Msomi Mkatatamaa anaingia akiwa na matabu makubwa mawili moja likiitwa How to Zap and Kill Uknown Killers na jingine, How To Make Uknown Known. Anayabwaga mezani akionyesha wazi kuwa na mawazo. Anaamkua na kuagiza kahawa yake. Mchunguliaji asiyepitwa na kitu ni wa kwanza kuchukua mojawapo na kuanza kusoma kana kwamba kimombo kinapanda.
Kabla ya kumwaga sera, Kapende anamchokonoa “Msomi leo unataka kuturudisha chuo nini; mbona umekuja na ma-cyclopedia leo; kunani?”
Kabla ya kuendelea Mgoshi Machungi anamkosoa “sema enseikoopidia siyo seikoopidia unatamka kama wasomi wa kisiku hizi wa chuo kikuu cha Manzese waliopata digii kwa vyupi.”
Msomi anatikisa kichwa, kutabasamu na kuzoza “hujui kuwa sijakubali damu ya rafiki yangu Tunduni Lissu imwagike bure? Nipo najichua kitaaluma lau niweze kuwanyaka waliomfanyia kitu mbaya rafiki yangu halafu wakaachwa waendelee kutanua mitaani.” Anapiga chafya na kuendelea “nashindwa kuelewa ni kwanini geshi la polishi limeshindwa genge dogo la wapumbavu na wahuni kiasi hiki wakati lina ujuzi.”
Kabla ya kuendelea Mipawa anajibu “sidhani kama limeshindwa. Kama limeshindwa basi limeshindwa kitu kimoja yaani kuwa na nia ya kuwasaka na kuwanyaka mbwa hawa wasio na huruma wala utu. Haiwezekani genge la majibwa wachache lituhangaishe kana kwamba hatuna wasomi wa security na intelligence. Kama limeshindwa, sasa linalipwa njuluku zetu kwa lipi wakati haliwezi kutuhakikishia usalama? Ni aibu ya mwaka kusema ukweli.”
Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anamchomekea “japo mbinu zako ni za kisayansi na zinaingia akilini, angalia wasikunyotoe roho kama walivyotaka kumfanyia Tunduni mchana kweupe huku kamera zikinasa kila tukio lakini ndata wakashindwa kuwanyaka.”
Mpemba anamchomekea Mbwamwitu “wallahi hawa hawamwezi Nsomi. Ninjuavyo mie japo hii siri, aweza uawa na SEAL peke yao wale waliomnyotoa roho bin Laden kule Aborabadi. Huyu tulie naye wengi hamnjui. Amewahi kutumiwa sana na FBI na M16 mbali na mashirika mengine ya kipelelezi duniani. Hata hivo, hii n siri. Huwa hataki julikana ingawa sie watu wake wa karibu tunjua hii kitu”
Msomi anatabasamu na kuzoza “hapo nimekupata vilivyo. Kitaalamu, uhalifu uliotendwa na wanaojiita wasiojulikana ni simple. Mfano, nashauri tuunde timu yetu ya kijiwe kuwasaidia geshi kuona udogo wa suala linalowashinda. Lazima hawa mbwa wasiojulikana wajulikane kwa uba na uvumba.” Anakohoa na kuendelea “kama nilivyosema, ni rahisi kuwanyaka hawa mbwa kirahisi. Kwa ufupi, nitaonyesha ramani ya namna ya kuwanyaka. Kwanza, unaangiza CCTV camera zote za maeneo lilipotokea tukio uzione na kuzichunguza kujua nani walifika eneo husika. Pili, ukishindwa hili, unaweza kuitisha camera za barabarani ili kubaini ni magari mangapi yanayofanana na lile linalosemekana kuwabebwa magaidi uchwara hawa. Tatu, unamhoji Lissu na dereva wake kuona kama wanaweza kukupa lau picha ya watuhumiwa. Nne, unawahoji wahishimiwa wote waliowahi kulalamika na kuripoti kufuatiliwa na kundi hili uchwara. Na mwisho, unawanyaka wote unaowastukia kama vile yule mpumbavu aliyejitangaza wavuni kuwa alikuwa tayari kumdedisha Lissu kama angepewa ruhusa na anaowaabudia asijue ni ngurumbili wa kawaida watakaodedi siku moja. Mwisho kabisa, baada ya kukusanya majina ya watuhumiwa na sura zao, nakwenda kwenye makampuni ya simu na kutaka mawasiliano yao mbali na kutaka yanipe simu zilizokuwa kwenye eneo hili mida lilipotokea tukio. Maana, lazima makampuni ya simu yatakuwa na mawasiliano yao na locators za simu zilizokuwapo eneo husika. So simple. Hii ndiyo summary ya mkakati wangu wa kuwanasa wanaharamu hawa tena haraka. Natamani nimpige zongo huyu nguuwe waahi.”
Baada ya kumaliza kuongea, kijiwe kinampigia makofi kwa kuonyesha umahiri katika masuala ya upelelezi aliyosomea kwa Joji Kichaka na kwa Maza huku mzee Maneno akichombeza “Ama! Kweli nyinyi ndiyo wasomi tunaowahitaji na siyo hawa wa kughushi kibashiteshite.”
Kabla ya kuendelea Kanji anakula mic “mimi dugu yanguni iko tayari kuleta peleleji toka Bombei.” Hata kabla ya kumalizia sentensi yake, Mijjinga anamnyang’anya mic “Kanji acha utani. Unadhani gabacholi wanaweza kumpata mtu zaidi ya kumtoa njuluku na kulejea kwao kama walivyofanya akina Chavda na yule aliyetorosha twiga wetu na wengine wa RITES? Unadhani tumesahau siyo?”
Sofia Lion aka Kanungaembe anamuunga mkono Mijjinga kwa kusema “hata mimi sikubaliani na Kanji hasa ikizingatiwa jamaa walivyo fisadi kinomi. Wao waendelee na mishemishe zao za kupiga njuluku zetu na kuwabagua ndugu zetu wanaofanya kazi jumbani yao.”
Mgoshi Machungi anaamua kula mic “tena imetikumbusha yue mpumbavu aiyeomba ruusa amuue Tunduni. Je geshi iishamnyaka au naye anaeewe kama hawa wanaojiita wasiojuikana.”
Mheshimiwa Bwege aliyekuwa akisikiliza kwa makini anaamua kutia guu “nadhani mmesema mengi. Kwanini tusiunde taskforce hapa hapa ili tukitoka hapa tuanze kazi ya kuwanasa hawa nguchiro. Chini ya uongozi wa SEAL Msomi sina wasi wasi tutawanyaka ndani ya siku mbili au tatu; au siyo?” akiwa anajiandaa si simu ya Msomi iliita! Kabla ya kujibu, anatuonyesha na kusema “unaona hii namba ya hatari? Ni ya rafiki yangu mkuu wa chuo cha kufundisha SEAL kule kwa Trumpet ananipa updates.
Chanzo: Tanzania Daima J'tano leo.
No comments:
Post a Comment