The Chant of Savant

Wednesday 25 January 2017

Wizi ndani ya wizi AUWSA wahusika wawajibike

Image result for photo of ruth koya
             Hivi karibuni, vyombo vya habari vilifichua wizi wa kutisha kwenye Mamlaka ya Maji kule Arusha (AUWSA) ambapo zilitumika jumla ya shilingi 198 milioni kuchunguza ufisadi wa shilingi milioni 18. Mwanzoni nilidhani utani. Kwa vile vyombo vya habari havina utaji na mafisadi, baada ya kusoma habari nzima nilibaki kuchukia na kupigwa na butwaa hasa kipindi hiki ambapo taifa limo kwenye mapito ya kulirejesha kwenye mstari na kupambana na ufisadi na wizi wa mali za umma. Kabla ya kusema mengi, lazima niseme wazi wazi kuwa wahusika wawajibike wenyewe au wawajibishwe mara moja ili kutoa onyo kwa masalia ya mafisadi yasiyosoma alama za nyakati.
Ni akili gani kutumia milioni 198 kuchunguza ufisadi wa milioni 18? Inanikumbusha kisa cha hivi karibuni ambapo dereva wa basi nchini Korea ya Kusini alitimliwa kazi kwa kuiba dola mbili za nauli wakati mkuu wa Samsung Jay Y Lee akidaiwa kumhonga jumla ya dola milioni 36 Choi Soon-Sil mshirika wa rais aliyesimamishwa madaraka Park Geun-hye. Ajabu ya maajabu, pamoja na kuhonga mamilioni ya dola, Lee aliachiwa huru kiasi cha kuonyesha kuwa kuna sheria za walio nazo na wasio nazo. Sidhani kama tanzania tunahitaji kuwa na sheria za namna hii ingawa kuna ushahidi kuwa serikali zilizopita zimewahi  kufanya hivyo hasa tukiangalia kashfa sugu kama vile EPA, Escrow, IPTL, Ndege ya Rais, Rada UDA na nyingine nyingi.
            Tukirejea AUWSA, ukisikia kuuza ng’ombe kwa kesi ya kuku ni huku. Je hii ni akili au matope? Kwanini wahusika hawakufanya mahesabu ya darasa la kwanza na kujua kuwa kiasi walichopanga kutumia kuchunguza ufisadi kilionyesha ufisadi mkubwa kuliko ule uliofanywa? Hii ni sawa na kumpiga mbu risasi huku ukitaka kumpiga kibao tembo kwa dhamira ya kuwaua wote.
            Je wahusika wanangoja nini wakati kila kitu kiko wazi?
Hivi nao wanangoja watumbuliwe na rais John Magufuli au waziri mhusika? Kwanini hawataki kutumia common sense na kuachia ngazi?
            Gazeti moja litolewalo mara moja kwa wiki lilifichukua kuwa wajumbe walioteuliwa na mkurungenzi wa AUWSA, Ruth Koya walikuwa wakilipwa shilingi 800,000 kwa siku fedha ambayo hata wabunge na mawaziri hawajawahi kulipwa kwa siku tena kufanya kazi isiyo na kichwa wala mguu. Ajabu ya maajabu, wahusika eti walikuwa wakilala kwenye mahoteli ya bei mbaya mjini Arusha wakati wao wenyewe ni wakazi wa mji wa Arusha. Haya ndiyo yale aliyowahi  kusema rais John Magufuli kuwa Tanzania ilifikia pabaya ambapo wajumbe wa bodi walifikia makufuru kwa kuweza kufanya vikao vya bodi ughaibuni wakishughulikia masuala ya Tanzania kana kwamba Tanzania hapakuwa na hoteli. Hapa hujagusia nauli za ndege ambazo hata hawa wa Arusha walilipwa.
             Sasa nini kifanywe?
Mosi, mbali na mkurugenzi wa AUWSA, wote waliohusika na ufisadi huu wa kijinga watajwe na kuwajibisha mara moja kama watashindwa kujiwajibisha ili kupisha uchunguzi kama kweli hawakuwa wamedhamiria kufanya ufisadi.
            Pili, wahusika wa kashfa hii hawapaswi kujiwajibisha wala kuwajibishwa tu bali kufikishwa makamani na kurejesha fedha ya umma waliyoiba kwa njia ya kuchunguza kipele wakati wao wakiwa ni majipu tena sugu bali wasimamishwe kazi kwanza kama nafsi zao zitashindwa kuwasuta wakajiwabisha wenyewe. Hawa ni wahalifu wanaposwa kutoonewa huruma hasa ikizingatiwa kuwa wanapofuja na kuiba fedha za umma hivi, hutumia njia za ajabu kama kupandisha bei ya huduma ili kuendelea kupata fedha ya kuiba na kuchezea.
            Tatu, nashauri uchunguzi ufanywe kwenye taasisi za umma ambamo kumetokea kashfa kama hizi na kuchunguzwa ndani kwa ndani. Inawezekana kilichotokea Arusha ni kipele wakati kuna majipu makubwa tu. Hii inapingana na juhudi za rais za kubana matumizi ili fedha itakayookolewa iwafae maskini badala ya kuendelea kufujwa na kuibiwa na matajiri wengi waliokwisha kujineemesha kwa njia hii miaka nenda rudi chini ya tawala za hovyo zilizopita.
            Nne, mtuhumiwa wa kwanza yaani Koya, alipaswa kuwa nje ya ofisi na mahabusu ili kuepuka kuharibu ushahidi kama ilivyozoeleka nchini ambao inapotokea kashfa kama hizi ushahidi hupotezwa hata kwa kuchoma ofisi bila kujali hasara wahusika wanazolitia taifa.
            Tano, uteuzi au uajiri wa Koya unapaswa kuchunguzwa kuona kiwango chake cha elimu na namna alivyoajiriwa hata kupandishwa cheo kufikia alipo kiasi cha kutojua mipaka ya wadhifa wake. Nimekuwa nikipiga kelele kuwa tunao vihiyo, mafisadi na wahalifu wengi kwenye ofisi na taasisi za umma karibu zote bila kusikilizwa. Sasa naamini wahusika watasikia na kuchukua tahadhari kuhusiana na kadhia kama hizi.
            Itoshe kumalizia kwa kutaka wizara husika ichukue hatua mara moja. Na kama itaendelea kusuasua basi rais aingilie kati ili kuepusha fedha ya umma kuendelea kuibiwa ukiachia mbali mzigo utokanao na kadhia kama hizi kutwishwa wananchi maskini wanaotumia huduma za mamlaka kama hizi. Wahusika wachukue hatua za haraka na za makusudi ili kuepuka kuwapa nafasi watuhumiwa kuharibu ushahidi. Tunaomba kutoa hoja kuwa watuhumiwa wa kashfa ya ufisadi ndani ya ufisadi ya AUWSA ima wajibwajibishe au kuwajiishwa mara moja.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: