Baada ya kungoja muda mrefu mkuu aje kukiaga bila mafanikio, Kijiwe kimekuja na ubunifu mwingine. Kwa vile jamaa amenogewa kwenda kutanua ughaibuni kwa kisingizio cha kuaga wageni utadhani ndio waliompa kula ya kura, basi Kijiwe kimeamua kumfuata huko.
Mgosi Machungi ndiye analinzisha kwa kulalamika, “Jamani hebu tisaidieni. Huyu mkuu mbona kia siku kiguu na njia akienda ughaibuni kuaga kunani jamani? Mbona hatimueewi au ndiyo anaaga njuuku zetu kwa kuzuua zaidi?”
Mijjinga anaamua kukamua mic hata kabla ya Mgosi hajamaliza, “Usemayo ni kweli. Kwani ni juzi tu alikuwa Ufaransa, Norway na Uswizi. Hata kabla hajapoa huyo, Australia. Nadhani kuna biashara ambayo hatujaijua inaendelea.”
Kapende anakula mic, “Wewe unashangaa hii. Juzi ukimsikia rahis Salama naye akiwa ziarani kule Malaya? Hawa inaonekana walilogezewe kuzurura.”
Mpemba anakula mic, “Unasemaje alhaj Kapende eti rahisa? Baba ni rahis na mama rahisa siyo? Hata hivyo, siamini kama hawa wazurura. Huenda wanayo miradi yao wenda kule kuikagua na kuchaji akaunti zao huku. Humuelewi hii? Hebu fikria kwa mfano umauona rahisa akikagua karakana za kutengeneza treni bila kuwa na waziri wa uchukuzi wala katibu wake mkuu. Anafanya hivyo kama nani kama si mradi wao?”
Machungi anakatua mic tena, “Jamani timfuate huko huko nasi timuage ndipo awaage wapendwa wake. Maana inaonekana kama hatina samani na kua zetu ziipotea bure.”
Mbwamwitu anakwanyua mic, “Acha mwenzenu aage. Maana, katika mambo yatakayomkondesha baada ya kuachia ulaji ni kukosa fursa ya kwenda kutanua ughaibuni. Kama tutapata mtu makini uwezekano wa watu kunyea debe ni mkubwa nawambia aminini.”
Mjumbe mpya Chilumba anaamua naye kula mic kwa mara ya kwanza, “Unadhani mwenzenu anakwenda kutanua tu? Kuna jamaa yangu mmoja wa inteligensia aliniambia kuwa jamaa huwa anahaha kutibu saratani. Ila aliniambia nisimwambie mtu maana hii ni top secret.”
Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kula mic, “We acha uongo. Kama uliambiwa usimwambie mtu kwani sisi unaowaambia ni nyani? Je huyo aliyekwambia alidhani ulikuwa nyani hadi akwambie mambo ambayo watu hawapaswi kujua au ni uongo na ujuha tu?”
Chilumba anajibu tena kwa hasira, “Da Sofi hata kama mimi ni mgeni tuheshimiane pasije kuchimbika bila jembe kwa kutetea huu uoza wako. Unadhani ninakundanganya wakati mimi mwenyewe ni mtu wa usalama?” Baada ya kutamka hayo tunaangaliana kuonyesha kuwa hii namba sasa hatari. Ni kamba tupu.
Mheshimiwa Bwege anadakia, “Mie ndiyo maana sitafanya kosa nikipe chama cha Maulaji kura yangu. Angalia mzee Tunituni che Nkapa. Alizurura na kuruhusu kimada wake aibe wee. Sasa wako wapi. Alikuja huyu mbayuwayu naye akamruhusi manzi wake aibe wee na kuzurura wee. Sasa yameisha. Nadhani kama tutamchagua mzee Kanywaji naye atageuka Vasco da Gama. Kwani kuzurura ndiyo sera yao tangu enzi za Nkapa che Makapi Tunituni wa Achimwene.”
Msomi Mkatatamaa aliyekuwa akiangalia na kutabasamu anaamua kutia daruga, “Nyinyi humjui. Mara nyingi chaguzi tunazofanya tunapiga kura kama kutimiza mradi tu hasa ikizingatiwa hawa waagwa ndiyo wanaolipia chaguzi na serikali tunazoita zetu. Kimsingi tunachojivunia kuwa uhuru si chochote wala lolote bali ukoloni mamboleo. Mbona mzee Mchonga alipoachia madaraka hakwenda kuaga hao wakoloni? Ni kwa sababu alikuwa hawategemei wala kujigonga gonga kwao.”
“Msomi umetoa mapwenti ya nguvu. Mbona Joji Kichaka alipomaliza muda wake wa kufanya ugaidi hakuja kuaga huku Uswekeni? Kweli nimeamini. Tunapaswa kudai uhuru upya ili tuwe na viongozi badala yak uwa na watawala na wazururaji ombaomba wenye kujigongagonga.” Anajibu Kapende.
“Yote tisa. Kumi ni pale waliojisahau baada ya kufadhiliwa kujikuta wakiwa uchi mbele ya kadamnasi. Sijui ndugu yangu Salva Rweyependekeza atakuwa mgeni wa nani baada ya Njaa Kaya kutimua?”
“Atarejea kwenye umbea wake na kutafuta wa kusifia ili ampe mlo hata kama ni mabaki ya mezani.”
“Kweli vatu mingi hapana jua kwanini kuu nenda aga ghaibuni. Kama veve nakwenda ombaomba napewa juluku kama hapana aga ile nakuja napata tabu. Fazili hapana nasaidia yeye sikini endesha kaya yake.”
“Kanji acha huni veve. Sasa iko sema kuva tafata Kwete ghaibu aga yeye. Mimi iko pendekeza Somi na Payukaji changia nenda ghaibu fata kuu eleza yote vananchi nataka.” Anachomekea Mbwamwitu kwa lafudhi ya Kihindi.
“Yakhe tuache utani wallahi. Wazo la Nbwamwitu la maana ati. Kwanini tusichangishane njuluku na kumtuma mtu au watu wawili kumfuata huko ghaibu na kumfikishia salamu zetu?” Mpemba anamuunga mkono Mbwamwitu.
Msomi anakula mic, “Hata kama jamaa huwa anajifanya hamnazo, angalau kitendo cha kumfuata kwenye matanuzi yake na kumghasi hakitambadili, kinaweza kumbeep atakayemrithi. Hivyo, naunga mkono mia kwa mia mpango huu ambao kama utafanikiwa unaweza kuwa suto kwa wengi wajao na wababaishaji kwenye ofisi kuu.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si ukapita msafara wa raisa Salama Kiwewe! Acha tuutoe mkuku kwa kuuzomea, kuumwagia kashata na kuurushia kahawa! Kimsingi, kwenye uchakachuaji ujao lazima nambari wani ipigwe chini. Maana hata ikimteua Kanywaji bado mambo yatakuwa yale yale. Heri kuwapa wapingaji nao wakajaribu kutuonyesha vitu vyao au vipi?
Chanzo: Tanzania Daima Julai 29, 2015.