Wiki juzi nilipoandika waraka wa kufurahia kutangaza vifo vya mafisadi kuna mafisadi au makuwadi wao kama kumi na ushei hivi waliniandikia emails za matusi; wasijue nshatukanwa matusi aina zote; na huwa sijali. Matusi ni maneno tu. Hayawezi kuvunja mfupa; tena fupa lenyewe la mlevi aliyezoea kila aina ya sulubu kwenye kaya ya sulubu. Hivyo, kunitukana ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa. Watukane wasitukane, nitaendelea kusherehekea pale mafwisadi yanapopukitika iwe ni kwa presha au ngoma kama siyo mkono wa bwana God. Hata hivyo, sikuwaacha wanahizaya hawa ambao wazazi wao walipata hasara kuzaa mijizi. Niliwaporomoshea mvua na vimbunga vya mitusi tena ya nguoni hadi wakanywea. Sipokea emails nyingine za kishenzi na kichovu kama hizo tena. Walidhani wanaweza kunitisha fyatu kama mimi wasijue nilishajifia nikingoja kuzikwa hasa usawa huu ambapo mijizi michache inahaha baada ya rais Daktari Joni Kanywaji Makufuli kutema moto si cheche kama tulivyomzoea. Aliwapa laivu walanguzi na mafisadi wanaoficha sukari ili iadimike walangue huku serikali ikichukiwa. Nilikuwapo pale Katesh alipofyatua kombora lake kuwa wote walioficha shuga wajiandae kunyang’anywa na kugawiwa walevi. Mifisadi hii uchwara imezoea vijiserikali ilivyokuwa imeweka mifukoni isijue Makufuli ni mtambo mwingine. Sasa mtakoma na kukomaa kama siyo kunyea debe kumbafuni zenu mafwisadi wote kayani na wale wote waliowaendekeza na kuwaabudia wasijue yana mwisho. Yako wapi sasa kumbafuni zenu?
Leo naandika waraka mwingine adhimu na muhimu tena kwa mtu muhimu–ambao kwa wasiojihangaisha kuangalia mambo kama yalivyo–watadhani namuwangia rahis wetu mpendeka anayelenga kuwakomboa walevi na wachovu wote kayani. Kwanza, hata Dk Kanywaji anajua kuwa mimi ni mtu wake tena ninayempa ushauri ambao anaufanyia kazi tena haraka. Mara hii mmesahau nilimtumbulisha Ombni Sifui? Si alijidanganya akidhani hawezi kutumbuliwa akaishia kutumbuliwa tena kavu kavu bila kutarajia. Yuko wapi sasa? Unafanya mchezo na mimi siyo usijue ulevi wangu si wa hasara bali busara na faida. Anayedhani najifagilia, ajiulize kama anaweza kuyachora haya ninayoyachora hadi Dk Kanywaji akayapenda na kuyashabikia. Au mnataka anitwangie simu au kuniandikia email. Na bado nina mpango wa kuwatumbulisha akina IPTL, UDA, na manyang’au wengine ukiachia mbali wale waliokuwa wakiwakingia kifua. Hata mzee wa Kiwira nitambulisha atake asitake. Hivyo basi, naandika bila woga wala kupinda maneno kumtaka achukue tahadhari na wanahizaya hawa wasijemfanyia kitu mbaya hasa baada ya kuwashika pabaya.
Pamoja na ulevi wangu, bado naikumbuka kuisoma vizuri historia. Nakumbuka mashujaa waliofanyiwa kitu mbaya kama vile rafiki yangu kipenzi rais Thomas Sankara wa Burkinabe na waziri mkuu wa zamani Edward Moringe Sokoine waliokatizwa maisha yao baada ya kukamia kuwakomboa wanyonge hasa walevi toka kwenye mikono michafu ya mafisadi wa kitaifa na kimataifa.
Leo–tena bila kupiga mma wala kuvuta bangi–nakuja na wosia muhimu kuliko zote na kwa mtu muhimu sana kwa kaya yetu. Napendekeza afanye yafuatayo:
Mosi, anapogundua jipu, atumbue waliotumbuliwa watatoa sauti wenyewe. Asitoe tishio au onyo ambavyo vinaweza kutumiwa na mashetani hawa kumhujumu kwa namna yoyote. Simba mwendapole na mkimya ndiye hula nyama. Hapa la kufanya si kuyatishia majambazi haya bali kuyapiga marufuku ikiwezekana kuyatupa lupango yakapate jambajamba ya kushea vyoo kule kama si kushikishwa ukuta. Asihau kuwa majipu mengine anatembea nayo ila hajayagundua. Kwenye msafara kenge mamba wamo.
Pili, kama sukari tajwa, alipaswa kuvamia maghala na kuinyakua na kuigawa kwa walevi badala ya kutangaza ili haya mafisadi yajue kaya hii ina wenyewe na wenyewe ni sisi na si yenyewe kama yalivyozoea.
Tatu, badala ya kuyazodoa na kuyaonya, ilibidi baada ya kukamata sukari na kuyatupa lupango, ayatwange faini wakati yakingoja kesi kamambe ya kuhujumu uchumi.
Nne, akumbuke historia ya mashujaa tajwa hapo juu. Nao walifanya kama yeye wasijue haya majitu hayana utu wala hayathamini uhai. Najua shujaa Sokoine alipodedishwa kwa kukamata mafisadi, Dk Kanywaji–kama mimi–alikuwa shule au jeshini. Hata hivyo, anajua chanzo na sababu ya kuSokoiniwa Sokoine. Najua anaweza kusema yule alikuwa waziri mkuu tu wakati Kanywaji ni rais. Mchezo ni ule ule–angalia na tahadhari waliokuzunguka–ili uchukue tahadhari. Sisi walevi tulishazoea. Ukiona mlevi wako wa karibu anajifanya kukujali na kukupenda jua anamnyemelea bi mkubwa wako ili apate majamboz.
Adui mwingine mkubwa anayemnyemelea Dk Kanywaji si mwingine bali genge lake. Limejaa mijitu yenye roho mbaya na minyama inayoweza kunyotoa mja roho hata kwa kuikosoa. Just imagine; kama Horace Kolimba aliliambia genge lake kuwa limepoteza mwelekeo ikaamua kumKolimba, fikiria huyu anayetishia maslahi yao uchwara ukiachia mbali kutaka kufumua mfumo uliozooza na wa hovyo wa muda mrefu. Kama waliweza kumdedisha mtu kwa kuwakosoa, unadhani watamfanya nini anayetishia kuwatumbua wakubwa na wadogo katika genge hili? Hamuoni jamaa anavyogwaya kuachia ukiti akiogopa kutumbuliwa. Hata agomee vipi ataachia na kutumbuliwa atatumbuliwa tu. If he has any skeletons in the closet. Ni suala la muda.
Kwa walevi sisi bangi na kanywaji hatuna majipu wala mzee usijekututumbua shida zilishatutumbua.
Chanzo: Nipashe.
No comments:
Post a Comment