The Chant of Savant

Tuesday 15 March 2016

Kijiwe chastukia sanaa za Lukuvi


            Hivi karibuni Kijiwe kilibaki kinywa wazi na maswali mia kidogo baada ya mjivuni mmoja kuja na mpya kuwa alikataa rushua ya madafu bilioni tano. Kukataa au kupokea si issue. Kinachogomba ni kutotoa ushahidi hata kiduchu. Issue hii aliinyaka Mijjinga ambaye anaileta kijiweni ili tuidurusu.
            Baada ya Mijjinga kuingia kwa madoido na mbwebwe anaamkua na kumwaga stori. Yeye hataki kusema mengi. Anabwaga gazeti la Danganyika Daima mezani na kuanza kutoa stori. Anakatua mic, “Hebu jionee wenyewe baadhi ya wajivuni wanavyotugeuza majuha na hamnazo.”
            Kabla ya kuendelea Mpemba ambaye alikuwa akivuta uradi anaamua kumuuuliza, “Yakhe mbona mie sikuelewi? Wamaanishani na nani huyu anayetaka kuwafanya hamnazo na majuha na kwanini?”
            Mijjinga anampoka gazeti Mchunguliaji ambaye alikuwa ameishalinyaka na kuanza kusoma. Anasoma kichwa cha habari, “Bill Lukuvi akataa rushua ya bilioni tano.”
            Kabla ya kuzama kwenye habari kamili, Mgosi Machungi anadakia, “Kumbe unaongelea hizi Sanaa za kutaka kumridhisha Dk Kanywaji ambaye anaonekana naye kupenda sifa kiasi cha kuanza kuvurunda? Umeona uteuzi wake wa wakubwa wa mikoa? Kuna sura ambazo hazikufaa hata kuwa wakubwa wa kijiji achia mbali mikoa.”
            “Bila kujipendekeza usawa huu hupati ulaji,” anachomekea Mbwamwitu huku akicheka.
            Msomi haridhishwi na mada ya Mpemba inavyopelekwa ndivyo sivyo. Anakula mic, “Hii stori kwanza haikubalanced. Mwandishi aliyemhoji Bill alikuwa kama anamfagilia. Nashangaa hakumuuliza kwanini hakuwaita Takokuru wawanyake hawa watoa rushwa au kuna kitu hataki kijulikana kama si kutaka umaarufu wa shilingi mbili.” Anakohoa kidogo na kuendelea, “Hata kwenye maelezo yake marefu hajaeleza atafanya nini kukomesha mchezo huu na wale ambao wamekuwa wakiushiriki atawafanya nini.”
            Kabla ya kuendelea Mipawa anampoka mic na kusema, “Huyu jamaa sijui anatuona sisi hamnazo au vipi. Umeona alivyoficha majina ya hao wenzake ukiachia mbali kupoteza fursa adimu ya kuwatia adabu. Maana sheria iko wazi. Kama ukikuta mtu anatenda kosa la jinai au yuko kwenye harakati za kulitenda, unatoa taarifa kwa vyombo husika.  Je huyu–kama si kutaka sifa za shilingi mbili kama ulivyosema Dk Msomi–alishindwa nini kuweka mtego na kuwakamata wanaharamu hawa? Cha kushangaza utakuta wanaofanya hujuma hii kwa kaya ni ima raia wa karatasi au wachukuaji uchwara wanaoshirikiana na akina Bill hao hao wanaojifanya kuwageuka. Si waseme kuwa dili halikuwaiva.”
            Mgosi Machungi naye anapoka mic na kuronga, “Hebu tifanye anaisis kidogo hapa. Kwanza, kwanini Bii ameficha majina ya hawa jamaa kama si washiika wake? Pii, imekuwaje hakutaka kuwakamata ii afichue mtandao wote wa wanaoibia kaya? Je inakuwaje seikai iuziwe aidhi yake yenyewe kama hakna namna? Je hawa jamaa waijuaje kuwa Kigamboni kutakuwa mai au nao wana siikai yao ndani ya siikai? Tiambie tiewe bwana Bii popote uiko.Vinginevyo huu ni uongo wa kawaida kama si usanii tu. Go tell it to the birds Bill humpati mtu hapa.”
            Msomi anaendelea, “Mimi hakuna aliponiacha hoi Bill kama kusema eti kuna wakubwa wamejilimbikizia ardhi lakini asiwateje wala kusema atawachukulia hatua gani. Ni ajabu kuwa na watu wanaofanya vitu kana kwamba hawakwenda shule. Unawezaje kuja na madai ya kitoto kama haya usichelee kuumbuliwa na wasomi kama sisi? Nadhani–kama rahis Kanywaji asingekuwa anendesha kaya kama mali yake binafsi kwa kujizungushia marafiki na waramba viatu–Bill alipaswa kutumbuliwa jipu mara moja. Maana hafai hata kidogo.”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kula mic, “Nyie kumbe hamfahamu hizi Sanaa? Kwani hapa kuna utumbuaji majibu au vipele na vijipu uchungu? Huwezi kutumbua majipu ukawa na watu kama Bill au Muongo wanaokumbwa na kashfa kama vile kughushi na Escrew. Mie sitaki nionekane mwanga. Huyu jamaa atachemsha muda si mrefu. Mliona alivyokwenda banki kubwa kwa pupa na kutoa maagizo kuwa wafanyakazi hewa wafutwe badala ya kuagiza waliowaajiri wapelekwe kwa pilato? Huku ndiyo kutumbua majipu au kuyafuga. Yeye anatoa amri ya kufutwa majina badala ya kuyatumia kama ushahidi kama nani? Kwani hii kaya ni mali ya mama yake? Kama yeye anafanya hivyo, kwanini wapambe na waramba viatu wanaotaka kumuingiza mkenge wasifanye mambo ya hovyo kama Bill kutoa habari za uongo?”
            Kanji aliyekuwa anateta jambo na mshikaji wake Sofia Lion aka Kanungaemba anakula mic, “Hata mimi hii iko changanya mimi sana. Sasa kama yeye shinda kamata hii jambazi natangaza nini kama si ongo tupu? Kwanza mimi hapana ami kama swahili naweza pewa feza kuba kama hii natakataa wakati sahara yake dogo sana.”
            Sofi anamuunga mkono Kanji, “Kuna uwezekano mkubwa kuna ukweli uliofichwa. Maana, ukiangalia usawa huu, na namna habari yenyewe ilivyoparaganyika na kuacha maswali mengi, unashindwa kuelewa lengo la Bill. Kama ni kutaka umaarufu nadhani hapa amepiga chini. Naungana mkono na wanaotaka atumbuliwe haraka. Maana, naye ni jip utu.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shankupe la Bill. Acha tuliotoa mkuku tukitaka tumtumbue jipu kama bosi wake anamgwaya au kumkingia kifua!
Chanzo: Tanzania Daima, Machi 16, 2016.

No comments: