Shambulio la kishenzi dhidi ya maisha ya mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) Tundu Lissu limegeuka kongwa kwenye shingo ya serikali. Hii ni kutokana na namna shambulio lilivyofanyika; na namna vyombo vya usalama vilivyolishughulika kwa kutolishughulikia. Mpaka sasa, hakuna anayejua kinachoendelea ukiachia mbali kutokuwepo kwa taarifa za kukamatwa kwa mtuhumiwa yoyote kuhusiana na kadhia hii. Kimsingi, hii inalitia taifa kwenye kona mbaya hasa tokana na kujengeka hisia kuwa mamlaka yameamua kulichukulia, ima kimzahamzaha au kutokuwa na uwezo wa kufanya lolote.
Kutokana na ukimya uliotawala, wapo walioanza kulitumia ima kwa manufaa yao kisiasa au kwa kutaka haki itendeke. Mfano wa hivi karibuni ni kuitwa polisi kwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania Ponda Issa Ponda tokana na msimamo wake dhidi ya kadhia ya kushambuliwa Lissu. Hili kidogo linachanganya. Kosa analotuhumiwa kulitenda Ponda ni kutoa lugha za kichechozi. Kwanza, lugha za kichochezi maana yake ni nini? Je inawezekana kuwachochea watu wenye akili zao kufanya vurugu au kuvunja sheria bila kuwa na sababu ya kufanya hivyo?
Pili, kwa hali inavyoendelea, serikali inaweza kujikuta pabaya hasa ikizingatiwa wapo wanaodhani kuwa haikulipa umuhimu tendo hili la jinai dhidi ya mwananchi wa Tanzania ambaye, kwa bahati mbaya, ni mwanasiasa wa upinzani ambaye anasifika kwa kuikosoa serikali jambo ambalo ni wajibu wake kisiasa kama mpinzani. Je kwanini serikali inapata kigugumizi ima kutoa maelezo yanayoingia akilini au kuwakamata watuhumiwa ambao ilishataarifiwa kuhusiana na kumfuatilia Lissu kwa muda mrefu bila kushgulikiwa? Hali hii, inaweza kufanya wabaya wa serikali kujenga hoja kuwa ilishiriki shambulizi hili jambo ambalo, hata hivyo, halina ushahidi tokana na wahusika kuendelea kutokamatwa wala serikali kutoa maelezo yenye mashiko. Mfano, hivi karibuni, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro alipoulizwa nini mikakati yake ya kuwasaka na kukamata waliomshambulia Lissu alikaririwa akisema “ahsante kwa swali lakini kwa hili sina majibu kwa sababu sitaki malumbano. Sisi tupo kwa ajili ya Watanzania wote ndiyo maana nchi ipo shwari. Mimi ndiye mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na ninawajibika kuhakikisha raia na mali zao zinakuwa salama na kwa kweli ni salama. Kwa hiyo swali lako sina jibu” Kiakili na kwa hali ilivyo tokana na unyeti wa suala husika, jibu la Sirro, licha ya kukosa mashiko na kukwepa kutoa suluhisho, halikutegemewa toka kwa mkuu wa taasisi iliyaominiwa usalama wa watanzania wote akiwamo Lissu. Hivi kweli, kama mkuu wa polisi anaotoa majibu ya kisiasa hivi, serikali itaepuka kulaumiwa?
Tatu, inapaswa serikali ijue kuwa Lissu licha ya kuwa mtanzania anayepaswa kulindwa na vyombo husika vinavyolipwa mishahara toka kwenye kodi ya watanzania wakiwamo wapinzani, ina jukumu la kuwalinda na kuwahakikishia usalama watanzania bila ubaguzi wowote. Mfano mdogo wa karibuni ni kuenguliwa kwa mtangulizi wa Sirro, Ernest Mangu pale aliposhindwa kuzuia mauaji ya Kibiti yaliyotikisa taifa miezi michache iliyopita. Nadhani ndiyo maana waandishi walimuuliza Sirro juu ya hali yake kama mkuu wa taasisi hii nyeti. Na hii si mara ya kwanza kwa Sirro kutoa majibu ya kisiasa na yasiyo ya kitaalamu. Kabla ya hapo, aliwahi kukaririwa akisema “yule kijana kwenye picha ukimwona yuko vizuri tu, sasa wanaposema anapata huduma ya kisaikolojia wakati kwenye magazeti anaonekana hii inatupa changamoto.” Alikuwa akijibu swali kuhusiana na jeshi la polisi kushindwa kumhoji dereva wa Lissu ambaye yuko Nairobi akitibiwa kisaikoloji tokana na trauma aliyopata wakati wa shambulio. Ni ajabu kwa mtu ambaye si mtaalamu wa magonjwa ya akili na trauma kutoa jibu la kisasa hivi. Sirro alijuaje kuwa dereva wa Lissu hakuathirika wakati yeye si mtaalamu wa masuala ya trauma? Picha pekee haiwezi kuonyesha hali ya ndani ya mhusika. Hivyo, ni makosa kutumia mwonekano wa picha kujibu masuala yanayoendelea kwenye kichwa cha mhusika. Mbali na hili, vyombo vya habari vilimkariri Sirro akisema kuwa ni aibu kwa mwanasiasa kutaka kumfundisha kazi askari anayetambua wajibu wake. Je kazi ya mwanasiasa ni ipi hasa pale inapobainika kuwa askari hakutimiza wajibu wake yaani kuwakamata waliomshambulia Lissu au kushindwa kutoa maelezo yanayoingia akilini? Sirro alionya kuwa wanasiasa wasiwafundishe siasa askari lakini yeye akaishia kutoa majibu hayo hayo ya kisiasa.
Wakati Sirro akituhumu familia ya Lissu kutaka kufanya suala lake kuwa la kisiasa, msemaji wa familia Alute Mghwai alimshangaa Sirro na alikaririwa akisema “sisi hatupigi siasa ndiyo sababu tumeamua kushirikiana na serikali na hatuko tayari kuona suala hili linaendeshwa kisiasa lengo letu apone na ukweli ujulikane, hali ya Lissu isitumike kufanya siasa. Tunataka utaratibu wa kawaida ufuatwe bila kuingiza siasa.” Huu si ushauri mbaya wala wa kisiasa.
Tumalizie na suala la kukamatwa Ponda. Je kosa la Ponda ni nini hasa ikizingatiwa kuwa kisheria, kusema kuwa alitoa lugha ya kichochezi haiingii akilini bila kueleza amevunja sheria kifungu gani. Ninachoona hapa, kuna uwezekano wa suala la Lissu likatumiwa kisiasa na pande zote jambo ambalo litazidi kuiweka pabaya serikali. Maana, kuna watakaojenga dhana kuwa haiwezekani serikali yenye kila nyenzo na vyombo vya upelelezi na usalama ishindwe na genge la wahalifu wachache pasiwepo namna. Shambulizi dhidi ya Lissu litaigharimu serikali isipokuwa makini na kuwakamta wahusika huku ikiwataka watendaji wake kuacha kutoa majibu ya hovyo na ya kisiasa.
Chanzo: Tanzania Daima j'pili kesho.
2 comments:
ndivyo inavyokuwa wanyonge huliwa
Je wao watakula lini?
Post a Comment