How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 4 January 2017

Mwaka huu tufukue kaburi lau moja

Image result for photos of iptl tanzania
 
            Katika mojawapo ya matamko yake, rais John Pombe Magufuli mnamo mwezi Novemba mwaka jana, alisema kuwa hana mpango wa kufukua makaburi. Kwani, yanaweza kumshinda kuyafukia. Kiakili, kuchimbua kaburi ni kazi kuliko kulifukia. Alikairirwa akisema “nimeshughulikia changamoto mbalimbali lakini siwezi kuyafukuwa makaburi yote; kwa sababu kuna mengine nitashindwa kuyafunika, sikuja kufukua makaburi nataka kuanza na yale niliyoyakuta ili tujenge Tanzania yetu.” Kauli hii ya kifalsafa iliwachanganya wengi hoi huku wakiwa wameshangaa na kugawanyika. Wapo waliochukia na kubeza ujasiri wa Magufuli. Wapo waliofurahi; hasa wale ambao uchafu wao utaachwa kuendelea kufichwa kwenye makaburi yao ya utawala wao. Wapo waliochanganyikiwa kiasi cha kushindwa la kufanya wala la kusema. Zaidi ya yote, wapo waliodhani makaburi tajwa na vigogo wa zamani katika serikali zilizopita. Wapo walitafsiri kama kashfa kubwa kubwa ambazo serikali tatu zilizomtangulia zilitenda. Kila mmoja aliambua chake ingawa ukweli uko wazi kuwa alichoongelea rais ni kwamba atashughulikia baadhi ya uchafu na kuacha mwingine. Jambo hili pia linampunguzia rais kwa wananchi hasa kama atakumbuka kuwa atashughulikia au kupambana na ufisadi bila kuogopa wala kupendelea.
            Ya mwaka jana yamepita. Sasa tugange yajayo. Mwanzoni mwa mwaka ni wakati mzuri wa kujiwekea vipaumbele vya kutekeleza kwa mtu binafsi hata taifa. Hivyo basi, tunapendekeza mwaka huu tufanye mageuzi katika malengo na vipaumbele vyetu.  Katika kufanya hivyo, tufukue japo kaburi moja tu. Kwa vile rais alisema hatafukua makaburi yote asijeshindwa kuyafukia, tungemtaka atoe sababu za kushindwa wakati ana kila zana chini yake.  Kama akiendelea kuyagwaya haya makaburi, basi awapishe wenye uwezo wa kuyafukua na kuyafukia ili haki itendeke.
            Mwaka huu tuanze na wezi wa Escrow ambapo kampuni tatanishi la Independent Tanzania Power Limited (IPTL) lilikwapua mabilioni ya shilingi toka kwenye fedha za umma kwenye akaunti ya Escrow. Mara nyingi serikali imesikika ikisema kuwa wananchi wenye taarifa za uchafu wowote waipe taarifa ili iweze kuushughulikia. Sisi hatutoi taarifa mpya bali kumkumbushia kuwa kaburi la wazi tena lililojaa vyetu ni Escrow kashfa ambayo tangu Magufuli aingie madarakani amejaribu kutoigusa. Je kunani? Je IPTL ni mali ya nani?  kuna haja ya kujua walioko nyuma ya kashfa hii donda ndugu ambayo inatishia mustakabali wa  taifa letu. Lazima tuwe na ujasiri wa kufanya maamuzi magumu yanayolenga kuliondoa taifa letu kwenye makucha ya mafisadi wachache. Leo serikali inapata wakati mgumu kuhusiana na huduma ya umeme. Leo EWURA wanapandisha bei ya umeme. Kesho waziri anazuia. Je kunani wakati tunajua chanzo cha mauti ya Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO) kuwa ni mikataba ya hovyo na ya kijambazi iliyowezesha wezi wa Escrow kuendelea kutuchezea. Tunajua hili nalo ni kaburi ambalo kama halitafukuliwa na kufukiwa, umma wa watanzania utaendelea kubeba mizigo ya wezi wachache. Lazima tuthubutu japo mara moja. Lazima tufukue na kufukia kaburi lau moja ili wanaopanga kuendelea kuzika taifa letu wapate taarifa.
            Wapo wanaosema Escrow si ya wale tunaowajua ambao habari na sura zao daima ziko kwenye vyombo vya habari. Hawa akina James Rugemalira ni vijididaa ambavyo vimewekwa mbele ili kuwakinga mapapa wenyewe. Wenye IPTL ni tofauti na hawa tunaowajua na kuwaandama japo nao ni washirika katika dhambi hii ya kulihujumu, kuliibia na kulifilisi taifa. Wapo wasio taka kujulikana; tena usiotegemea. Wanajionyesha kama waungwana wakati ni wezi tu wakawaida. Wanajionyesha wanaipenda Tanzania wakati wengi wao walishiriki kuifukia kwenye makaburi haya yanayomshinda rais kufukua kwa hofu ya kushindwa kuyafukia. Je rais anashindwa kuyafukua na kuyafukia au ameamua kushindwa ili asiwaudhi wenzake? Je rais ana mpango wa kuchimba kaburi kama hawa tunaowagopa leo? Sidhani kama Magufuli anashindwa kuyaufukua na kuyafukilia mbali haya makaburi. Wapo wanaosema tumvutie muda. Tumpe muda apate ngwe ya pili tuone vumbi litakavyotimka.
            Ukitaka kujua tunachomaanisha jaribu kusoma historia ya kampuni tata la IPTL. Jiulize rais alikuwa nani, waziri wa nishati alikuwa nani na baadaye alipanda cheo na kuwa nani; na nani alikuwa rais baada ya rais mwanzilishi wa mkakati wa kuingiza kampuni hili kinyemela nchini. Kama taifa, kama kweli tutadhamiria, hatuwezi kushindwa na genge la wahalifu wachache wanaojificha nyuma ya wenzao au ukubwa wav yeo walivyowahi kushika. Hatuwezi kuwa taifa la waoga kiasi cha kushindwa hata kuanzisha miradi ya kuzalisha umeme ili kuwakosesha soko wezi hawa ambao wametuibia kwa miaka nenda rudi. Kwanini nchi huru kwa zaidi ya nusu karne ishindwe kuwa na vyanzo vyake vya umeme hadi kushindwa na vijikampuni vya kitapeli? Hii haiwezi kuwa Tanzania ambayo wazee wetu walipigania; na wengine kufia. Ni aibu na laana ya ajabu kuendelea kushikwa mateka na vijikampuni tapeli kama IPTL kati vya vingi.
            Tunaongelea makaburi makubwa. Je na haya madogo kama yale yaliyoko bandarini yakiendelea kutuibia nayo yatushinde? Tunashindwa na makaburi kama hiki kilichojitwalia Kampuni ya iliyokuwa Shirika la Uma la Usafiri Dar Es Salaam (UDA)? Tumekuwa wa hovyo hivi!
            Leo sisemi mengi. Nashauri lau tufukue kaburi moja kuonyesha kuwa tunaweza hata kulifukia bila kujali uoza uliomo au aliyeuweka humo.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: