Hivi karibuni mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda aliwalisha viapo wakuu wa idara mkoani mwake kufichua wafanyakazi hewa. Huu ni utaratibu mpya ambao sijui unatoka kwenye katiba gani hasa ikizingatiwa kuwa kuna baadhi ya kada ya wafanyakazi isiyohitaji viapo inapoajiriwa. Je sheria za nchi zinasemaje kuhusiana na masuala kama haya? Je hivi viapo vina uzito na uhalali kisheria? Je walioviandaa wamezingatia sheria gani na mambo gani? Je viapo hivi vinaweza kuheshimika mahakamani kama waliovila watavivunja? Sijui kama kisheria viapo kama hivi–ambavyo bila shaka–havina mashiko kisheria vinaweza kutekelezwa mbele ya mahakama au kupata hadhi ya mkataba kisheria. Nasema hili ni jambo jema linalofanyika vibaya kutokana na kutokuwa na mizizi katika katiba yetu. Kulishana viapo kienyeji bila miiko inayoeleweka ya uongozi na utumishi wa umma ni kama kutapatapa. Hata huko makanisani wanapolishana viapo, huwa kuna kanuni na utaratibu vinavyoeleweka na kukubalika kisheria. Si hilo tu, kuna namna ya kisheria ya kutekeleza viapo hivyo na madhara yake vinapovunjwa kisheria. Rejesheni katiba mpya muepuka kusumbuka na kuhangaika jambo ambalo linaweza kutafsiriwa kama ombwe la sera jambo ambalo si jema kwa serikali iliyodhamiria kuleta mageuzi katika mfumo wa utawala wa taifa letu.
Wengi wanashangaa sana namna ambavyo baadhi ya watu wanaweza kufanya mambo. Japo huu unaweza kuonekana kama ubunifu, bila kuwa na utaratibu maalumu kisheria, ubunifu unaweza kuonekana kama vurugu na hata ubabaishaji. Inashangaza sana kufikia hatua hii hasa ikizingatiwa kuwa kulikuwa na fursa ya kurekebisha mambo na kuwa na utaratibu unaojulikana lakini watu wachache wakaifuja. Fursa hii ilijitokeza pale ilipoamriwa kukusanywa maoni kwa ajili ya kuandika katiba mpya ambayo watawala woga na wasio na udhu waliyapuuza na kuizika katiba ikiwa hai huku wakiwa wameitia nchi hasara ya fedha na muda. Ni ajabu sana kuona hawa wanaowaapisha wenzao ndiyo wanaosifika kuua katiba mpya ambayo bila shaka ingeondoa huu uoza kirahisi. Nchi haiwezi kuendeshwa kwa mipango na mawazo binafsi ya rais ua wasaidizi wake bali kanuni na sheria vinavyoeleweka na kukubalika kwa wananchi wote. Leo Makonda anawalisha wakuu wa idara wa Dar es Salaam kwa kiapo fulani. Kesho atakuja mwingine na aina yake ya kiapo. Je hii haijawa vurugu na usumbufu kwa umma usio na mabavu ya kupinga wala kuzuia vurugu hii? Tunajua hawa wanaolishwa viapo hawawezi kufurukuta tokana na woga uliolikumba taifa hasa kutokana na wafanyakazi wengi kuzoea kufanya kazi kwa mazoea na kuvurunda kiasi cha kutoa nafasi ya mambo kama haya ya hovyo kufanyika.
Ni jambo la hovyo na hatari kumwachia kila mkuu kwenye nafasi yake kujiundia utaratibu wa kuleta uwajibikaji. Kufanya hivyo–zaidi ya kuonyesha ombwe–ni vurugu na fursa ambayo inaweza kutumika vibaya. Lazima katika uongozi wa taifa, kuwe na vigezo na kanuni zinazofanana. Leo mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam anajiundia kiapo chake. Kesho mkuu wa mkoa mwingine atafanya hivyo. Mwisho wa siku, tutakuwa na wafanyakazi wenye nyadhifa zinazofanana lakini waliolishwa viapo tofauti. Ni vizuri tukafahamu na kukubali si watendaji wote wana ujuzi wa mambo ya kisheria wala si wote wanaoweza kuwa na utashi wa kuheshimu haki za wenzao hasa wakati huu ambapo kila mkubwa anajitahidi kumridhisha rais na si wananchi.
Kwa wanaomfahamu mtu kama Makonda ambaye anasifika kwa kutenda kwa mabavu, watakubaliana nasi kuwa kama viapo vyake vitakiukwa–jambo ambalo ni la kawaida kwa binadamu–uwezekano wa kutoa huku zisizolingana na makosa ni mkubwa hasa ikizingatiwa kuwa viapo vya namna hii havina nguvu na uhalali kisheria. Kwa lugha nyepesi ni kwamba ombwe la kanuni na sera linaanza kuzaa vurugu bila sababu. Hivyo tunamtaka rais afanye yafuatayo:
Mosi, akemee ujitwaliaji huu wa madaraka ambao unaweza kufanyika kwa kisingizio cha kuteleza amri zake. Pia hii inaweza kuonyesha kuchanganyikiwa kwa wahusika kiasi cha kufanya mambo kwa mazoea au hisia badala ya sheria.
Pili, kuondokana na kadhia hii, rais anapaswa kuanzisha utaratibu wa kurejea kwenye katiba mpya akianzia pale tulipoishia baada ya katiba husika kuuawa kifisadi na kiwoga.
Tatu, rais atangaze utaratibu utakaofuatwa na muda utakaotumika kuipata katiba mpya ili kuepuka kupoteza fedha na muda zaidi kwenye jambo ambalo lilishakamilika.
Nne, rais atangaze wazi wazi kuwa utumishi wa umma hufuata sheria zilizowekwa na hivyo uzingatiwe; na kama zinapwaya zirekebishwe ili kuepusha vurugu hii ya kimfumo. Haiwezekani mtu akaamka na kujichukulia uamuzi wa kufanya vitu vinavyofunja sheria akaachwa hata kama nia yake ni nzuri. Huwezi kutekeleza jambo zuri kwa njia mbaya bado likaendelea kuwa baya wala kufanya jambo baya kwa nia nzuri likawa jema.
Tumalizie kwa kusisitiza kuwa serikali ianzishe utaratibu kwa watendaji wake kufanya mambo ndani ya sheria tena kwa sare kwa taifa zima badala ya kila mtu kujifanyia atakavyo. Kwani kufanya hivyo ni vurugu tupu. Nani anataka kuishi chini ya mfumo wa jazba, vurugu na ombwe?
Chanzo: Mwanahalisi.
No comments:
Post a Comment