The Chant of Savant

Wednesday 18 January 2017

Kijiwe chalaani bakora Rorya


            Baada ya kurushwa picha za akina Mura Msama, Magesa, Nyambora, Wambura na Kitamara wakimsulubu mama mmoja kwa utovu wa nidhamu, kujiwe kimeamua kuongeza shinikizo dhidi ya udhalilishaji huu wa kizamani na kinyama. Kama si ukata, kijiwe kilitaka kwenda Kinesi hata Kuruya kuangalia kadhia nzima na kuwasulubu wale waliomsulubu mwenzao bila aibu wala stahiki.
            Sofia Lion aka Kanungaembe ameguswa kiasi cha kuanzisha mada kwa mara ya kwanza.
“ Nadhani kila mmoja amejionea udhalilishaji wa akina mama unaoendelea kwenye karne ya 21. Kama mwanakaya na mwakakijiwe naleta hoja ya kutaka tulaani upuuzi huu; na hata ikiwezekana twende kule tutoe adhabu ili liwe somo kwa wengine. Hivi hawa hawajui kuwa anayemdhalilisha mwanamama ni kumdhalilisha mama yao?”
            Mpemba anamchomkea Da Sofi na kusema “japo si tabia yangu kuchomekea, wacha leo nkuchomekee dadaangu. Sie tumefunzwa kuwa jicho nkwa jicho. Kwanini hawa wazee nao wasiitwe wakachapwa bakora hadharani lau waonje chungu ya kile walichontendea huyu mama asokuwa na hatia? Maana bila kufanya hivo, wawezaendelea na huu utwahuti wao.”
            Mgoshi Machungi anakula mic “kama ingekuwa Ushoto hawa wangeitwa na kuchapwa bakoa ii nao waonje uchungu wa huu ujinga na ujima wao. Kama wanajichukuia sheia mikononi, mahakama zitafanya kazi gani?”
            Msomi Mkatatamaa anaamua kula mic “nadhani tunapowalaumu hawa wazee wa jadi peke yao wanaofanya upuuzi chini ya kivuli cha mila tunakosea. Kinachojionyesha hapa ni kwamba tangu tupate uhuru, mamlaka zetu hazikuelimisha wachovu wake juu ya haki za kiraia na haki za binadamu. Hata hivyo, sichangai. Ni matapeli wangapi wamejaa kayani wakiwaibia wachovu chini ya kuhubiri dini wakati ni wizi mtupu? Je hawa wana tofauti gani katika kudhalilisha wachovu na hawa wababu wa kimura walioamua kujifanya sheria? Nadhani tukubali. Kaya yetu ina uoza mwingi wa kimfumo ambao mamlaka yameufumbia macho tokana na kuogopa kuamsha waliolala wakalala wao.”
            Mipawa anakula mic “ukweli ni kwamba ukombozi wa mwana mama uko mbali sana. Huoni hata kwenye siasa namna wanavyogawiwa nafasi za nyuma huku wakitumika kama nyenzo ya kusakia kura? Ni bahati mbaya kuwa hata vyama vya upingaji vimeukwaa mkenge huu wa ubaguzi na unyonyaji wa kijinsia.” Anamgeukia Sofia na kusema “hata hapa kijiweni mwana mama uko peke yako. Kwanini? Ni kwamba wenzako wanazuiliwa na waume zao kuja hapa kutoa changamoto zao ili ziwekwe wazi na kushughulikiwa. Au nadanganya?” Sofia anatikisa kichwa kumuunga mkono.
            Kapende naye anaamua kung’ata mic “ japo nakubaliana kuna ubaguzi na udhalilishaji wa akina mama wa kimfumo kama wa kuwadai rushwa ya ngono kama mhadhiri wa Chuo cha Usafiri aliyenyekwa juzi, wengine wemezidi. Ukisikia vipigo vya kuua wachovu vimetokea, ni huko huko kwa akina mura. Zikilipuka habari za mapigano ya kikabila kule kule. Hii maana yake ni kwamba lisirikali limelala. Na sasa hawa wababu waliotoa amri ya mama kusulubiwa hadharani wanalistua ili liamke na kufanya mambo kiutuuzima na kisasa badala ya kupiga politiki za kutishia vyombo vya umbea.”
            Kanji anaamua kuchumpa na kuzoza “mimi ikolia chozi kuba sana siku naona ile mama sulubiwa. Veve Sofi sema kitu kuba sana. Iko nyonyaji sana ya mama.  Kwa jumbani yetu mama yote nanyonya. Kwa dukani yetu bado nanyonya. Kwa taa yetu bado nanyanyasa mama. Mimi taka vatu vote badilika na hesimu mama yote ya kayani.”
            Mheshimiwa Bwege aliyekuwa akisikiliza kwa makini anaamua kutia buti na kuzoza “Kanji nakubaliana nawe usemayo. Majumbani hasa kwa magabacholi ambapo dada zetu wengi wanatumikishwa kama watumwa wananyonywa na kubaguliwa kweli kweli. Juzi juzi dada mmoja alisimulia anavyolazimishwa kula mabaki ya magabacholi kila anapowapikia na kuwatengea. Alidai kuwa haruhusiwi kulia mezani bali chini tena jikoni. Kusema ukweli, huu ni uoza wa kimfumo dhidi ya kina mama ambao nao wanaonekana kuushiki hasa ikizingatiwa kuwa hata wasaidizi wengi wa majumbani wananyanyaswa na mabosi wao ambao ni akina mama wenzao.”
            Sofia anakula mic tena “kaka Mheshimiwa nakubaliana nawe. Kama alivyosema Msomi, huu ni uoza wa kimfumo uliotambuka nyanja zote za kimaisha. Kama nilivyosema, hawa wazee wa kimura wanapaswa kuwekwa hadharani na kuchapwa bakora. Kama alivyosema kama Mpemba, wanastahili kupewa shubiri ile ile waliyompa mama mwenzetu ambaye sasa amedhalilika zaidi baada ya picha yake kurushwa kwenye mitandao dunia nzima. Ni jana tu kaka yangu aishie Kanada alinitumia picha hiyo kwenye simu yake akilalamika kunani hadi tunajivua nguo hadharani. Kama haitoshi, hata vyombo vya habari vya kimagharibi vimeishaidaka na kuionyesha Afrika kama bara la watu wakatili wasio na kifani.”
            Mbwamwitu anaamua kumchokea da Sofi na kusema “hapa dawa ni moja. Just kick their ass. Hawa wadingi ni akina nani hadi watangaze ubabe hadharani? Au hawakujua kuwa miongoni mwao walikuwamo mapaparazzi waliotumia simu zao kuwaanika? Ama kweli ujinga ni mzigo.”
            Kabla ya kuendelea si akapita mura Nyambola, acha tumtie kati ili tumpe adhabu! Kama si kujitetea kuwa yeye hakuwako kule wala haungi mkono upuuzi huyu, angeishia kutolewa kafara na kusulubiwa kwa niaba ya wenzake.
Chanzo: Tanzania Daima leo Jumatano.
 

No comments: