The Chant of Savant

Tuesday 15 March 2016

Magufuli usitegemee kuombewa uchukue hatua

            Akiwa mkoani Arusha baada ya kuweka jiwe na msingi la ujenzi wa barabara ya inayoelekea Nchini Kenya yenye urefu wa Km 234.3 hadi Holili rais John Pombe Magufuli aliwaambia wananchi kuwa Tanzania ilikuwa imegeuzwa shamba la bibi. Pia aliwaomba wamuombee ili aweze kufanya kazi ngumu ya kuisafisha nchi na kuirejesha kwenye mstari, kazi ambayo ni hatari na ngumu. Magufuli aliyasema haya huko Tengeru.
            Kwanza ni kweli kuwa Tanzania tangu baada ya kung’atuka kwa baba wa taifa Mwl Julius Nyerere mwaka 1985 hadi Magufuli anaapishwa, ilikuwa si shamba la bibi tu bali chaka la wezi waroho na wenye roho mbaya. Kimsingi, tawala zote ukiondoa wa awamu ya kwanza, ziliongozwa na viongozi wasio na visheni wala uchungu na taifa. Ili tusionekane tunawapunja marais wastaafu, tutatoa mifano. Nani mara hii amesahau kuwa serikali ya awamu ya pili iliyosifika kwa falsafa ya hovyo ya ruksa iliasisi ufisadi? Rejea kashfa ya uuzwaji wa mbuga ya wanyama ya Loliondo, vimemo vya mikopo ya daladala na utoaji wa viwanja. Awamu ya pili iliyofuata ya Benjamin Mkapa ya kauli mbiu ya Ukweli na Uwazi vilivyokuwa kinyume imeondoka na kashfa nyingi kuliko ya awamu ya pili ya Ali Hassan Mwinyi. Kwani, hadi anaondoka madarakani, Mkapa alikuwa ameasisi kashfa za EPA ambayo iliasisiwa kumsaidia mgombea aliyeshinda na kumrithi Mkapa, Rada, Ndege mbovu ya rais, uuzwaji wa iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Ubinafsishaji wa kijambazi, uzururaji uliofanywa na rais na washikaji zake, na mwisho wa yote utwaliwaji wa Machimbo ya Makaa ya Mawe ya Kiwira kati ya mengine bila kusahau NGO ya ulaji ya mkewe ufisadi uliorithiwa na mke wa aliyemrithi. Hadi sasa Magufuli ameuepa mtego huu. Kwani, hatujasikia NGO ya mkewe.
            Baada ya Mkapa kuondoka madarakani, iliingia awamu ya nne ambayo imevunja rekodi kwa uchafu.ilifikia mahali watu wakasema nchi ilikuwa ikijiendesha. Wengine walisema ilikuwa kama ndege au meli iliyoko kwenye autopilot–hawa kwa kiasi fulani waliipendelea. Rais wa awamu hii Jakaya Kikwete alisifika kwa kupenda kuzurura nje hadi akaitwa Vasco da Gama, yule jambazi wa kireno aliyezunguka dunia akitafuta makoloni na sehemu za kuiba. Kikwete atakumbukwa kwa kuwa na serikali kubwa isiyofanya kitu (a big and do-nothing government) iliyoundwa ima na marafiki zake wa karibu, waramba makalio na wengine wengi. Kikwete hakuachia hapo–kama alivyodai waziri wake mmoja January Makamba kuwa serikali ya Kikwete ilijaa kulindana na kuoneana aibu–aliruhusu mafisadi kila aina wajiibie watakavyo kiasi cha kugeuka hiki anachosema rais Magufuli–shamba la bibi.
            Historia ya uovo wa serikali za awamu za pili, tatu na nne ni ndefu. Kwa vile Magufuli amegundua huu uhovyo, ugumu na hatari ya kazi yenyewe na jinsi waliozoea kunufaika na upuuzi huu wanavyotaka kumkwamisha, anapaswa kuchukua hatua madhubuti za–ikiwezekana–kuwakamata kwanza akasema baadaye badala ya kusema kabla hajawaweka sehemu salama. Nadhani alipoua Edward Sokoine alikuwa shule. Hata hivyo, anajua kilichotokea. Hivyo, tunamkumbusha, awe msiri kama chui. Akamate kwanza atangaze baadaye. Hana haja ya kulalamika wala kueleza mipango yake zaidi ya kukamata kwanza akatangaza baadaye. Anapaswa awe simba mwenda kimya badala ya kuwapa faida wabaya zake ambao ni wabaya wa wananchi.
            Tokana na ugumu na hatari ya kazi anayofanya Magufuli alisikika akiomba wananchi wamuombee. Kuomba si jibu wala siyo kile anachopaswa kufanya. Wananchi watamwombea. Ila ajua maombi mengine huwa hayajibiwi au hujibiwa baada ya muda mrefu hasa ikizingatiwa shaka ya usafi wa wanaomwombea ambao wanaweza kuhongwa udohodoho au hata wengi wao kutamani wapate fursa waibe. Hao hao anaotaka wamwombee wengi wao ndiyo wanaokula na hao anaotaka kuwatumbua majipu. Unaweza kuona jinsi ulivyoibuka utitiri wa makanisa, makundi na viongozi wa kiroho kujifanya wanaliombea taifa kana kwamba lilipokuwa likigeuzwa shamba la bibi hawakuwapo. Hawa wanaomba kweli au wanatafuta ukaribu na ulaji? Tanzania–nilishaandika mara nyingi tu–ahitaji kuombewa bali kuambiwa na kukombolewa na watu wasio na mchezo na nyani. Hata Magufuli ahitaji kuombewa bali kusadiwa na kushirikiana naye kufichua maovu.
            Hivyo basi, tumalizie kwa kumshauri Magufuli aachane na matangazo, malalamiko wala maombi. Badala yake akamate majibu na kuyakamua kimya kimya halafu atangaze. Akiendelea na staili hii, atakwamishwa kweli kweli hata na wale anaodhani ni wenzake wakati ni maadui zake. Wapo wengi waliomuunga mkono wanaojuta kwa kufanya kosa kubwa tu. Kama alivyowaambia viongozi wa Jumuia ya Afrika Mashariki, awahakikishie waovu hawa kuwa walifanya kosa kubwa kumuunga mkono na kumpitisha wakati wao ni wachafu kama nguruwe hata wawe wakubwa kiasi gani.  Kama Magufuli anataka kuikomboa Tanzania basi aanze kuwatumbua hawa waliosababisha iwe shamba la bibi. Kwani walizembea kwenye majukumu yao. Anawajua; tunawajua; na wanajijua.
Chanzo: Tanzania Daima, Machi 13, 2016.

No comments: