Wiki hii ni ya kuadhimsha miaka 18 tangu baba wa taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere atutoke hapo tarehe 14 Oktoba, 1999 huko mjini London Uingereza. Kwa wale waliozaliwa kipindi hicho, sasa ni watu wazima wanaoweza kupiga kura na kufanya baadhi ya mambo kama watu wazima kwa mujibu wa sheria.
Watanzania wengi wenye miaka kuanzia 35 wanamkumbuka Mwalimu Nyerere kama nguli wa siasa aliyotoa mchango mkubwa si kwa Tanzania tu bali Afrika yote. Kiongozi mwenye maadili na asiye na makuu wala ubinafsi, mwalimu Nyerere anaingia kwenye vitabu vya historia kama kiongozi aliyejua alichokuwa akifanya hasa yanapokuja masuala ya uadilifu, uwajibikaji, usawa, na haki kati ya mengi. Kwani aliyahubiri haya na kuyaishi tofauti na wasanii wengine wanaotumia siasa kama nafasi ya kujitajirisha. Katika makala hii ya kumbukumbu ya Mwl Nyerere nitajikita kwenye sifa binafsi kama kiongozi. Sitaingia kwenye mambo aliyofanya. Kwani, nafasi haiwezi kutosha.
Mosi, kama baba, mume na kiongozi wa familia, mwalimu Nyerere aliwalea watoto wake na taifa katika maadili aliyohimiza. Hadi sasa, hakuna mtoto wa Nyerere tajiri, au mwanasiasa aliyepata mafanikio au nafasi ya kisiasa tokana na jina la baba yake au kusukiwa na baba yake kama wengi waliotamalaki kwa sasa iwe kwenye ubunge, ubalozi, uwaziri, na vyeo vingine kwa sababu baba zao walikuwa wakubwa.
Pili, kama mwanaume na mume, Nyerere aliishi na kuondoka bila doa lolote la ufuska ambapo baadhi ya viongozi hutumia madaraka kujipatia rushwa za kimapenzi huku wakitoa zawadi za vyeo kwa nyumba zao ndogo. Hili linajidhihirisha kwenye uteuzi wake ambao mara nyingi haukulalamikiwa na yeyote kutokana na kujiepusha na ukabila, urafiki, ukaribu au ulipaji fadhila. Kila mwalimu alipomteua mteule wake, alihakikisha anachujwa na historia yake inawekwa wazi kupitia vyombo vya habari. Ni bahati mbaya; siku hizi uadilifu umetoweka. Kwani, si ajabu kusikia fulani kateuliwa kwenye nafasi fulani ya umma bila kusikia wala wahusika kuwa tayari kuweka wazi historia ya mhusika. Tulifikia mahali hata viongozi wakawa wanasafiri kwa fedha ya umma na watu wasiojulikana majina yao baada ya kuanzisha mtindo wa kuyaficha. Matokeo yake, sasa tunao wateule wenye mabaka kuanzia walioghushi au kutumia vyeti vya wengine huku wakizidi kulindwa na kusifiwa wakati na wahalifu wasio na maadili.
Tatu, mwalimu Nyerere alikufa maskini ikilinganishwa na viongozi wa wakati ule hata wa sasa ambao kwao siasa na mtaji wa kujitajirisha wao, wake, watoto, warambaviatu wao na marafiki zao. Kwa Nyerere, hili halikuingia akilini. Aliishi na kufanana na wale aliowaongoza huku akipambana kuhakikisha pengo kati ya walio nacho na wasio nacho linazibika. Kwa tunaokumbuka kijumba chake cha Butiama, tunafahamu namna alivyojengewa nyumba yake ya pili ambayo hata hivyo, alilazimika kuipokea na hukuishi mle hata kwa mwaka.
Nne, Nyerere alikuwa muadilifu wa kupigiwa mfano. Hakuendekeza urafiki wala kujuana. Hata pale marafiki zake walipopatikana na hatia ya kukiuka maadili, alikuwa mkali kama pili pili. Rejea alivyoamuru kuchapwa bakora rafiki yake na waziri wake marehemu Abdallah Fundikira pale alipobainika kuwa alikuwa amepokea rushwa. Hata baada ya kumpa adhabu hii, Mwalimu aliwatangazia watanzania bila kujali ni aibu gani angepata muathirika. Kimsingi, alitaka huu uwe mfano na onyo kwa watanzania.
Tano, Nyerere alikuwa msomi aliyeelimika na wa kupigiwa mfano. Licha ya kusoma hadi kuwa na shahada ya uzamili, alijisomea sana, kuandika na kuelimisha kila alipopata nafasi. Ni nadra sana kuona kazi zenye kuingia akilini za kitaaluma na kisera za wale waliomfuatia. Kimsingi, Nyerere alikuwa mtu aliyekombolewa na elimu kiasi cha kutaka iwakomboe na wengine. Ndiyo maana, baada ya kupata uhuru, aliamua kutoa elimu, afya na huduma nyingine kwa watanzania wote kwa usawa akitumia vizuri kodi zao.
Sita, Mwalimu Nyerere alipenda sana haki na usawa kiasi cha kutotaka kutendewa tofauti na wale aliowaongoza. Mbali na kutoruhusu watoto na mke wake watumie cheo chake kujineemesha kwa njia yoyote, mwalimu aliwasomesha watoto wake nyumbani sawa na watanzania maskini aliowaongoza tofauti na waliomfuatia ambao walisifika kwa kusomesha watoto wao nje ukiondoa rais John Magufuli ambaye, kwa kiasi fulani, amefuata mfano wa Nyerere kwa kutoruhusu mkewe kuibia au kuutumia umma kwa kuwa na Asasi Isiyo ya Kiserikali au NGO ambayo baadhi ya wake waliomfuata walitumia kujitengenezea utajiri na umaarufu bila stahiki kutokana na kuwa na kulala kitanda kimoja na rais.
Saba, mwalimu Nyerere hakuwa muongo wala msanii. Alisema ukweli hata kama ulikuwa ukiudhi. Rejea alivyowaambia ukweli wakati akitangaza vita ya kumg’oa nduli Idi Amin imla na muuaji wa zamani wa Uganda kuwa vita hii ingeumiza uchumi wa Tanzania kiasi cha wananchi kuwa na maisha magumu kama ilivyokuja kutokea.
Mwisho, Nyerere alikuwa mzalendo wa kupigiwa mfano. Aliheshimika na anaendelea kuheshimika kutokana na sifa hii. Si utani. Leo ukiweka jina la Nyerere kwenye kura, atawashinda wengi walio hai kutokana na sifa chache kati ya nyingi, nilizotaja hapo juu.
Kwa ufupi, huyu ndiyo Mwl Julius Nyerere, kiongozi mahiri na mtaua ambaye ni wachache wanaoweza kuwa kwenye daraja lake duniani. Mungu ilaze pema roho ya mpendwa na baba yetu Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Chanzo: Tanzania Daima J'tano kesho.
No comments:
Post a Comment