Kwa wale waliofuatilia namna mbunge wa Chemba Juma Nkamia alivyotaka kupeleka mswaada wa kubadili katiba ili rais wa Tanzania aongezewe muda wa kukaa madarakani na kurefusha muda huo toka miaka mitano hadi saba, watakubaliana nami kuwa jambo hili si aibu na pigo tu kwa taifa bali limepitwa na wakati. Wakati mwingine nashindwa kuelewa kama kweli wapenzi wa udikteta huu uchwara wanaamini haya wanayotaka tufanye. Sijui wanatumwa au wanajituma. Sijui wanajipendekeza au wanapendekeza; hata sijui kusema ukweli.
Tanzania ina watu wengi wanaoweza kuongoza nchi. Nani alijua kuwa atatokea John Magufuli na kufanya anayofanya kiasi cha dunia nzima kushikwa na kihoro? Mama zetu bado wanazaa watu wenye akili lakini si mataahira wasioweza kuongoza nchi yao. Hawa wanaotoa mapendekezo ya ajabu ajabu wakilenga kujipendekeza lau wateuliwe, wanapoteza muda. Kwa wanaomjua rais Magufuli, hatawateua na wala hawatamtumia kufikia malengo yao binafsi. Sidhani kama Magufuli anapenda watu wasiojiamini, wala wasiosoma alama za nyakati wakaacha kufikiri sawa sawa na kuchapa vilivyo wakaendekeza kujikombakomba na kujipendekeza.
Watu wanaotaka kujipendekeza, kama wale waaandishi wa habari waliojipendekeza utawala uliopita wakazawadiwa vyeo, kwa utawala wa sasa wanakosea. Tunawasoma wengi waliogeuza magezeti yao waimbaji kwaya wakidhani dhamira zao chafu hazijulikani. Inakuwa jambo baya sana hasa pale mwakilishi wa wananchi anapojichafua kiasi hiki. Licha ya kuwa aibu, ni hasara kuwa na wawakilishi hata wasiosoma historia ya nchi yao na ya dunia huku wakishindwa kusoma alama za nyakati. Tanzania si nchi ya kutawaliwa na mtu mmoja kama viinchi vingine vya hovyo vilivyotekwa nyara na maimla tokana na kuogopa kuondoka ili madhambi yao yasianikwe. Sijui kwanini hawa wanaodai kuwa tubadili katiba wanashindwa kujua jambo lililotokea wakiwa watu wazima pale ambapo marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere alipoombwa asiachie madaraka mwaka 1985 akakataa. Tena kwa wakati ule, chini ya siasa za vita baridi, Nyerere angekuwa mpenda madaraka, angeweza kuendelea kuongoza hadi kufia madarakani. Ila kwa vile Nyerere aliheshimu watu wake kama watu wenye akili sawa sawa na wasio na ukapa wa mawazo wala watu wa kuwaongoza, aliamua kuwapuuzia wote waliokuwa wanamshauri upumbavu.
Wakati akina Nkamia wakijikomba na kujidhalilisha, rais Magufuli ameonyesha mwelekeo kama kiongozi mkuu wa taifa. Kwani, amesema wazi wazi kuwa hana mpango wa kubadili katiba. Akimjibu mbunge wa Korogwe Vijijini Stephen Ngonyani, Magufuli alikaririwa akisema “ndugu yangu Majimarefu, uliposema niongezewe miaka 20 nilikuelewa kuwa unaniombea niishi miaka 20 ijayo.”kwa watu wenye akili sawa sawa, jibu hili lilitosha kuwakata kilimilimili na kusahau ghilba yao ya kutaka kumtumia rais kufikia malengo yao binafsi.
Tunampongeza kwa dhati kwa kuwaumbua wajinga wasiotaka na kukubali kujifunza kuwa dunia ya sasa si ya kuanzisha utawala wa kifalme. Kwanini watu wa namna hii hawataki kuelewa asili ya mwanadamu kuwa ni kiumbe wa muda? Mnaweza kubadili katiba hata mkasema rais fulani atawale miaka mia. Je ataweza? Wako wapi madikteta kama vile Hastings Kamuzu Banda (Malawi), Felix Houphouet-Boigny (Ivory Coast), Jean-Bedel Bokassa (CAR) Joseph Mobutu (DRC) Gnassingbe Eyadema (Togo) na Omar Bongo (Gabon) ukiachia wachache waliobakia wakiaibika na kuhangaika utadhani hawatakufa? Ni upuuzi kiasi gani kwa binadamu ambaye ni tunda la msimu kufikiri anaweza kuishi muda mrefu kama udongo au jiwe? Hata rais wetu angekuwa mti usiozeeka haraka, tusingekubali kudhalilishwa kiakili kwa kubadili katiba kwa maslahi ya mtu mmoja.
Hata hivyo, Tanzania bado ina watu wenye akili timamu na wanaosoma alama za nyakati. Mmojawapo ni Pius Msekwa aliyekaririwa akisema “ni kwamba miaka kumi tu inatosha, ili kama mtu ni mbaya tuvumilie kwa hiyo miaka kumi na siyo kwamba haikufikiriwa. Na sidhani kama CCM itakuwa na nafasi ya kujadili hilo kwa sasa.” Pamoja na pendekezo la Nkamia kuchefua na kutokubalika, alikaririwa akisema “naomba ibaki hivyo hivyo kama ilivyo kwenye meseji sina cha kuongeza, kuhusu ni lini nitapeleka tena nayo subiri kwa sababu nimesema nimesitisha kwa muda, maana yake nitawasilisha tena nitakapokuwa tayari.” Hii maana yake ni kwamba Nkamia amekamia kuendelea kutuchefua roho wakati rais mwenyewe anayelenga kumpigia debe na kutaka kumuingiza kwenye ujinga huu alishasema wazi kuwa hana mpango huu wa kipumbavu.
Akitetea hoja yake isiyo na mashiko Nkamia alikaririwa akihoji kuwa kuna ubaya gani kuongeza muda hadi miaka saba wakati jirani zetu wa Rwanda wanafanya hivyo? Kwanza, inaonekana Nkamia hajui ni kwanini Rwanda wamefanya hivyo. Pili, huwezi kuilinganisha Tanzania na Rwanda kidemokrasia hata kihistoria. Rwanda wameamua kuwa na miaka saba na kuondoa hata ukomo wa rais kutokana na matatizo yao ya vita vya kikabila ambalo si tatizo la Tanzania.
Kwa mtu anayejua maana ya demokrasia, hawezi kuilinganisha Tanzania na nchi yoyote katika Afrika Mashariki hata Afrika ukiondoa nchi chache kama vile Afrika ya Kusini, Botswana, Zambia, Msumbiji na nyingine ambazo, kwa kiasi fulani, demokrasia yao inakua na kuleta maana.
Tumalizie kwa kumtaka rais Magufuli awaonye hawa wanaotaka kurejesha nchi yetu nyuma wakitaka kufanikisha ujinga na maslahi binafsi. Wakome na kukomaa.
Chanzo; Tanzania Daima J'pili leo.
No comments:
Post a Comment