Kashfa ya hivi karibuni iliyokikumba Chuo Kikuu cha St Joseph inapaswa kulifumbua taifa macho. Baada ya kuingia kwenye sera mbovu za kiliberali mamboleo za kubinafsisha kila kitu, nchi nyingi za kiafrika–ikiwamo Tanzania–zilipwakia kila aina ya takataka na ujinga. Tuliambiwa kuwa ubinafsishaji ndiyo chachu ya maendeleo ingawa maendeleo yenye hatujayaona. Badala ya uwekezaji kuleta maendeleo, umeleta maanguko katika nyanja nyingi ikiwemo elimu.
Nyanja ya elimu nchini ni mojawapo ya maeneo yanayoonekana kuathiriwa na sera za hovyo za uhuria ambao umegeuka uholela. Hivi karibuni kulifumka kashfa ambapo St. Joseph kilifungwa kutokana na:
Mosi, kutoa elimu chini ya kiwango ambayo matokeo yake ni wahitimu kuondoka chuoni wakiwa wamesheheni ujinga kiasi cha kutofanana na elimu wanayodai kuwa nayo ukiachia mbali kutoajiri. Hali hii ina athari kama vile kupoteza wahitimu muda ukiachia mbali kuwanyima hali ya kujiamini na kutoweza kuajirika kirahisi.
Pili, licha ya kutoa elimu chini ya viwango, iligundulika kuwa chuo hiki kilikuwa kikiwalangua, kuwahadaa, kuwatapeli na kuwaibia wanafunzi kwa kuwajaza ujinga. Je viko vyuo vingapi kanywabwoya kama hivi nchini na vimeishaibia na kuwahadaa ukiachia mbali kuwajaza ujinga wangapi?
Tatu, kuajiri wakufunzi wasio na ujuzi wa kutosha wala kukidhi viwango wa ufundishaji kwenye vyuo vikuu. Tunadhani kuwa kufungia chuo si jibu. Kwani chuo husika licha ya kufuja dhamana yake kimetenda makosa mengi ya jinai kama vile kutoa elimu na huduma mbovu, kulangua wanafunzi, kuharibu maisha ya wanafunzi, kuwaibia na pia kukiuka taratibu za uendeshaji taasisi ya elimu ya juu. Hivyo, chuo husika kinapaswa kuchuliwa hatua mojawapo zikiwa, kurejesha fedha za waathirika, kuwaomba msamaha, kuwalipa fidia wahusika na yote katika yote, kupigwa marufuku kutoa huduma yoyote ya kielimu nchini ili liwe soma kwa wengine wenye mawazo ya kuligeuza taifa letu shamba la bibi.
Mapungufu hayo matatu ni kati ya mengi ambayo hayakuwekwa wazi. Hata hivyo, malalamiko ya wanafunzi yaliyokaririwa na vyombo vya habari ni kwamba chuo kilikuwa kikiwatapeli kwa kuwapa alama za juu wakati wahusika hawakuwa na ujuzi wowote. Hali inakuwa mbaya hasa pale ukosefu wa ujuzi uliotarajiwa unapobainiwa na mwanafunzi mwenyewe na si muajiri wala mtu mwingine.
Je kwanini tumefika hapa? Nitaazima maneno ya rais John Pombe Magufuli aliyekaririwa akisema kuwa Tanzania ilikuwa imegeuzwa shamba la bibi na tawala mbovu na hovyo zilizopita ambapo kila kitu kilikuwa kikijiendea kana kwamba hapakuwapo na serikali. Kwa hiviyo basi, madhara ya ukosefu wa uongozi wenye visheni na mapenzi mwa taifa uliathiri kila idara na mahali nchini. Rejea jinsi umma ulivyomlalamikia waziri wa elimu na ufundi wa zamani Dk Shukuru Kawambwa kwa kuharibu elimu na rais ambaye alikuwa rafiki yake asimchukulie hatua.
Tokana na uoza huu uliokithiri nchini, tunashauri wizara inayohusika na Vyuo Vikuu ifanye yafuatayo:
Mosi, ihakikishe inatunga sheria na kupanga utaratibu wa kuwa na waangalizi na wakaguzi wake ndani ya vyuo vikuu vyote nchini.
Pili, ajira zote za walimu wa vyuo vikuu zisifanyike bila kuwasiliana na sheria ili kuangalia kama wanaojaliwa wanakidhi viwango vyote kuanzia elimu hata tabia kama vile rekodi za jinai, kwa wageni vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini.
Tatu, kuwepo na utaratibu wa wizara husika na vyuo vyenyewe kutumia mfumo huria unaotumika sana vyuo vya nje wa wanafunzi kuwafanyia tathmini walimu wao kila baada ya kumaliza muhula. Katika utaratibu huu, wanafunzi hupewa fomu za tathmini ambazo huzijaza bila kuandika majina yao (Anonymous) ili kuepuka kuwajengea woga au kuchelea kupatilizwa na watathminiwa. Mfumo huu huwajengea kuthaminiana, kuheshimiana na kutendeana haki wadau yaani walimu na wanafunzi wao. Huu ni mfumo unaojenga demokrasia kitaaluma, kujali, kuchapa kazi na ufanisi wa hali ya juu katika vyuo vingi katika nchi za magharibi. Maana, kila mdau anamtathmini mwenzake vilivyo. Kimsingi, elimu yetu inatolewa kwenye mazingira kandamizi ya kikale ambapo baadhi ya maprofesa hujigeuza miungu watu kiasi cha kuwaumiza wanafunzi badala ya kuwasaidia. Wengine hutumia udhaifu huu hata kujiingiza kwenye rushwa za ngono ambalo ni janga kwa vyuo vyetu nchini. Ni dhahiri, hakuna namna ya kujua ufanisi au vinginevyo vya walimu kama hakuna mfumo wa kupata taarifa na tathmini ya wanafunzi. Mfumo huu huondoa ubabe na ujinga wa baadhi ya walimu kuwaonea wanafunzi na kujiona kama miungu. Pia mfumo huu huondoa utegaji na ubabaishaji.
Nne baada ya serikali ya Magufuli kuthibitisha kuwa nchi yetu si maskini, kuna haja ya kuangalia namna ya kuwezesha kila mkoa kuwa na chuo kikuu angalau kimoja cha umma. Maana, unapokuwa na vyuo vingi vya umma, unapunguza uhitaji na uhaba wa vyuo kiasi cha kuondoa motisha wa majambazi yanayotumia elimu kuwajaza ujinga watu wetu.
Eneo jingine linalotaka uangalizi, ni kupambana na kughushi sifa za kielimu ambako husaidia na kuwezesha watu wasio na ujuzi kughushi na kuishia kuajiriwa kama walimu na wataalamu wakati si chochote si lolote.
Tumalizie kwa kuishauri serikali ikichukulie chuo husika hatua kali huku ikivisaka vyuo vingine hewa kama hivi ili kuepuka kulanguliwa na kuchezewa watu wetu. Unapochezea elimu, unaharibu mstakabali wa taifa kwa ujumla. Hivyo, suala hili lipewe uzito usio wa kawaida ili kuepuka kuendelea kuchezewa watu wetu na nchi yao.
Chanzo: Dira
2 comments:
Naam Mwalimu Mhango ni kweli kabisa sera mbovu za Kiliberali mambo leo za kubinafsisha kila kitu na kile walichokiita soko huria ndio chanzo au mwanzo wa mabalaa yote ya kuzifanya nchi zetu za kiafrika kiujumla na nchi yetu hususa kurudi nyuma kimaendeleo nakumbuka Mwalimu Nyerere alikuwa na hoja ya kuwanyamazisha wakosoaji wake wa siasa yake ya Ujamaa pale alipokuwa akiwauliza "Nionyesheni nchi yoyote ile ya kiafrika inayofuata siasa ya kibepari ambayo inafanya maendeleo kwa siasa hiyo ya kibepari"
Mimi naamini kabisa kwamba shindikizo waliowekewa nchi za kiafrika na nguvu za kibepari na za kabeberu kuukubali mfumo wa uchumi wa kiliberali au soko huria kwa kukidhi mahitaji ya mashiriika yao makubwa ya kibiashara kwa kuendelea kuziibia nchi zetu utajiri wake na rasilimali zake wizi ambao umekuja kwa utaratibu wa matual consent na viongozi wetu waliotudanganya kwamba ndio mwanzo wa maendeleo
Naam Mwalimu Mhango.kwa watanzania baada ya utawala wa Mwalimu Nyerere kulisikika malalamiko kwamba Mwalimu Nyerere amewanyima watanzania elimu na hatimae watanzania waka2a wengi wao wanajihisi upungufu muda wa kudumu tu hawana uw3zo mzuri wa kujieleza katika lugha ya kiingereza kama ilivyokuwa kwa wale waliotawaliwa na mkoloni wa kifaransa kwamba kifaransa ndio kila kitu kwa hiyo ikaambatanishwa kuongea kiingereza au kifaransa ndio elimu au umeelimika kwa mfumo huu wa kufikiri ilipokuja mfumo huu wa kiliberari tunakuta tu wajanja wakaingia sana kuwekeza ktk sekta ya elimu kwa shule binafsi kuanzia chekechea,msingi,sekondari mpaka chuo hatimae ndio hayo yaliyotokea na yanayotokea katika baadhi ya vyuo vikuu yva watu binafsi.
Lakini swali muhimu hapa la kujiuliza au linalojiuliza lenyewe je kama asingekuja rais Magufuli madarakani uhoza huu na ufisadi huu si ungekuwa ukweli wa kuendelea?Na katika ufisadi huu je hakuna uwezekano wa baadhi ya viongozi wa ngazi za juu kushiriki katika kuwatia wanafunzi wa kitanzania ujinga na wao kufaidika kiuchumi wakati watoto wao wanawasomesha nje ya nchi katika vyuo vyenye majina?Kama ilivyoathirika sekta hii ya kielimu kwa kupitia mfumo mbovu wa kileberali ndivyo hivyo hivyo wajanja hao hao na viongozi hao hao mafisadi walivyoiathiri sekta ya afya katika nchi yetu.
Na tuzidi tu kumuombea na kumpongeza rais wetu Magufuli kwa kutupia macho sekta zote hizo zinazogusa msatakibali wa vijana wetu na nchi yetu pia nakupongeza kwa kushauri ufumbuzi wa ufisadi huo ni matumaini yangu rais Magufuli na serikali yake watauzingatia na kuutekeleza.
Anon swali na shaka yako ni vya muhimu. Jibu la swali lako unalo hasa unapowaangalia watu kama January Makamba mtoto wa kihiyo na Dk Hussein Mwinyi walivyosomeshwa nje wakaja kurithi nafasi za wazazi wao. Hao ni wachache tunaowaona kwenye medani za kisiasa. Ukienda kwenye mabenki hasa BoT na wizara zenye mishiko na balozi zetu nje unaweza kuzimia kujua kuwa kumbe wakubwa ndiyo walioanzisha kiama hiki. Akina Msekwa watoto wao wamejazana kwenye balozi zetu nje. Nadhani walifanya makusudi ili watoto wao wapate wajinga wa kutawala kama wao. Tofauti ya Magufuli na wao ni kwamba yeye ametokea kwenye kizazi cha kajamba nani. Hivyo, anaelewa matatizo ya wenzake na ndiyo maana anakuwa mkali hivi ili angalau taifa liende mbele kwa pamoja. Tuombe Mungu wasimkolimbe au kumSokoine.
Post a Comment