How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Sunday, 1 January 2017

Magufuli alicherewa kutumbua

Mkurugenzi wa Tanesco naye aachie ngazi

             Vyombo ya habari hivi karibuni vilimkariri Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO), Felchesmi Mramba akijisifu kuwa wamewawajibisha baadhi ya maafisa wa Tanesco tokana na kushiriki vitendo vya wizi na uhujumu wa shirika na taifa. Alikaririwa akisema, “Tumechukua uamuzi mgumu wa kuwafukuza maofisa wetu kutokana na kujihusisha na vitendo mbalimbali.” Kwanza, vitendo mbali mbali maana yake ni nini zaidi ya kuendelea kutumia lugha za kulindana? Pia kusema eti ni uamuzi mgumu ina maana wahusika walilazimika kuchukua hatua walizochukua ima kwa hofu ya rais Magufuli au kutaka kumfunga Kamba awaone wanawajibika wasijue  hawawezi kunusurika hasa watakapoulizwa ni kwanini sasa ni si siku za nyuma.
            Pili, huyo mkurugenzi na wenzake waliowafukuza wahusika walikuwa wapi hadi rais John Magufuli aanze kuwasaka wazembe na wezi wa mali za umma? Kama tunakuwa wa kweli–aliyepaswa kuachia ngazi kwanza kutokana kutofanya kazi yake vizuri–si mwingine ni Mramba mwenyewe ambaye tangu ashike usukani hakuna kilichobadili zaidi ya Tanesco kuzidi kuzama.
            Hivyo, kama Mramba na wenzake wanaamini wametenda haki, wanajidanganya. Wameonea wa chini yao ili waoenekane wanachapa kazi. Swali ambalo wahusika hawa hawawezi kujibu ni kwanini sasa na si miaka ya nyuma? Wanachofanya ni sawa na uhuni wa mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paulo Makonda aliyetaarifiwa kuwaonea maafisa wa chini yake kwa kuwaweka ndani masaa sita akijitahidi kumridhisha rais wakati hafai kabisa.
            Mramba aliongeza, “huu ni mwanzo tu tumedhamiria kupambana na wafanyakazi wasiokuwa waadilifu ndani ya shirika.” Je hao walioazimia kupambana na wafanyakazi wasio waaminifu wao ni waaminifu? Je walikuwa wapi siku zote? Anachomaanisha Mramba ni kwamba walikuwa wakiwavumilia watendaji waovu kutokana na kufanana nao.  Je wafanyakazi wameanza kutokuwa waaminifu baada ya kuingia Magufuli au wamekuwapo wakijibia watakavyo kila mtu kwa nafasi yake kiasi cha kustuliwa na kasi ya Magufuli?   Mramba alisema kuwa maofisa saba wamefukuzwa kazi katika mikoa ya Dodoma (Kondoa Kaskazini), Kagera, Shinyanga, Katavi na Mkoa wa Tanesco wa Ilala. Hata hivyo Mramba hakueleza vigezo na utaratibu vilivyotumika kuwafukuza wahusika. Wengi wanajiuliza. Kwanini sasa na wametumia vigezo gani kama lao halikuwa moja? 
            Tungeshauri wakubwa waache kukurupuka kwa kutaka kwenda na kasi ya rais. Wanaweza kujikuta wakitimua watu ambao watakwenda mahakamani na kurejeshwa kazini na kulisababisha taifa hasara. Kama kuna jambo ambalo wakubwa wa Tanesco wangefanya si jingine kujiwajibisha wao kwanza bila kungoja yawakute yaliyowakuta wakuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bandari na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Kwa wanaokumbuka kisa cha kuchekesha ni pale ambapo mkurugenzi wa zamani wa TRA aliyesimamishwa kazi Rished Bade kujifanya hakuwa akihusika na hujuma ya kutokusanya kodi kwa kuridhia wa chini yake wawajibike ili anusurike asijue angefuata. Nitashangaa rais Magufuli kama hatamfukuza Mramba hasa ikizingatiwa kuwa Tanesco imekuwa ikifanya madudu kiasi cha kutumiwa na hata na mafisadi na matapeli wa kimataifa kama IPTL kuliibia taifa. Rejea ujambazi wa Escrow ambao nao unamngoja Magufuli.
            Kimsingi, wapo akina Mramba wengi. Chukulia mfano mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Taifa letu sasa linasifika kwa kupitisha unga hadi mwingine unakamatiwa nje ya nchi tena kwenye mabegi. Je mtu kama huyu na watendaji wake wanangoja nini? Ukienda mipakani ndiyo usiseme. Uhamiaji pale ni uoza mtupu ambapo pasi zetu zinauzwa mchana kweupe kwa wageni kiasi cha kutumika kusafirishia na kutendea jinai nyingine.  Somo tunalopata toka kwa Mramba ni kwamba taifa lilikuwa limeoza na halikuwa na serikali zaidi ya nchi kujiendesha kama ndege iliyoko kwenye Autopilot.
            Kama rais Magufuli anataka kufasaisha taifa na kukuza uchumi aanze na Tanesco. Maana bila kuwa na umeme wa uhakika kutokana na uongozi ambao umekuwa ukiachiwa kuhujumu shirika kiasi cha kusababisha mgao na ulanguzi wa umeme visivyo na sababu.  Leo Mramba anaongelea watumisha saba wakati nchi imejaa vishoka karibu kila mji na wakuu wa Tanesco kwa kuogopa kukosa maslahi yatokanayo na jinai ya kuibia shirika wanasuasua kutumia mfumo wa kompyuta wa kusambaza umeme ambao una uwezo wa kugundua umeme uliounganishwa kinyume cha sharia. Je ni viwanda vingapi tena vikubwa vimejiunganishia umeme au kuiba umeme na wakuu wa Tanesco hawa hawa wanaowatoa kafala wenzao hawavishughulikii?
            Tumalizie kwa kumtaka Mramba ajiwajibishe yeye kwanza badala ya kuwatoa kafara wenzake ili yeye anusurike. Maana swali kuu la kwanini aanze kuchukua hatua hizi baada ya rais Magufuli kuanza kufuatilia uoza linamtoa knockout. Turudie. Tutashangaa kama rais Magufuli hatamtimua kazi Mramba na kuvunja Bodi ya wakurugenzi ya Tanesco wakifuatiwa na sehemu nyingine ambazo tumezitaja kwa uchache.
Chanzo: Tanzania Daima, Desemba 20, 2015.

No comments: