Kampuni ya Azimio Housing Estate, iliyotuhumiwa kujihusisha na ufisadi kwenye mradi mzima wa Dege Eco Village ilitoa mpya kwa eti ilijifanya kuwa na huruma na kuwajali watanzania kwa kutoa hekari 1,500 bure kwa mkoa wa Dar Es Salaam ili kujenga viwanda vidogo vidogo. Wema mara nyingi ni kitu chema japo kinaweza kuwahadaa wengine hasa unapotendwa na mtu mwenye kutia kila aina ya shaka. Sina ugomvi na wema kupitia kutoa misaada inayohitajiwa na jamii. hata hivyo, nina ugomvi na sifa na dhima ya kutoa misaada husika hasa mtoaji anapokuwa na mawaa au tuseme tuhuma za kuwahujumu wale wale anaolenga kuwahadaa kwa kujifanya anawajili kiasi cha kujinyima na kuwasaidia leo wakati aliwaibia jana. Ieleweke; sina haja ya kuwa hakimu katika kashfa hii ambayo kesi yake bado iko mahakamani. Ninachojitahidi kufanya hapa ni kuonyesha utata na shaka vinavyoweza kujengwa na msaada wa namna hii na wakati unapotelewa ukiachia mbali mazingira ya kuupata ambayo hayajabainishwa. Kwanini sasa ambapo mtoaji na mpokeaji wanaandamwa na kashfa kibao zote zikijikita kwenye upatikanaji na ulimbikizaji haramu wa mali?
Ukiachia kuhoji muda na watoaji na wapokeaji misaada, napata taabu sana. Je tunahitaji kupwakia misaada kama jamii bila kujua nani anatoa na kama ana sifa hasa pale tunapojua kuwa mhusika ni mtuhumiwa katika kashfa ya wizi mkubwa kwa taifa ukiachia mbali lengo la kufanya hivyo? Je tumegeuka wa hovyo kiasi cha kupewa vitu vidogo vidogo ili tusiulize vikubwa vikubwa vimeliwa na nani?
Je Mkuu wa Mkoa aliyepokea ardhi kwa niaba ya rais alijiuliza namna nchi ambayo sheria inatamka wazi kuwa serikali yake ndiyo yenye dhamana ya kusimamia ardhi kwa watanzania ilikuwaje maskini wa ardhi hadi kupewa ardhi na watu binafsi? Je huyu mkurungenzi wa Azimio Housing Estate, Mohamed Ikbar, alipataje na lini ardhi hii anayogawa? Je nani atamrejeshea fedha aliyotumia kununua ardhi husika kama kweli aliinunua? Je anategemea kupata nini au anajenga mazingira gani? Kinachoshangaza sana na kuhuzunisha, utakuta baadhi ya wale wale waliohujumu taifa letu na kufanya vijana wawe maskini ndiyo hao hao wanaojifanya kuwajali kwa kuwapa udohoudoho huku wao wakikalia makubwa. Kuna ushahidi wa wazi kuwa kuna watendaji wetu wanaopwakia kila kitu bila hata kufikiri wala kuhoji. Mfano mzuri ni mbunge Mbunge wa Mkuranga (CCM), Abdallah Ulega alikrarirwa akibariki upogo huu akisema “papai si haramu, ila kinachotokana na papai ndicho haramu ambayo ni pombe ya gongo. Sasa kama mtu katoa ardhi yake bure tupambane kupata viwanda maana ajira hakuna. Tupate Sido kubwa na siyo kuwaza mtu aliyetoa ardhi hiyo,”
Kama jamii na taifa, je tutaendelea na upofu, uroho na upogo huu hadi lini? Yaani tumegeuka samaki kutegwa kwa utumbo wetu wenyewe? Samaki ni hayawani. Je sisi tumeridhika na uhayawani huu tena wa kujitakia? Nani ameturoga.
Tunashauri yafanyike yafuatayo:
Kwanza, kabla ya Azimio Housing Estate kutoa ardhi, ima ichunguzwe ilivyoipata huku serikali ikiulizwa ilikuwa wapi hadi inakuwa maskini wa ardhi wakati ndiyo yenye dhamana ya kusimamia ardhi nchi nzima?
Pili, hili dili la Makonda na Ikbar lizuiliwe ili kujua ukweli wa ardhi iliyotolewa na namna ilivyopatikana? Waingereza wana usemi kuwa amlipaye mpiga filimbi ndiyo huchagua nyimbo. Je tunahitaji msaada wa watu ambao wametumia mianya ya ufisadi na upumbavu kwenye mfumo wetu hadi wanatupa kilicho chetu wakati ni chetu tena wakiondoka wakijiona wametutendea hisani wakati siyo?
Wasiojua chanzo cha maswali haya, warejee ukweli kuwa mwaka 2015 Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa fedha aligundua ufisadi wa kutisha ambapo inadaiwa kuwa NSSF imenunua ekari hizo kutoka kwa mbia mwenzake Azimio Housing Estate Limited kwa zaidi ya Sh800 milioni kwa ekari, wakati shirika hilo linamiliki viwanja vingine maeneo hayo vyenye thamani ya Sh4.5 milioni kwa ekari. Kwanini Azimio Housing Estate wasimalize kashfa hii ambapo hata hizi hekari 1500 ni sehemu ya kashfa. Huu ni ukarimu au kugeuzana majuha. Vijana wasitumiwe kuhalalisha ufisadi tena uliofanywa dhidi yao. Kwanini serikali isitaife hii ardhi kama watuhumiwa watashindwa kutoa maelezo yanayoingia kichwani? Je hawa siyo wale ambao waziri mmoja waliyetaka kumhonga kama alivyodai aligwaya kuwataja majina? Ilikuwaje akaficha majina yao? Kuna haja ya watendaji wetu kujifunza kujenga shaka na kila anayetaka kuwafadhili kwani si wote wanaowafadhili ni wasafi au wanafanya hivyo kwa nia njema zaidi ya kuficha uovu wao. Haiwezekani maafisa walioshiriki kwenye kashfa ya Dege eco village wawe gerezani wakati washirika wao wakitoa sadaka kwa serikali ili wasamehewa madhambi yao. Kwanini waswahili hatupendi kujifunza? Kila kashfa nyuma yake kuna hawa hawa na wanawaacha washirika zao solemba huku wakiendela kusuka madili mengine tokana na ukosefu wa kushukiana na kupenda vya dezo. Huu msaada wa Makonda si wa dezo na wala wa nia nzuri.
Tumalizie kwa kuwashauri watanzania wasikubali kugeuzwa samaki kutegwa kwa nyama yao wenyewe. Badala ya kupwakia ofay ardhi inayodhaniwa ni ya ubwete, tuhoji upatikanaji wake na sifa binafsi za wahusika tusije kuingizwa mkenge kwa kuhalalisha harama na mauti yetu kama jamii na taifa.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.