Tangu kuondoka kwa serikali ya awamu ya kwanza chini ya baba wa taifa Marehemu Mwl Julius Nyerere, Tanzania ilikoma kuwa nchi inayofuata maadili ya utumishi wa umma. Badala yake iligeuka nchi ya madili ambapo kila mwenye cheo aliitumia ofisi yake kujinufaisha huku taifa likitopea kwenye umaskini wa kunuka. Iko wapi Air Tanzania, NBC, na mashirika mengine mengi yaliyokuwa lulu ya taifa?
Siwezi kusema ni laana japo yawekezekana. Pale marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere aliposema kuwa patakatifu pa patakatifu hapapaswi kugeuzwa pango la wezi, sijui kama wahusika walimwelewa. Kwani, badala ya kufuata alichowaeleza, walifanya kinyume hadi tunajikuta hapa tulipo.
Chini ya utawala wa awamu ya kwanza, ikulu ilikuwa patakatifu pa patakatifu na waliokaa mle walikaa kitakatifu na si kijambazi wala kifanyabiashara kama ilivyotokea. Kwa vile nchi huendeshwa kutoka Ikulu, ugonjwa wa ulafi, ufisadi, ubinafsi, upogo na uzembe ulipopiga hodi ikulu, watanzania walipoteza matumaini na kujikuta wakishikwa mateka na kikundi kidogo cha wezi.
Kabla ya kuaga dunia, Mwl Nyerere alisema wazi kuwa ikulu ilikuwa imegeuka pango la wezi na kukoma kuwa patakatifu pa patakatifu hasa wafanyabiashara–tena wenye kutia kila shaka–walipoanza kuigeuza kijiwe chao cha kusukia mipango ya kuliibia taifa. Mwalimu alihoji: Ikulu kuna biashara gani, mbona nimekaa pale kwa muda mrefu na sikuona biashara yoyote?
Tukirejea historia, hakuna ubishi kuwa Tanzania ilianza kushambuliwa na mdudu wa rushwa pindi tu Mwalimu alipoondoka madarakani. Kwani, baada ya kuondoka tu ukaanzishwa utaratibu wa hovyo uliopewa jina zuri ruksa. Kwa mara ya kwanza tulianza kuona wafanyabiashara wenye kutia shaka wakiigeuza ikulu kijiwe chao kabla ya kuigeuza pango la wezi hadi Mwalimu akaamua kung’aka. Wengine walikunywa mle hadi wakalewa wakafikia hata kumwita mke wa rais ambaye alikuwa umri sawa na mama zao shemeji.
Baada ya kuondoka kwa utawala ulioruhusu kila upuuzi, ukaja utawala wa uzauza ambao nao uliuza kila kitu bila wakubwa zake kujisahau. Rejea kutwaliwa kwa Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira na ufanyaji biashara nyingine kama kuanzisha utaratibu mke wa rais kuwa na kampuni yake binafsi aliyoipachika jina zuri la Taasisi Isiyo ya Kiserikali (TIK) au Non-Governmental Organisation (NGO) kwa kimombo. Ghafla tulianza kuona mama nambari wani wafanyabiashara chini ya kivuli cha kuwasaidia akina mama kana kwamba wizara husika haikuwapo wala kutosha.
Baada ya kuondoka utawala uzauza ukaji utawala wa mdundiko ambapo kila mwenye kujihisi kucheza anaweza kucheza kwa staili apendayo. Badala ya wakubwa kuhimili na kuendesha nchi, walipoteza muda mwingi kwenye uzururaji huku wakifanya mambo ya ajabu. Ghafla tukasikia tuhuma kuwa utawala huu uliingia kwa fedha za wizi za EPA tuhuma ambazo hadi wahusika wanaondoka madarakani hawakuzijibu wala kutaka hata kuzikanusha au kukiri.
Mungu si Athumani. Umeingia utawala wa Hapa Kazi Tu kazi yenyewe ikiwa ni kutumbua majipu na kuirejesha Tanzania kwenye mstari. Wengi wameupokea kwa imani na upendo mkubwa. Ndiyo maana tunautaka urejeshe maadili ya utumishi wa umma ili uchukue nafasi ya madili ya kuuibia umma.
Katika kufanikisha hili, tunamshauri rais Magufuli afanye yafuatayo:
Mosi, arejeshe miiko ya utumishi wa umma kama ilivyokuwa awali ili kuoindoa nchi kwenye mikono ya majambazi na wezi.
Pili, afumue mifumo ya kale na kujenga mifumo mipya ya uendeshaji nchi, mfano, wananchi wote waeleze utajiri wao na namna walivyoupata kwa mujibu wa sheria na si utashi. Wale ambao wana utajiri usio na maelezo ya kina wawekwe ndani na utajiri wao utaifishe huku sheria ikiipa mamlaka serikali kushuku na kukamata yeyote aliyelala maskini na kuamka tajiri ili kuondoa motisha wa kuibia umma kama ilivyo sasa.
Tatu, kila mwananchi awe ana kitambulisho cha uraia kisichoghushika na anwani ya kudumu. Ikiwezekana majina ya watanzania wote na wageni wanaoishi kihalali yaingizwe kwenye kompyuta kama wanavyofanya nchi zilizoendelea.
Nne, zitungwe na kusimamiwa sheria za kupambana na uovu mfano, mtu asiyeishi kihalali nchini asipwe huduma ya aina yoyote hasa makazi, na nyingine zinazomwezesha kupata unafuu na mwanya wa kuishi nchini kinyume cha sheria.
Tano, kuwepo na tabia ya kuripotiana na wananchi wasipofanya hivyo wachukuliwe hatua. Mtu anapoona kosa linatendeka lazima aripoti polisi.
Sita, taasisi zote zilizoshindwa kulinda usalama wa mali za umma kama vile jeshi la polisi lifumliwe na kuundwa upya huku kukiwa na taasisi za siri za kuzichunguza sambamba na taasisi na idara nyingine ili kubaini ufisadi hasa rushwa na kujilimbikizia mali. Hata hivyo, kama tutarejesha maadili na kuwa na sheria za kila mtu kutaja mali zake, motisha wa kujilimbikizia mali kwa namna yoyote utakuwa umekufa.
Mwisho, Tunaweza kwenda hata nyuma na kuwabana hawa matajiri tunaowatilisha shaka kwa sasa kueleza walivyopata au kuchuma mali zao.
Chanzo: Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment