Baada ya Mkaguzi na Mdhibiti wa njuluku za lisirikali kutoa taarifa yake ya kuudhi, kusikitisha na kustusha, Kijiwe kimekaa kama kamati kuu ya kuendesha kaya kuijadili na kutoa onyo kuwa tunaweza kuchenchiana kama wezi waliosababisha madudu yaliyomo kwenye ripoti wataendelea kuendekezwa na kukingia kifua.
Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa njuluku za lisirikali aka CAG imetukera sana kama wahanga wa ujambazi wa kutisha uliokuwa ukiendelea kwa miongo kama mitatu hivi kabla ya kuchomoka Dk Joni Kanywaji Makufuli. Huwezi kuamini kuwa kaya apeche alolo iliweza kutoa misamaha ya kodi ya takriban trilioni nane. Hii siyo njuluku ya kahawa hasa kwa kaya kapuku na bingwa wa kubomu kama yetu.
Msomi Mkatatamaa ndiye anayelianzisha, “Waheshimiwa, sijui mmesoma hii ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa njuluku za lisirikali?” anaweka kabrasha lake mezani huku akijifuta jasho tokana na kupashwa joto na kahawa na kuendelea, “Wenzenu sijui kama leo nitakula wala kulala. Inakuwaje kaya yetu ifanyiwe kitu mbaya hivi tena kwa miaka mitano?”
Anakohoa na kuendelea, “Nitawapa ripoti nzima kwa sentensi moja kuwa kwa miaka mitano iliyopita, kaya yetu imepoteza zaidi ya shilingi trilioni nane tokana na kuwapa magabacholi na wachukuaji misamaha ya kodi wakati wachovu wetu wakiendelea kusota na kupukutika kwa magonjwa yanayotibika.”
Mgosi Machungi anatikisa kichwa na kuronga, “Hii ni hatai kusema ule ukwei. Ina maana rahisi aikuwa wapi na aikua akifanya nini na akiipwa mshahaa na kwa faida ya nani?”
Mbwamwitu aliyekuwa akifunua makabrasha anamchomekea mgosi Machungi, “Kila nikisema kuwa kaya hii inaliwa watu wanadhani nawatukana. Huyu kilaza aliyeruhusu madudu haya anapaswa kuchomwa moto kama kibaka au vipi?”
Kapende anadandia mic, “Utadhani Mbwamwitu umesoma mawazo yangu. Kama ingekuwa siyo kaya ya wehu na waoga, hawa jamaa walipaswa kula shaba au kukamatwa na kufanyiwa kitu mbaya wao na wenzao waliotufanyia kitu mbaya hii.”
Mijjinga anaamua kula mic, “Sasa naamini madai ya mze Mpayukaji kuwa kaya ilikuwa ikitawaliwa na mataahira ambao tuliwachagua bila kujua kumbe walikuwa na ugonjwa wa akili. Hivi inawezekanaje utoe misamaha ya matrilioni kama haya halafu ukeshi kiguu na njia kwenda kuomba usiwe chizi hata bwege jamani? Hawa lazima watakuwa mtihani unaomnyima usingizi Daktari mwenzetu Kanywaji kusema ule ukweli.”
Msomi anaamua kurejea, “Kwa taarifa yenu hii njuluku si ya kawaida. Ukitaka kujua ukubwa na thamani yake, iweke kwenye matumizi. Kwa utaalamu wangu –haraka haraka –naweza kusema kuwa njuluku hii kama ingetumika humu kayani, ingeweza kupunguza umaskini kwa aslimia zaidi ya 20. Si hilo tu, njuluku hii inaweza kusomesha watoto wa kaya hii kwa miaka zaidi ya 50 au kujenga barabara ya kutoka Dar hadi Mwanza. Si mlisikia Dokta Kanywaji akisema kuwa ana mpango wa kununua ndege tatu aina ya Airbus? Kwa njuluku hii unaweza kununua ndege zaidi ya mia na kufanya shirika la ndege la Bongolalaland kuwa kubwa kuliko yote barani. Kama ukiamua kujenga mashule ndiyo usiseme, unaweza kujenga shule za sekondari si chini ya 300.”
Mheshimiwa Bwege anaamua kutia guu huku akisonya na kutukana matusi ambayo hatutaki kuyarudia hapa, “Nakubaliana na Msomi mia kwa mia kuwa kumbe tulitawaliwa na wagonjwa wa akili ambao hawakupaswa kuwa ikulu bali Milembe wakiuguza vichaa vyao. Ukiuliza hii njuluku yote imefanya kazi gani wala usiende mbali. Mnadhani mkiona majiji kama London, Dubai, Paris, Panama City na mengine yanapendeza ni kwa sababu gani zaidi ya fedha inayofichwa na wezi wenu wapumbavu? Mijizi mingi inatoka kwenye majimbo maskini lakini bado inaficha fedha Jersey. Hii akili au matope?”
Mpemba naye hajivungi, “Yakhe hakika wankata sana hapa. Maana kama hii njuluku ingetumika Visiwani, basi Pemba na Zanzibar vingetokezea kuwa kama Hong Kong wallahi. Hapa lazima tukazane hadi hawa walotenda huu uovu wanyongwe kama siyo kuchomwa moto kama vibaaka. Maana hawa ni hatari kuliko hata hao vibaka tuniowachoma moto.”
Kanji naye anaamua kumchomekea Mpemba, “Pemba acha mimi chomeka veve dugu yangu. Hii juluku kuba kuweli kweli. Lakini mimi hapana unga kono choma vatu kama wibaka. Napaswa heshimu haki ya binadamu dugu yangu.”
Da Sofia Lion aka Kanungaembe hakubaliani na Kanji. Anaamua kumpinga wazi wazi, “Kaka Kanji sikubaliani nawe. Waachwe waendelee kutukoga wakati twaumia tokana na ujinga na upumbavu wao? Hawa lazima wachomwe moto. Angalia ndugu zetu wa mabondeni wanavyoishi kwa mateso wakati njuluku yao ikitolewa sadaka kwa majambazi wa ndani nan je. Hii haikubaliki; na namshauri dokta Kanywaji chonde chonde ahakikishe anaweka gendaeka hawa lupanga vinginevyo hataeleweka.”
Mipawa aliyekuwa akisoma makabrasha anamua kutia timu, “Bengh’we hawa ni wa kitanzi tutake tusitake. Tukiwaoneaga huruma basi wafunge maisha ili wasiendelee kufaidi njuluku zetu. Naungana na da Sofi; huu kweli ni mtihani mzito kwa dokta Kanywaji. Ama kweli ukishangaa ya Nkapa utaona ya Kikwekwe!”
Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shumbwengu la toto Riz! Acha tulitoe mkuku ili kumkamata na kumfanyia kitu mbaya!
Chanzo: Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment