Kisa cha hivi karibuni cha afande mmoja kukataa kunyanyaswa kwa mjuba na limbukeni mmoja kutaka kutumia ukubwa wa bedroom, kimenilazimisha kuandika makala hii. Kwa wasiojua inshu nzima ni kwamba huko Namanga jijini Dar-Si-Salama, mke mmoja wa waziri mwandamizi alitoa mpya alipojifanya waziri eti kwa vile mumewe ni waziri. Kama unataka ukubwa si ugombee hata ule ubunge wa vitu vya dezo ambao umezua kasheshe mjengoni hivi karibuni baada ya mwishiwa mmoja ambaye akina mother walimwita teja kuwaita babies bimana wanabebwa na kubembezwa ili kupata ulaji.
Bila aibu wala kutumia chembe ya akili, bi waziri alitaka kumdhalilisha afande pale alipomdaka dereva wake baada ya kusimama kwenye mstari wa pundamilia ambao ni kuvukia walevi asijue ndata naye anajua mipaka ya ulaji wake! Afande alipoamua kutimiza wajibu wake, acha bi mkubwa huyu–mshamba na dandizi, bila shaka–amporomoshee mvua ya matusi. Maskini bi mkubwa huyu alisahau kuwa utawala wa familia uliisha zamani kayani pale Njaa Kaya alipotimka kwa aibu! Alisahau kuwa tangu rais Joni Kanywaji Makufuli aingie madarakani, hatujasikia Makufuli junior, NGO ya bi mkubwa wake wala kaka au mdogo wake akigombea ulaji chamani.
Kwa vile baadhi ya wake za mawaziri–japo si wote–wanapenda kubembea kwenye migongo ya walume wao, basi wake za mawaziri waitwe mawazira huku wake wa wabunge wakiitwa wabunga. Niliwahi kupendekeza mke wa rais aitwe raisa
pale bi Njaa Kaya alipoanza kupokelewa mikoani kama rais mwenyewe. Namshukuru subhanna Janet wetu siyo limbukeni na dandizi kama waliomtangulia ambao sasa wamedoda kama kiporo.
Kilichonifurahisha ni kitendo adhimu na cha haki cha Dk Kanywaji kumpandisha cheo afande aliyefuata sheria bila kujali ukubwa au ujinga wa mke wa waziri. Sijui kama mulume wa bi huyu limbukeni angeukwaa urahis angenyodoa vipi? Ama kweli God is not Mlevi! Thankful, hakupenya. Nashangaa kusikia eti rahis amemuonya mumewe. Alipaswa amtimue; ili naye aumie na kumpa talaka kidhabi huyu. Mbona watani zangu wanyalukolo huwa hawana ushamba na ushambenga kama huu au bi huyu anatoka milimani kwa wavijivuni? Kama unataka uwaziri si ugombee ubunge na rahis akuteue uwe waziri unyodoke. Ni ushamba, ulimbukeni na kujilisha pepo kiasi gani kutumia ile hali ya kushea bedroom na waziri kujiona–na kutaka, bila stahiki yoyote haya ya kibangi–utendewe kama waziri. Tafadhalini msilete mambo ya bedroom kwenye shughuli za umma. Nani alikuapisha wewe bi mkubwa mpenda sifa? Wakati mwingine mnatulazimisha kutumia maneno makali bila sababu. Yaani kila atakayelala na waziri naye anakuwa waziri siyo? Sijui ikitokea waziri akalala na changu nalo lijiite waziri siyo? Huyu dingi ambaye bi mkubwa wake amechemsha na kuboa namheshimu sana. Vinginevyo ningewashauri walevi na wavuta bangi wamuandamanie hadi atumbuliwe.
Kwa vile namfahamu mume wa mama huyu mpenda sifa, nilishangaa hata alivyoweza kuishi ughaibuni ambako haki na sheria ni jambo la kufa na kupona. Ama kweli, baadhi ya viongozi wa wengi wa Kiswahili ni wagumu kujifunza! Mnaleta mambo ya kijima kwenye karne ya 21? Ebo, shame on you na kumbafuni wakumbafu na limbukeni nyie. Madhani uwaziri ni mali ya familia siyo? Gendaeka wengine michosho kweli kweli. Wanakwenda ughaibuni kizurura kila mwaka; lakini bado hawajifunzi kutenda kama watendavyo watasha huko ughaibuni. Mnatuletea ufalme hapa. Go to hell! Nendeni Ghuba ambao ushenzi kama huu ni sehemu ya utamaduni au vipi?
Nilishasema mara nyingi kuwa kaya yetu inaibiwa na hawa wanaojiita watawala. Siku zile nikisoma kule Ukanadani niligundua kuwa anayeendeshwa kayani mle ni waziri mkuu peke yake ambaye ni kama rais wa kaya ile. Waliobaki wote wanaendesha ndinga zao wenyewe. Sasa nashangaa kusikia eti na mke wa waziri, vitegemezi vyake, baba yake, mama yake, hata mashoga wa bi mkubwa wake wana madereva na anayelipa ni mlipa kodi mlevi!
Uibiaji walevi haushii hapa. Kila waziri ana mlinzi, mtunza bustani, mpishi na makandokando mengine. Toka hapo shuka kwa wakuu wa wizara, manaibu waziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na walaji wengine ambao nao wana madereva wao na makandokando mengine kiasi cha kuwalewesha hata wake na ndugu zao kudhani nao ni mawaziri. Ama kweli wahenga walisema kuwa mbwa wa mfalme naye ni mfalme wa mbwa wote. Je namna hii tutafika? Nauliza kwa ulevi na mibangi yangu. Hata hivyo, mimi kuwa rahis wa walevi, huwa siruhusu bi mkubwa wangu kujipatia ujiko kwa kutumia cheo changu. Wanaofanya hivyo nao ni majipu lazima dokta Kanywaji awatumbue badala ya kuwaonya. Hivi huyu afande angemuonea mke wa waziri angeonywa au kuonyeshwa mlango? Huko siendi sana leo.
Nimalizie kwa kuwaonya wote wenye mtindio wa ubongo na ulimbukeni kutaka kutumia nyadhifa za walume au ndugu zao wakome na kukomaa. Vinginevyo nitawachomea kwa Dk Kanywaji–ambaye mar azote huwa anasikiliza kuliko hata Makondakonda–awatumbue kabla ya walevi hawajawatokea na michupa ya mupipi na vipisi vya bange.
Chanzo: Nipashe.
No comments:
Post a Comment