Tangu alipoingia kwenye ulaji baada ya kuchukua ukanda toka kwa Njaa Kaya aliyeonekana kuwa kilaza kiutawala kiasi cha kuigeuza kaya shamba la bibi kama alivyodai rahis hivi karibuni, nilitokezea kumzimikia rahis Dk John Kanywaji Makufuli. Nilichetuliwa na kasi na namna yake ya kuwasaka na kuwatumbua majipu wagonjwa wa ufisadi. Hata hivyo, tangu juzi alipotangaza timu yake ya wakubwa wa mikoa, badala ya kumzimikia, natamani nimuwakie kama si kumbwatukia. Maana, ametoa rungu kwa machizani ili watuumize tena watakavyo ukiachia mbali kuwaangiza watembeze undavandava hata kama ni kwa makosa ilmradi baadaye warekebishe.
Hakuna kauli iliyonkata na kunifanya nivute na kunywa kama sina akili nzuri kama kuwapa ulaji wageshi wastaafu wakati kuna vijana wengi–tena waliobukua mambo ya siasa na ma-political sciences na madude mengine magumu yahusuyo utawala–wanaoweza kutawala hiyo mikoa bila kulazimisha wala kutoa maamuzi bora maamuzi ili warekebishe baadaye kama alivyowaagiza. Kikatiba, wageshi hawapaswi kujiingiza kwenye siasa hata kama wamestaafu isitoshe siasa zenyewe zinapokuwa za majitaka na kupeana fadhila. Hii maana yake ni kwamba hawa jamaa walikuwa na kadi za nambari wani kibindoni jambo ambalo ni kosa la jinai. Ina maana walikuwa wakifanya kazi ya umma na kulipwa njuluku wakati wamevunja sheria ukiachia mbali upendeleo na kupokea amri za kijinga kama kusimamia uchakachuaji wa kura. Ndiyo maana jamaa amewaamini na kuwaachia kila kitu wafanye watakavyo. Nadhani hapa kamchezo kachafu ka kulipana fadhila karudufiwa. Katika kuwafunda na kuwaagiza, rahis Makufuli alisikika akisema ni heri wafanya maamuzi hata kama ni mabaya watarekebisha baadaye kuliko kutofanya maamuzi. Je kinachotakiwa hapa ni kufanya maamuzi au kuchukua maamuzi ya maana? Kwa walevi, heri mtawala asiyefanya maamuzi ya hovyo ili arekebishe baadaye kuliko anayechukua maamuzi ya kijinga na kutegemea kufanya maamuzi mazuri baadaye. Kwani kazi ya ukubwa wa mikoa ni ya majaribio ya kufanya au kuchukua maamuzi au namna ya kuwafundisha wageshi wastaafu mambo ya utawala?
Kama haikutosha, jamaa aliwaambia wakamate walevi na kusweka ndani hasa wale akina sie tunaoshinda vijiweni kutokana na kutokuwa na ajira. Hebu fikiri. Wachizani kama jamaa yangu Po Makondakonda ambaye alishasweka ndani wahishimiwa na watumishi wengine wa halmashauri atatumiaje rungu hili? Kwani kaya yetu ni ya kigeshi au vipi? Tuambizane kabla ya kuchenchiana bwana. Mbona akina Jimmy Rugemalayer, Roastatamu Kagoda, Singansinga Sethii na mzee wa Vijisenti na majambazi wengi waliosababisha umaskini na ukosefu wa ajira hawakamatwi kama hapa siyo usanii wa Ki-SISIEM?
Simuwakii wala kumbwatukia rahis Makufuli. Badala yake nampa ushauri wa bure. Kama anaamini kuwa wageshi ndiyo wanaweza kukomesha matatizo ya kaya bila kufumua mfumo na kuufuma upya anajidanganya ten asana. Mara hii amesahau tulivyoambiwa kuwa Njaa Kaya alikuwa mgeshi. Hivyo angeweza kuinyoosha kaya akaishia kuiharibu hadi kumpa ujiko Makufuli? Kinachotakiwa si ugeshi wala utishi bali kufuata sheria na kubadili mfumo mfu na muovu ulioanzishwa baada ya kung’atuka mzee Mchonga wa Burito. Hata ukitumia bangi na kanywaji, huwezi kutoa amri za kutatua matatizo ya miaka zaidi ya thelathini ndani ya siku 15. It is impossible sir.
Kitu kingine kinachonifanya nitamani kumuwakia Makufuli ni ile kutoa maagizo ya kihasara hasara kama vile kuwaambia wakubwa wa mikoa na wale wa Banki kubwa kuwa wafute majina ya wafanyakazi hewa ili kuanza upya. Tutaanzaje upya bila kuwakamata na kuwashughulikia walioajiri wafanyakazi hewa na kupiga njuluku kwa miaka nenda rudi?
Nijuavyo aina mpya ya utawala unaoanza kuota mizizi wa kumridhisha Dk Kanywaji, wahusika watakwenda kuumiza walevi bila sababu ili kumridhisha bosi wao. Tushawaona wengi hasa kwenye jiji la Bongo ambako jamaa yangu Makondakta alifanya kila vituko kwa kuvunja kila sheria kitabuni kuhakikisha anamuingiza mkenge Makufuli na kuishia kupewa rungu zaidi ili avurunde zaidi. Siku moja ataniambia kama si kukumbuka haya ninayochora hapa. Angajua usanii wa huyu dogo wala asingejivunjia heshima kumpigia debe wazi wazi. Atajuta baadaye baada ya malalamiko kuzidi juu ya tabia yake ya umungumtu itakapoanza kujitokeza na kuumiza wale anaodai analenga kuwaondolea kero. Sijui kama kuruhusu wakubwa wa mikoa kufanya watakavyo kama ni kuwasaidia walevi. Ni kama ametangaza utawala wa kigeshi kwa mlango wa nyuma asijue madhara yake. Walevi tunapinga kukamatwa na kuswekwa ndani au kuburuzwa simply because wahusika wanataka wajijenge na kumfurahisha muungumtu wao aliyewaumba. Huwezi kuendesha kaya kwa amri ya mtu badala ya kanuni zilizotugwa na kukubaliwa na wanakaya wenyewe. Huu ni uimla hata kama tunaambwa una nia nzuri.
Nimalizie kwa kuwamba wahusika warejeshe kaya yetu kwenye utawala wa kiraia badala ya kuigesisha kwa mlango wa nyuma. Hii kaya ni ya walevi wote bila kujali kazi wala vyeo vyao. Natamani nimuwakie jamaa niliyemzimikia sasa anaanza kuniangusha.
Chanzo: Nipashe, Machi 26, 2016.
No comments:
Post a Comment