Japo kashfa ya wizi wa mabilioni ya fedha za umma kupitia kashfa ya escrow umefutikwa chini ya busati, bado unazidi kuwaandama na kuwaumbua wakubwa wanaojifanya kutohusika wala kuchukua hatua dhidi ya wahalifu wakuu nchini. Taarifa za hivi karibuni kuwa maafisa sita wa ikulu wanatuhumiwa “kukatiwa mshiko” na mtuhumiwa mkuu wa escrow James Rugemalira si za kupuuza. Unaweza kuwa mwanzo wa mengi machafu na makubwa kufichuka ambapo utawakuta hata wale ambao hukuwategemea achilia mbali kuwataka wamshughulikie mwenzao na mtu wao.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa Mdhibiti Mkuu wa ikulu, Shaban Gurumo –pamoja na maafisa wengine watano wa serikali –anatuhumiwa kukatiwa jumla ya shilingi za kitanzania 800,000,000. Hii si hela ya ugolo. Ni kiasi kikubwa cha fedha ambacho kinaweza kujenga shule kama tatu hata nne za vijijini. Ni kiasi ambacho kinaweza kujenga zahanati kama nne au tano ukiachia mbali kuleta maji kwa vijiji kama kumi hivi. Hivi ni ufisi na uchafu kiasi gani kwa watu waliokabidhiwa dhamana –tena takatifu ya kuangalia ikulu –kushirikiana na majambazi kuibia taifa? Ama kweli alisema marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere kuwa alipong’atuka ikulu iligeuka pango la wezi badala ya kuwa patakatifu pa patakatifu kama ilivyokuwa chini ya utawala wake!
Japo taarifa za maafisa wa ikulu kukatiwa kitu kidogo na kikubwa hazijathibitishwa na mahakama, ukweli ni kwamba mafisadi wameiteka ikulu jambo ambalo ni kuiteka nchi hasa ikizingatiwa kuwa ikulu ndiyo moyo wa nchi. Je ikulu iliyotekwa na wahalifu na kusimamiwa na waroho na mafisadi inaweza kuitumikia nchi kama ilivyo azma ya kuwapo kwake? Je rais Jakaya Kikwete ameyasikia haya na kama ameyasikia anatwambia nini au kuchukua hatua gani kuonyesha yeye yuko upande gani? Wakati huu tunamtaka asikae kimya kama alivyofaya kwenye kashfa ya EPA ambayo ilimgusa karibu kila mmoja. Je atakaa kimya ili mambo yaishe au atawawajibisha wahusika ili angalau kupisha uchunguzi? Je ikulu inapoguswa vibaya namna hii, rais anaweza kusema hajui au ahusiki?
Japo tulishasema tangu zamani kuwa kuna namna ikulu inahusika na wizi wa escrow bila kusikilizwa,ukiangalia –kwa mfano – jinsi rais alivyomtoa kafara waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka huku waliomkatia hiyo fedha iliyosababisha atimuliwe wakiendelea kupeta, unapata wasi wasi tu kuwa ikulu inahusika bali imetiwa mfukoni tu. Kama haikutiwa mfukoni, inakuwaje watuhumiwa wakuu yaani Rugemalira na Harbinder Sethi Singh bado wako nje hata bila kuitwa kuhojiwa na mamlaka husika? Je kama wanufaika wa wizi huu wengine wako ikulu unategemea ni taasisi gani itawashughulikia watuhumiwa hawa? Wapo wanaolaumu Tume ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ambayo hivi karibuni ilikumbwa na kashfa ya kuwa moja ya taasisi zinazoongoza kwa kuomba na kupokea rushwa. Kimsingi TAKUKURU ambayo iko chini ya rais yaani ikulu haina ubavu wa kuwachukulia hatua washirika wa ikulu. Ni mbwa gani anaweza kumng’ata aliyemfuga? Akifanya hivyo atapigwa mpini na hatima yake itakuwa ni mzoga wake kutupwa machakani na kuozea huko na mambo kwisha.
Hatutaki tumuingize rais kwenye kashfa hii japo kitendo cha maofisa wake kutuhumiwa kinamuweka kwenye nafasi mbaya kimaadili. Kipindi fulani mke wa Kaisari, mtawala wa Kirumi alituhumiwa kwa uchafu. Akiwa anajitetea mbele ya mumewe Kaisari, mke wa Kaisari alisema kuwa ahusiki hata kidogo. Mume wake alimjibu kuwa achilia mbali mke wa Kaisari kuhusika na uchafu uaotuhumiwa nao. Mke wa Kaisari anapaswa kuwa msafi kiasi cha kutoweza hata kutuhumiwa. Watumishi wa ikulu hawana tofauti na mke wa Kaisari linapokuja suala la usafi kimaadili. Hawapaswi kutuhumiwa achilia mbali kutenda hicho wanachotuhumiwa nacho.
Kwa rais Kikwete kujisafisha yeye na serikali, ikulu yake na chama chake, anapaswa kuwachukulia hatua mara moja wote waliotajwa kwenye wizi wa escrow tena mara moja. Awasimamishe kazi wachunguzwe na matokeo ya uchunguzi kuwekwa hadharani. Kama atakuwa rais mchukia uchafu, atawawajibisha mara moja hata kama watasafishwa kutokana. Maana “mke wa Kaisari” hapaswi kutuhumiwa achilia mbali kutenda lile analotuhuiwa nalo.
Kama Kikwete atakaa kimya kama alivyozoea, sifa yake itaporomoka na wengi watadhani wezi wa escrow ndiyo wenye uamuzi wa mwisho. Haiwezekani isiwe hivyo iwapo wameishawaweka wengi mfukoni. Rejea mawaziri wawili kuondolewa na kashfa hii, majaji, viongozi wa kiroho wenye uroho na sasa maafisa wa patakatifu pa patakatifu. Kikwete anaweza kuchagua kukaa kimya ili mambo yapoe na kusahaulika. Ila ajue. Kuna siku yatafichuka –saa nyingine akiwa nje ya madaraka – na hii inaweza kumgharimu vibaya sana. Sidhani kama rais ajaye atakuwa kama yeye alivyomkingia kifua mtangulizi wake Benjamin Mkapa alipokumbwa na kashfa ya yeye, familia yake na marafiki zake kujitwalia mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira. Mambo huwa yanabadilika. Akina Fredrick Chiluba, Bakili Muluzi, Abdulaye Wade na wengine hawakujua kama mambo yangegeuka na kuwaacha pakanga.
Tumalizie kwa kumtaka rais Kikwete awawajibishe watuhumiwa mara moja ili kulinda hadhi yake, ikulu na ya taifa. Serikali yake pia iache kujivuta vuta kuwachukulia hatua watuhumiwa wakuu wa escrow kwa kuwatoa kafara waliopokea chumo la wizi huku wanaotuhumiwa kuiba wako nje wakitanua. Ama kweli escrow imeiteka hata ikulu! Tusingeshauri rais Kikwete aipe mashiko dhana hii kwa ukimya na kutojali. Taifa ni zaidi ya marafiki na washirika na isitoshe madaraka yana mwisho ambao kwa Kikwete ni mwishoni mwa mwaka huu.
Chanzo: Tanzania Daima Machi 4, 2015
No comments:
Post a Comment