How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Thursday, 26 May 2016

Kijiwe chamuaga Kitwanga

            Baada ya rais Dokta Joni Kalaji Makufuli kumpiga kalamu mlevi mmoja aliyekuwa amefanikiwa kujichomeka kwenye safu yake, Kijiwe hakikumuacha aende hivi hivi bila angalau kumzomea japo kiduchu tu. Japo Mipawa huwa si muanzishaji wa inshu, leo ndiye anaingiza mada hii tena akisikitika ikizingatiwa kuwa mzee huyu wa kutwanga ulabu ni mwishiwa wa jimbo lake huko makwao.
            Mipawa analianzisha, “Wazee mmeona jinsi huyu muishiwa wa jimbo langu Chaz Kitawangaji kanywaji alivyonitutia aibu? Natamani nimkamatage na kumraba vichwa kama siyo bakora. Nadhani saa hizi waliomnyima kura mheshimiwa Mijjinga na kumpatia yeye wanajilaumu. ”
            Mijjinga anamnyang’anya Mipawa mic, “Pole sana ndugu yangu.Tuache utani. Tangu ilipofumka kashfa ya Ligumi, Kitwangwa Kanywaji alikuwa amekalia kutika kavu hasa ikizingatiwa kuwa kama muathirika anayengojea saa na sekunde za kufungashiwa virago.” Anapiga chafya na kuendelea, “Uzuri ni Kwamba, sasa Kitwanga ameamua kujitwanga mwenyewe tena kitoto na kijinga hivi. Sijui huyu jamaa amesomea nini na wapi kiasi cha kujisahau kiasi hiki?”
            Mbwamwitu anamchomekea,”Nasikia ni mtaalamu wa makompyuta usipime. Si ndiyo maana alianzisha Infyosys na kuwaajili akina Ligumi huku yeye akijificha nyuma ya pazia huku akiwasukumia tenda.”
            Mgosi Machungi anakamua mic huku akitabasamu, “Huyu hata kama amesomea makompyuta aishindwa kutumia akii. Hapa nazani aitumia akii ya ooboti siyo ya binadamu. Tutajuaje kama hakufoji kama iivyozoeeka kwa vigogo? Aizani kuwa bado kaya hii iko mikononi mwa muevi asijue Dk Kanywaji achiia mbali kunywa, haonji. Sasa ataijua dunia. Sijui atawambia nini wae waiomkopesha kua zao akaishia kuwadhaiisha kwa kupiga mma.”
            Msomi Mkatatamaa anaamua kutia guu, “Hapa lazima tu mpongeze dokta Kanywaji kwa kumtwanga huyu mtwangaji wa kanywaji ili aendeke akalewe vizuri huku akiwaachia wenye uwezo wa kupiga mzigo wapige mzigo kwenda mbele. Kimsingi, bado tuna walevi wengi kwenye ofisi za umma. Maana ukiangalia hata hawa wanaoficha sukari bila shaka ni walevi wa utajiri ambao mwisho wao unaweza kuwa mbaya kwao kwa wanavyohujumu kaya. Hata hawa wanaogeuza bunge kuwa uwanja wa mipasho wamelewa u-mwenzetu wa Chama Cha Mafisadi (CCM) nao wanapaswa kutumbuliwa tu.”
            Mheshimiwa Bwege anakula mic, “Nakuunga mkono mheshimiwa Msomi. Kimsingi, kaya hii ilipokuwa chini ya utawala wa kilevi, kila mlevi alijiona mjanja asijue siku zao zilikuwa kikiheshabika.Je wangapi watafuata? Unaingia kwenye mjengo mtukufu kitukutu halafu unategemea upone siyo? Mie nadhani hata wanaoleta bejeti feki zenye kutaka fedha kwa mambo ambayo yalishangetengewa fedha ni majipu na wanapaswa kutumbuliwa kwani wanatuibia kila mwaka.”
            Kanji anakamata mic, “Hata mimi hapana penda ile pasho napasa kwa bungeni na hishiwa. Kama nakwenda kwa mjengoni napaswa veve fanya kazi ya vananchi nakopesa veve kula siyo kufanya pasho.”
             Kapende anatia guu, “Nasikia jamaa alikuwa amekunya pombe aina ya Lingumi ambayo siku hizi inawasumbua waishiwa wengi Njengoni. Hata hivyo, mie nampongeza Kitwanga–kwa kuutwanga kabla hajatwangwa–kwa kujionesha alivo wa hovyo ili wale walonchagua waandae ntu mwingine wa kuwawakilisha ili huyu apate fursa ya kwendalewa atakavo. Sijui akina Jan Makambale walioguswa na kashfa ya kutumia dada zao kula njuluku za watasha wanangoja nini?”
            Sofia Lion aka Kanungaembe anakula mic, “Huyu Dokta Kanywaji kwanini anapendelea. Sijui kwanini hamtumbui Meeki Sidi Sadiq ambaye swahiba yake Kabwela alirejesha namba hivi majuzi. Sijui anangoja nini baada ya kufumka kashfa ya Kituo cha Mangwala ngwala ya mikoani pale Ubungo?”
            Msomi anarejea, “Acha Kitwanga aende akautwange mma ili uchaguzi ujao wapika kula yake wamuulize ni kwanini alithamini ulabu kuliko wao waliokuwa wamempa ulaji.Natamani Dk Kanywaji aende kinyume nyume na kuwatumbua majipu kama Prof J’4 Majembe walioua ilm yetu chini ya Njaa Kali Kikwekwe.”
            Kabla ya kuendelea Mpemba anakula mic tena, “Yakhe kuna jamaa moja alintonya kuwa huyu Kitwanga aliupiga chakari na kuondoka kwenye baa na kwenda kwenye nyumba ndogo kutwanga asijue naye atatwangwa! Maskini ulaji wa dezo sasa umtoka huku akiregea benchi. Wallahi ingekuwa miye, ningejiuzulu hata uhishimiwa kwa vile mimi ni muishiwa.”
            Mzee Maneno anakula mic, “Nashangaa ni kwanini hata yule waziri ambaye bi mkubwa wake alimtolea nyodo afande kwanini hakufutwa kazi ili akampe twalaka vizuri baada ya kumsababishia kutemwa kwenye ulaji. Kuna kazi kweli kweli. Mmeona pale uwanja wa ndege jinsi wanaizaya walivyokuwa wakimdanganya rahis kuhusiana na kuharibika kwa mitambo ya kukagulia mizigo. Sijui kwanini hajawatumbua!”
            Mijjinga anaamua kutia guu tena,”Usinikumbushe huu upuuzi wa juzi pale Uwanja wa Ndege wa Mzee Mchonga. Nilikuwapo pale. Kwa macho yangu nilishuhudia mijitu mizima ikongopa utadhani inamuongopea mtoto. Kuna wauza unga ninaowajua ambao hupitisha bwibwi pale kama bangi toka bara na kusambaza hapa bongo kabla ya kuexport nje. Ama kweli cha mlevi huliwa na mgema!”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si akapita Kitwanga akiwa ameutwanga! Acha tumpe kampani kwa kumzomea kabla ya kuanguka mtaroni. Sijui kama alinusurika bila kufanyiwa kitu mbaya kwa kuangusha gari vile!
 Chanzo: Tanzania Daima.

No comments: