The Chant of Savant

Wednesday 18 October 2017

Kuna dawa moja ya kukomesha ufisadi nchini


            Hakuna ubishi. Kwa sasa, rais John Magufuli ni rais anayechukiwa sana kuliko na mafisadi na waliozoea kutajirika bila kufuata utaratibu kuliko rais yeyote wa Tanzania. Vita ya kupigiwa mfano aliyoanzisha dhidi ya ufisadi, pamoja na baadhi ya mapungufu, inafanya aonekane mbaya. Kwa sababu ametia mchanga kitumbua cha baadhi ya watu nchini. Kukamatwa kwa vigogo wa kashfa ya IPTL-Escow ni mfano mzuri hapa. Sidhani kama waathirika na wategemezi na washirika zao wanafurahia kinachoendelea. Uzuri, Magufuli analitambua hilo kiasi cha kuchukua hatua na tahadhari. Hata hivyo, kuna mambo akiyafanya rais Magufuli, atazidi kuwa mwalimu na kivutio duniani juu ya namna bora ya kuendesha nchi. Magufuli anachukiwa sana kutokana na tawala zilizopita kuhalalisha ufisadi kwa mlango wa nyuma bila kujua madhara yake kwa taifa.
            Katika safu hii leo nitatoa ushauri kwa rais Magufuli. Naamini ataupata ima kwa kusoma mwenyewe au watu wake ambao wana uwezo wa kufungia magazeti pale yanapoandika kisichotakiwa. Ufuatao ndiyo ushauri wangu kuhusiana na namna ya kisayansi ya kupambana; na hatimaye kuushinda ufisadi, wizi wa mali ya umma, uuzaji mihadarati na jinai nyingine nyingi zinazomhangaisha rais Magufuli.
            Rejesha sheria ya maadili. Kila mtanzania awajibike kisheria kueleza utajiri alio nao na namna alivyouchuma. Hapa lazima kila mtanzania kujaza taarifa zake za kodi kila mwaka ili kuona kama kinachotangazwa kinalingana na kile anachopaswa kuwa nacho kihalali kwa mujibu wa kumbukumbu za kodi. Hili litaondoa motisha wa watanzania kujiingiza kwenye jinai za kusaka utajiri ambapo ilikuwa jambo la kawaida kwa mtu kulala maskini na kuamka tajiri bila kuulizwa. Wengi walizoea kutuibia na kutumia utajiri wetu kutukoga huku wengi tukijua walichofanya kufikia ukwasi huu.
            Serikali ya awamu ya kwanza ilitumia utaratibu huu kuondoa uoza kama vile uuzaji mihadarati, wizi wa mali za umma, ujambazi na ufisadi katika taifa. Kwani, hapakuwa na namna yoyote ya mtanzania kuchuma na kula bila stahiki. Mfano, viongozi wa umma wawe wa kisiasa au kiroho au wa namna yoyote, wasiruhusiwe kuwa na mishahara miwili wala kufanya siasa au dini na biashara. Hili licha ya kuondoa ubinafsi, litaondoa au kupunguza ukosefu wa kazi kwa vijana wetu wanaohitimu kwa maelfu wakaishia kushawishika kujiingiza kwenye jinai kama mihadarati na wizi hata umalaya kwa wale wa kike.
            Kuzuia mianya yote ya kupata kipato au utajiri bila kutoa jasho au kwa njia yoyote haramu kutaondoa na kadhia nyingine iliyokuwa imeanza kuzoeleka yaani uvivu na kupoteza muda kwa baadhi ya watanzania hasa wafanyakazi katika ofisi za umma.  Kwani, kuna watu ni matajiri lakini hawajulikani wanafanya kazi gani. Kukosekana kwa sheria iliyokuwa ikiwataka waeleze walivyochuma kulikuwa motisha tosha kwa baadhi ya wahalifu kuvunja sheria na kujiingiza kwenye jinai mbali mbali kama zilivyotajwa hapo juu. Hii haivumiliki hasa kwa taifa ambalo lilikuwa linaelekea kujiangamiza lenyewe tokana na kuachia mambo yajiendee.
            Pamoja na kuwa na sheria inayowataka watanzania kutoa taarifa za utajiri wao kwa lazima siyo kutaka, lazima ziwepo taasisi za siri za kuwachunguza na kuchunguzana huku wananchi nao wakiwa sehemu ya macho ya umma dhidi ya ufisadi au upatikanaji mali kiharamu. Hili ni muhimu ukiachia mbali ufuatiliaji na utaratibu unaoeleweka wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa mali za watanzania. Tokana na uzoefu uliopo ambapo baadhi ya watu wanaweza kupendelewa kutokana na ukaribu wao na wakubwa, kuna haja ya kuwa na sheria za wazi ambapo kitu kama hiki kitatokea iruhusu mwananchi yeyote kwenda mahakamani kushughulikia kadhia hii.  Tukitumia uzoefu tulioupata kwenye zoezi la kufichua na kupambana na walioghushi vyeti vya kitaaluma au kutumia majina ya wengine, lazima kuwepo na mfumo unaoweza kumbana yeyote mali zake zinapotuhumiwa kupatikana bila stahiki bila kujali ukubwa wa cheo chake au ukaribu wake kwa wenye madaraka.
            Uchochoro uliobakia kwa mfumo wa kifisadi nchini ni ukosefu wa sheria ya maadili ambayo nayo haiwezekani kuwa na maana wala makali bila kuwa na katiba mpya ambayo watanzania waliitaka na wanaihitaji pamoja na  wakubwa wachache waliowahi kutenda uovu kuiua ili wasiishie mikononi mwa vyombo vya dola. Hivyo, namna mojawapo kwa Tanzania kuondokana na ufisadi uliokithiri ni kuwa na katiba mpya ambayo inaweka wazi namna ya kupambana na kushughulikia ufisadi nchini. Hivyo, tunaishauri serikali kupambana vita inayoonyesha wazi haitashinda wala kulalamika bali irejee mchakato wa kupata katiba mpya ili iwe nyenzo muhimu katika kupambana na ufisadi. Kwa yeyote anayeitakia Tanzania mafanikio, awe mwananchi wa kawaida au kiongozi, anapaswa kuliona hili vinginevyo kushindwa kuwa na katiba mpya na sheria ya maadili ni kufuga ufisadi huku tukiulalamikia wakati tunaogopa kuchukua hatua za kisayansi kupambana nao.
Chanzo: Tanzania Daima J'tano leo.

No comments: