Hali ya upungufu na ulanguzi wa sukari unaolikabili taifa imezua maswali mengi kuliko majibu. Wapo wanaomlaumu rais John Pombe Magufuli kwa kuchukua hatua kali ambazo zimewaathiri wafanyabiashara waliozea kuuza sukari ya bei nafuu waliyokuwa wakiiagiza toka nje hata “kama imeisha muda wa matumizi” kama alivyowahi kusema rais Magufuli. Wafanyabiashara hawa fisadi na waroho waliamua kufanya hivyo ili kupata faida ya haraka haraka hata kama ni kwa kuhatarisha afya za walaji ukiachia mbali kuua viwanda na kilimo cha miwa nchini. Ni ajabu kwa nchi yenye viwanda vinne vya sukari kuagiza sukari nje huku wakulima wakikosa pa kuuza miwa yao. Huu ni uhujumu wa uchumi. Hakuna jina jingine stahiki linaweza kutumika kuelezea jinai hii iliyotokana na uwepo wa serikali fisadi na legelege ambayo wafanyabiashara waroho wachache walikuwa wameiweka mifukoni na kuitumia kama kijiko kuchotea utajiri bila kutoa jasho.
Hata hivyo, wapo wanaolaumu hata bila kunagalia upande wa pili wa taifa na watu wake. Wao wanaangalia uwekezaji na faida zake bila kuangalia hasara na madhara kwa walaji hasa wananchi hasa ikizingatiwa kuwa awamu mbili zilizopita ziliingia mikataba ya kijambazi kwenye uwekezaji karibu katika sekta zote. Hili nalo ni jipu kwa Magufuli kutumbua ili kurejesha nchi katika mstari kama alivyoahidi kwenye kampeni za uchaguzi uliomuingiza madarakani.
Wanaomlaumu Magufuli wanasahau kuwa yeye si wa kwanza kuchukua hatua kama anazochukua ili kulinda afya, uhai na uchumi wa mtanzania. Mchezo wa wafanyabiashara kuficha bidhaa ili wawalangua walaji umekuwapo tangu enzi za awamu ya kwanza ambapo marehemu baba wa taifa akishirikiana na waziri wake mkuu marehemu Edward Sokoine walimua kuwakamata walanguzi na waficha bidhaa tena bila kutoa onyo kama ambavyo Magufuli amekuwa akifanya. Tuwakumbushe ambao hawakuwapo wala hawajui kilichotokea. Waziri mkuu Sokoine siku chache kabla ya kuaga dunia hapo Machi 7, 1983 alikaririwa akisema “Tumeruhusu Walanguzi na Wahujumu Uchumi kuongoza nchi. Wananchi wamefika mahali ambapo wanashindwa kutofautisha kati ya viongozi wa chama (CCM) na Serikali na Walanguzi na Wahujumu uchumi wa nchi.” Haya ni maneno ya kamanda aliyeongoza vita dhidi ya uhujumu uchumi uliokuwa ukifanywa kwa kuficha bidhaa ili kuwalangua walaji kama ilivyo sasa. Hivyo, kwa kutoa historia hii kidogo, angalau tunaweza kudurusu nini kifanyike na kwanini.
Aliyekuwa mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba alikaririwa akisema, “Kauli ya serikali ya kuzuia utolewaji wa vibali vya uingizwa wa sukari kutoka nje ndiyo iliyosababisha upungufu wa sukari, asiuaminishe umma kuwa sababu ni wafanyabiashara kuficha sukari.” Lipumba kama mchumi aliliangalia sakata la sukari kiuchumi hasa uchumi wenyewe wa kiliberali mamboleo ambao haujali umma bali faida. Alimlaumu rais huku akijipinga kwa kusema, “Ingawa utolewaji wa vibali utaathiri viwanda vya ndani kutokana na kushindwa kushindana na wafanyabiashara, ni vema serikali ikatoa vibali kwa watu wote,” hii kauli ni tata. Kwanini Lipumba hakueleza ni kwanini viwanda vya ndani vilishindwa kushindana na vya nje? Jibu liko wazi kuwa wakulima wengi ambapo sukari inaagizwa–tena ambayo inakaribia kuisha muda wake–wanakuwa wameishapata chao. Isitoshe nchi kama Brazil ambako sukari nyingi inaagizwa–licha ya kuwa ya bei ndogo tokana na kukaribia kuisha muda wa matumizi–ina fuko maalum kusaidia sekta ya kilimo na ufugaji. Mfano, kwa mujibu wa http://thehandthatfeedsus.org/index.cfm, mwaka 2008/09 wakulima na wafugaji nchini huko walipata jumla ya dola za kimarekani 38 billioni kwa ajili ya kuwawezesha kupata mikopo na usaidizi mwingine. Hivyo, hata bila kuuza sukari iliyokaribia kuisha muda wake, wakulima wa Brazil hawawezi kushindana na wetu. Si hilo tu, Brazil haiuruhusu ushindani anaoutetea Lipumba inapokuja kwenye zao kama sukari inalozalisha kwa wingi duniani.
Wanaomlaumu Magufuli wanamuonea tu ima kwa sababu za kisiasa au ugumu wa kuelewa kama si kuwa watetezi wa wafanyabiashara wahujumu uchumi wanaoficha sukari ili wawalangue wananchi. Kama watakumbuka jinsi Magufuli alivyosema wazi wazi kuwa anatarajia kujenga Tanzania ya viwanda vikubwa na vya kati, watakubaliana nasi kuwa hawezi kufanya hivyo bila kulinda viwanda vilivyopo ili kutoa motisha kwa wengine kuanzisha viwanda. Kimsingi, wakosoaji wa Magufuli wanapaswa kukubali na kufahamu kuwa zoezi hili litakuwa na mauvimivu kidogo kabla ya mambo kutulia na watu wakafuata sheria na kutengeneza faida kwa kufuata sheria.
Ukiachia sukari inayoagizwa kutoka nje japo si yote kuwa ya bei nafuu kutokana na kununuliwa kwa bei nafuu ima kutokana na ubora wake au hali ya wakulima huko itokako, si siri kuwa wafanyabiashara wengi nchi walikuwa wamezoea kuingiza bidhaa na kufanya biashara bila kulipa kodi inavyostahili. Hivyo, ujio wa Magufuli umewapunguzia faida ya haraka haraka kiasi cha kuwachukiza. Hawaendekezi kama seriakali mbili zilizopita ambazo hazikukusanya kodi ukiachia mbali kutoa misamaha kibao ya kodi. Kama watanzania tunataka kujenga taifa la viwanda, hatuna budi kuweka uzalendo mbele badala ya kulaumulaumu hata mahali pasipohitaji lawama.
Tumalizie kwa kusema kuwa wanaomlaumu Magufuli kwa uhaba wa sukari ni kama wanamuonea badala ya kutoa mchango wa nini kifanyike. Suala la sukari haliwezi kuachwa liendelea bila utatuzi huku walaji wakilanguliwa na kuuziwa bidhaa mbovu na hatari kwa afya zao. Hili liko wazi;na halihitaji utaalamu wala ubobezi.
Chanzo: Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment