Hakuna ubishi; rais John Pombe Magufulli sasa ni jina kubwa duniani. Hii ni kutokana na staili yake ya uongozi hasa kupambana na maouvu na kubana matumizi
Alipokataa kufanya ziara nje ya nchi wengi walisema mengi. Alinyamaza na kuendelea na mipango yake ya kuiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia baada ya kupoteza umaarufu uliokuwa umejengwa na baba wa taifa Mwl Julius Nyerere. Kwa msimamo na staili ya Magufuli, uwezekano wa kuwa kioo na si kiongozi tu wa Tanzania bali Afrika ni mkubwa. Hata hivyo, kuna mambo machache anayopaswa kufanya Magufuli ili kuweza kufikia hadhi hii adhimu duniani.
Leo nitadurusu baadhi ya mambo yanayoonekana kumharibia au kukwamisha, kama si kupunguza, sifa za rais Magufuli.
Mosi, kama atataka kuwa kioo mithili ya wachache kama vile Nelson Mandela, rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini na kwa mbali marehemu Ketumire Masire wa Botswana, anapaswa kuachana na kuvizuia vyama vya upinzani kumpinga na kufanya siasa. Kwani, hakuna jambo linalomtia doa Magufuli kama katazo hili linalofanya baadhi ya wakosoaji wamshuku uimla jambo ambalo bado si kweli.
Pili, Magufuli ameonyesha nia na ujasiri mkubwa katika kupambana na ufisadi nchini chini ya dhana yake ya kutumbua majipu. Mfano wa karibu ni pale alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa Jumuia ya Afrika Mashariki. Kwa ushupavu wa hali ya juu, alipunguza na kubana matumizi. Hata hivyo, katika azma yake ya kupambana na ufisadi, Magufuli ameonyesha kupwaya pale alipokumbana na watu wake wa karibu kama vile Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda anayetuhumiwa kughushi vyeti vya kitaaluma. Ni bahati mbaya kuwa si Magufuli wala Makonda aliye tayari kupambana na kadhia hii vilivyo kwa kuzingatia kanuni za uwajibikaji na utendaji haki. Ingawa Magufuli, na hata Makonda, wanaweza kudhani hili limepita, halijapita. Watanzania na ulimwengu bado wanahitaji maelezo na majibu yanayoingia akilini kuhusiana na ukweli wa mambo. Kimsingi, Makonda, kati ya watu walioutia doa utawala wa Magufuli, anaweza kuchukua namba moja.
Japo Magufuli amejitahidi kuwa kimya, ukiachia mbali kusema wazi kuwa hatamuondoa Makonda, kuna madhara makubwa atakayopata. Kwani, kadhia hii inamuonyesha kama mtu mwenye upendeleo, kulindana na kujuana. Mbali na Makonda, ni ile kauli ya Magufuli kuwa hatawachunguza watangulizi wake wanaoshutumiwa kwa ufisadi katika tawala zao. Magufuli alisema kuwa tuwaache wazee yaani watangulizi wake wastaafu vizuri wakati kuna kelele kuhusiana na namna tawala zao zilizyoingiza nchi kwenye dimbwi kubwa la ufisadi kama vile kutunisha deni la taifa bila maelezo, kuingia mikataba mibovu ya uwekezaji inayomhangaisha Magufuli kwa sasa ukiachia mbali matumizi mabaya ya madaraka, fedha na raslimali za taifa. Kwa wanaojua namna haya mambo yalivyofanyika, Magufuli hawezi kuisafisha Tanzania bila kufanya yafuatayo:
Mosi, kuacha sheri ifuate mkondo wake bila kujali cheo wala ukaribu wa mhusika. Pia haiwezekani Magufuli akaonekana anatenda haki ilhali kuna wasioguswa kwenye utawala wake. Mfano wa karibu ni ile hali ya zoezi la kubaini na kushughulikia walioghushi. Kuna wanaoamini kuwa zoezi hili liliuawa baada ya Makonda kujikuta hana utetezi kuhusiana na kashfa zinazomkabili.
Tatu, Magufuli amekuwa akisikiliza upande mmoja wa wanaomuunga mkono hata kutaka kumtumia kwa kujifanya wanapenda huku wakimmwagia sifa lukuki ili kulinda kitumbua chao. Kimsingi, kama kiongozi wa taifa, Magufuli anapaswa kusikiliza wote bila kujali itikadi zao. Anachopaswa kuzingatia ni mantiki na mashiko ya hoja wanazotoa wakosoaji. Yeye ni binadamu; na si Mungu. Na isitoshe yupo madarakani kuwatumikia watanzania wote kwa usawa bila upendeleo wala uonevu. Mfano mzuri ni ule wa marehemu baba wa taifa Mwl Nyerere aliyewahi kuacha watu wake wa karibu kama vile marehemu Chadiel Mgonja alipokabiliwa na tuhuma za uoza mbali na marehemu Abdallah Fundikira alipokabiliwa na tuhuma za kula rushwa. Aliwaacha wakabeba mizigo yao au kuwawajibisha bila kujali uchapakazi wao wala ukaribu wao kwake. Huu ndiyo uongozi wa mfano; na ndiyo maana Mwl Nyerere ameendelea kuwa maarufu hata baada ya kufariki. Huu ni mfano na msaada wa hali ya juu kwa rais Magufuli kama ataamua kuufuata.
Mbali na mapungufu hayo hapo juu, Magufuli amejitofautisha na watawala wengi wa kiafrika wanaopenda kutumia ofisi za umma kwa manufaa binafsi wakifuja mali na ofisi za umma bila kujali kuwa wanaongoza watu maskini. Mfano, Magufuli hajawahi kuhudhuria mikutano mingi ya kimataifa ambayo, mara nyingi, ni mzigo kwa taifa. Rejea alivyoacha kuhudhuria kikao cha 72 cha wakuu wa Umoja wa Mataifa kinachoendelea ambapo viongozi wengi hukutana na kuishi kwenhye mahoteli ya bei mbaya huku walipa kodi wao maskini wakitwishwa zigo hili. Kwa hili, tunampongeza na kumuomba aendelee hivyo bila kujali kelele za wanaomtuhumu kwa kutoiwakilisha Tanzania kwenye vikao hasara vya kimataifa.
Tumalizie kwa kumshauri rais Magufuli aweke sawa, pamoja na mengine, mambo tuliyoainisha hapo juu. Mungu ibariki Tanzania. Mungu mbariki rais Magufuli.
Chanzo: Tanzania Daima J'pili leo.
No comments:
Post a Comment