wa dezo na wa kifisi, nani anakerwa na kauli kama hizi ambazo ni maudhi kwa wananchi? Nani amshughulikie nani wakati wote ni kambale wenye sharubu?
          Kwa jinsi mamlaka zinavyowaendekeza, kuwalea na kuwagwaya mafisadi na wezi wakubwa kwa vile wana fedha ya kuhonga, si vibaya kujenga dhana kuwa serikali yote inaundwa na wale wale wanaoweza kujipayukia bila vinywa vyao kuwasiliana na ubongo. Ni balaa kiasi gani kwa taifa?

          Tumalizie kwa kumpinga Tibaijuka kuwa hata huko Marekani wakubwa zetu wanakokesha wakijigonga na kutembeza bakuli bado shilingi milioni kumi si fedha ya mboga. Yatosha kusema kuwa maneno ya Tibaijuka ni ushahidi kuwa sifa zake zina mshikeli. Mtu anayetumia shilingi milioni kumi kwa mboga ahitaji kazi toka kwa umma wala hafai. Hivyo, sitegemei kama Tibaijuka atapitishwa na chama chake kugombea tena ubunge. Ili kutaka nini na kufanya nini wakati ameishajilipa?
Chanzo: Tanzania Daima Machi 11, 2015.

No comments: