How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 14 January 2017

Barua kwa mpendwa na munusurika Escrow

Image result for andrew chengeImage result for tibaijukaImage result for muhongoImage result for mkapaImage result for ali hassan mwinyiImage result for kikwete
             Mpendwa Escrow,
         Baada ya kukosa ofa na kanywaji na njuluku za kununulia bangi ka muda mrefu, nimekumbuka mpendwa wangu marehemu Escrow aliyetujaza minjuluku hadi tukasahau kuwa kuna siku kutakuwa na ukapa na ukata baada ya mchezo wa kupiga madili kuuawa na maadili ya Bwana nkubwa Joni Kanywaji wa kutia makufukuli ulaji wetu rahisi.Japo sikupata mgao wa njuluku uliotembezwa baada ya wewe kufanyika moja kwa moja, nilizoea kupata ofa kibao za kanywaji toka kwa wale waliofaidi mabilioni uliyotengeneza. Waingereza huita hii kitu “to trickle down” ambapo majambazi wakubwa kama waliokutengeneza kuwahonga wachovu kama sisi ili kuwa washiriki kwenye jinai ya kuhujumu kaya yao.
            Kwa vile sasa miaka inazidi kuyoyoma tangu wakubwa wapya waingie kwenye ulaji, wapo waliojidanganya na kuota mchana wakidhani kuwa angalau wangekufukua huko uliko ili ima njuluku za umma zirejeshwe kwake huku walevi kama sisi tukiendelea kukosa ofa zilizotufanya tuwe na furaha kana kwamba hakuna huzuni. Nilisikia wakosoaji wakitushauri tuache kuwa kama samaki ambao mara nyingi hunaswa kwa nyama ya wenzao kwenye chambo.  Kabla ya kusahau, siku hizi napenda kuwasiliana na kuwasilisha kwa njia ya barua tokana na kutunukiwa shahada ya juu ya udaktati katika barua yaani Doctor of Letters kwa kifupi Litt. D. hivyo, usishangae kwanini natumia sana barua badala ya makala. Nataka kuonyesha ugwiji wangu katika nyanja hii ya kisomi japo kilevi.
            Mpendwa Escrow, huwezi kuamini kuwa wanywanywa walihanikiza na kuchonga sana eti wale waliokuzaa washughulikiwe. Nakumbuka baba na mama yako Jimmy Rugemalayer na Gabacholi Sethii wa ukoo wa IptL. Walisakamwa wee hadi mkuu akasema hana hamu, nia wala uwezo wa kufukua makaburi ili yasijemuua kwa uoza na harafu. Sijui kama nawe ulikuwa mmojawapo; au ni wengine.
            Mpendwa Escrow, wanywanywa na wambea siku zote hawana adabu. Hivi walitaka mkuu atende makufuru ya kuwagusa wasiogusika? Walitaka aumbue wazee wazima tena wazee wenyewe walioridhia uzaliwe nao wapate chao? Mbona hawakutumia akili kushangaa kichanga kama wewe wakati kuna babu yako IptL? Walidhani haya mambo yalianza jana siyo? Mbona walinoa ile mbaya hasa ikizingatiwa kuwa chezo zima lilianza zama zile za ruxa ya kufanya kila mlevi afanyavyo mradi asimuumize mkuu? Mbona walisahau kuwa hata baada ya ruxa kufutika mambo yaliendelea kufanywa kwa uwazi na ukweli kabla ya kuwekwa mikononi mwa maisha bora kwa walevi wote ambapo nawe ulipewa uhai mpendwa? Je hapa utamkamata nani umuache nani?  Je hapa akina Rugemalayer na Sethii ndiyo wa kulaumiwa tu au genge zima la wanene? Sijui kwanini walevi hawapendi kusoma historia kuwa wakati babu yako IptL anazaliwa wakunga walikuwa wengi tu tena wakipokezana vijiti baada ya kila mmoja kumaliza ngwe yake? Huu ndiyo ukweli hata kama unakera na kuuma. Hii ndiyo historia. Huwa haiandikwi upya wala kufanyiwa uhariri vinginevyo iwe imeandikwa kwa upendeleo kama ile ya kikoloni.
            Mpendwa Escrow, hawa wanywanywa walipenda hata wachungaji wa kondoo wa Bwana waliojazwa minjuluku nao waumbuliwe? Sijui kama akina Father Kigumu aka Kilaini wengependa makaburi yafukuliwe ili nao waumbuke. Sijui kama akina profedheha Anae Kajuamlo wangefurahia ufukuaji wa makaburi. Sijui kama mzee wa Vijisenti angefurahishwa na ufukuaji huu ambao bila shaka ungemuacha uchi yeye na wenzake ingawa wako uchi siku zote.
            Mpendwa Escrow, hakuna nilipofurahi na kufarijika kama kuona ulivonusurika hivi juzi pale Shirika la kutoa mimeme lilipotaka kulangua huduma hii. Kwa vile hii haikuwa halali, mkuu aliamua kuwatumbua wanene wa shirika huku akikuacha wewe utanue. Najua hapa wanywanywa watakuwa walichukia sana. Niliwasikia wakisema kuwa hawa jamaa walitolewa kafala. Nilishangaa sana kusikia ujinga huu. Kwani ni Mungu gani asiyetolewa kafala?
            Kwa vile sijapata kanywaji na zile zana nyingine vinifanyavyo nichangamke, leo sitasema mengi zaidi ya kuzidi kukuombea maisha marefu mpendwa wangu Escrow. Wala usiwe na shaka. Wajinga ndio waliwao na mwenye nacho huongezewa.  Nimalizie kwa kuomba unikumbuke kwa ofa kwa ajili ya kanywaji. Mimi sitaki mabilioni na mamilioni kama wale waroho tena wakubwa wakubwa wenye kufanya mambo ya kitoto na kifisi na kifisadi. Mungu ibariki Escrow. Mungu ibariki IptL.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: