The Chant of Savant

Wednesday 9 March 2016

Kijiwe: Makonda acha kudhalilisha walimu


            Baada ya mkuu wa wilaya ya Kinondo Po Makonda kuchemsha kwa kuja na mpango wa kudhalilisha wanafunzi, Kijiwe kimekaa kama kamati kulaani ujinga huu. Pia kijiwe kinatoa mapendekezo ya nini kifanyike kuepuka baadhi ya wazito kutumia matatizo ya wachovu kujipendekeza kwa Dk Kanywaji ili aendelee kuwabikiza kwenye ulaji.
            Mgosi Machungi ambaye alikuwa mwalimu kabla ya kuacha baada ya kuona ualimu ulivyokuwa umesahaulika na kuzikwa na kubakia kuwa kazi ya kudhalilishwa na wito anakula mic, “Wagoshi leo nina hasiaa sana. Mmemsikia huyu mtafuta uaji akijipendekeza kwa Dk Kanywaji akisema eti waimu wapande daadaa bure kana kwamba wanafanya kazi ya Bwana” sijui ametumia akii gani zaidi ya matope”      
            Kapende anajibu, “Unamshangaa huyu bingwa wa kujikomba ili asitimuliwe kwenye ulaji baada ya kuteuliwa kimazabe ukiachia mbali kudhalilisha ukuu wa wilaya? Nami nimesoma upuuzi huu kwenye magazeti na kupandwa na hasira nusu nimtafute mtoto wa mtu na kumfanya kitu mbaya; kama siyo ustaarabu wangu.”
            Kanji leo naye anahiwahi kula mic. Anazoza, “Hata mimi sangaa sana hii toto. Kwanini fanya walimu sikini sana? Kama napanda dala dala bure ile konda tafanyie yeye huni kama nafanyia toto ya sule. Takuwa aibu sana kwa walimu kama takubali hii jinga.”
            Msomi Mkatatamaa anakatua mic, “Nadhani huyu aliyekuja na pendekezo hili la kidhalilishaji na kimaskini ameonyesha alivyo maskini upstairs. Kwanini walimu wasafiri bure kana kwamba hawalipwi mishahara? Je kusafiri bure ndiyo jibu?”
            Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anamchomekea, “Kwa huyu mjikombi aliyelitoa ni jibu. Sijui wakienda na hotelini wale bure?”
            Msomi anaendelea, “Nadhani baadhi ya watawala wetu wana mawazo mgando na ya kimaskini. Kama wanataka kuwasaidia walimu –au kama wana uchungu na elimu –wawape maslahi mazuri walimu badala ya kutaka kuwaingiza mkenge kuwa wanawajali wakati wanataka kuwadhalilisha ukiachia mbali kuwanyanyasa. Sijui kama walimu nao watakuwa hamnazo wakubaliane na upuuzi huu?”
            Mipawa anachomekea, “Mbona walimu wameishamuonya jamaa aache kutumia matatizo yao kujipendekeza ili asitumbuliwe jipu? Walimu walimtolea kavu kavu kuwa hawahitaji msaada wala hawakumuomba awe msemaji wala mtetezi wao.  Kwani wana chama chao tena imara tu.”
            Mijjing aliyekuwa akisikiliza kwa makini huku akiweka vizuri ulimi wake wa nyoka vizuri kifuani anaamua kupoka mic, “Nyie kumbe hamjui! Huyu dogo baada ya kusifiwa kujamba sasa anataka kupoop. Anafanya kila awezacho hata visivyoingia akilini ili kumfurahisha Dk Kanywaji ili aingie mkenge asimtumbue jipu au ampandishe cheo baadaye ajute. Sijawahi kuona mtu wa hovyo na mwenye mawazo ya hovyo kama huyu anayetaka kuua elimu kwa kuwadhalilisha walimu. Walimu si maskini kiasi hicho. Kwanza, nani alimtuma awe mtetezi na msemaji wa walimu? Ama kweli jina baya humuharibu mwenyewe. Huyu jamaa kweli amekonda kiakili kweli kweli.”
            Sofia Lion aka Kunungaembe anakula mic, “Hata nami naungana mkono na wale wanaoona kuwa huu licha ya kuwa udhalilishaji wa walimu ni upuuzi. Kwanini zipatikane elimu za kutoa elimu bure sikosekane pesa za kutosha kuwalipa walimu wakajilipia nauli? Je tatizo la walimu ni nauli tu? Je wale wanaosafiri wiki nzima kuendea mishahara yao kwenye makao makuu ya wilaya nao wafanye nini? Shame on him!” anamalizia kwa ung’eng’e kiasi cha kuacha kijiwe hakina mbavu. Maana yeye si mpenzi wa kiswanglish kama alivyo Dk Kanywaji ambaye juzi alionyesha kuwa anahitaji kusoma tena grammar tokana na ung’eng’e wake kutonyooka ukiachia mbali kuchanganya na uswa.
             Mheshimiwa Bwege aliyekuwa akisoma habari ya Makonda kutaka walimu wasafiri bure huku akitabasamu na kutikisa kichwa anakula mic, “Japo Dk Kanywaji amemsifia huyu dogo kuwa alitatua matatizo ya ardhi, nadhani anapaswa kufikiri upya. Sijawahi kuona ubabaishaji unaoanza kuonyeshwa na baadhi ya watendaji kwa kisingizio cha kumfurahisha na kwenda na kasi ya rais. Kila siku utasoma magazeti mkubwa fulani amfukuza mkubwa fulani wa chini yake. Sijui kama wanafuata sheria au wanataka kuanzisha vurugu kiutendaji. Kwanini –kama kweli Dk Kanywaji anataka kubadili kaya hii iliyoozeshwa na awamu zilizopita –asifumue na kuufuma upya mfumo wetu wa hovyo? Kuhusiana na Makonda, huu ni mwanzo tu. Mtaona madudu yake mengi zaidi ya yale ambayo mmeishaona. Hafai kiumbe huyu. Ila ashukuru siasa za kulindana kama alivyosema Jan Makamba kuwa utawala uliopita ulijaa kulindana na kuoneana haya.”
            Mpemba ambaye alikuwa akisikiliza kwa makini anaamua naye kula mic, “Yakhe mie nshangaa sana huyu bwana. Yeye adhani kuwa tatizo la walimu usafiri tu? Kwanini haongelei mishahara midogo, mazingira magumu ya kufundishia na kuishi maisha ya kifakiri? Kama ataka wasaidia basi atetee mambo ya maana badala ya huu udoho udoho uso na maana yoyote zaidi ya kuendelea kumfichua alivo wa hovyo.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si yakapita maandamano ya walimu wakimsaka Makonda wampe vipande vyake aache kuwatumia kutafuta ulaji!
Chanzo: Tanzania Daima, Machi, 8, 2016.

No comments: