Baada ya rais John Magufuli kuamua kuwatolea uvivu wachafuzi wa maadili ya taifa, tunadhani ni wakati muafaka kwa waziri anayehusika na masuala haya kumsaidia rais badala ya kungoja kila mara rais ndiye aone tatizo. Leo tunaandika makala hii maalumu kwa ajili ya waziri anayehusika na habari ambaye wizara yake inaguswa na kadhia hii ya uchafuzi wa maadili. Hii ni kutokana na ukweli kuwa baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele katika kutangaza uchafu mwingi unaokinzana na maadili ya kitanzania. Kwa mfano, tangu ateuliwe kuwa waziri anayeshughulikia habari, waziri Harrison Mwakyembe amekuwa mstari wa mbele kufungia magazeti hasa yale yanayoonekana kulalia upande wa upinzani au yale yanayopinga baadhi ya maamuzi ya serikali yanayoonekana kukinzana na ima matarajio ya wananchi au kuwa na ukakasi.
Japo kufungia magazeti yanapokiuka maadili ya uandishi, kama kunafanyika kwa haki bila patilizi wala upendeleo limo kwenye mamlaka ya waziri, kumekuwapo kufumbia macho macho magazeti ya uchafu na udaku yaliyotamalaki nchini. Kimsingi, magazeti haya hayakiuki maadili ya uandishi tu bali yanakiuka maadili ya taifa kwa ujumla kosa ambalo ni kubwa kuliko ukosoaji. Inashangaza kuona ukakasi kwenye magazeti yanayozikosoa mamlaka, lakini ukakasi huu usionekane kwenye magazeti ya uchafu na udaku yaliyotamalaki yanayoikosea jamii kwa ujumla wake.
Je wahusika wanangoja rais ang’ake ndipo walione tatizo na kuchukua hatua mujarabu? Je ni mantiki ya kupewa dhamana na mamalak husika? Je rais atafanya kila jambo wakati anawateua wasaidizi wake kumsaidia? Kwanini wahusika hawaoni uchafu unaoenezwa na magazeti haya hatarishi kwa maadili ya taifa na umma kwa ujumla ukiachia mbali kuwalisha uchafu walaji wake? Inakuwaje rais, kwa mfano, aone upungufu fulani lakini waziri ashindwe na aendelee kuwa ofisini? Anaendelea kuwa ofisini akifanya kazi gani wakati uhalisia ni kwamba kitendo cha rais kupotezewa muda kushughulikia jambo ambalo linaweza kufanywa na waziri ni ushahidi tosha kuwa mhusika ana tatizio?
Si siri wala kupiga chuku. Kabla ya rais Magufuli kuingia madarakani, Tanzania iliegezwa dampo ya kila aina ya uchafu. Nchi iligeuzwa taifa la kidaku na kipuuzi kwa vipindi vingi vya tawala zilizopita ukiondoa ule wa marehemu baba wa taifa ambaye serikali yake haikuvumilia upuuzi huu kwa kisingizio chochote hata kama ni kutoa ajira na kulipa kodi kwa taifa. Nani anapenda kodi au ajira itokanayo na kazi chafu kama ya magazeti ya udaku?
Kwa vile rais Magufuli ameamua kuona yale ambayo wengi huyaona na kuogopa kuchukua hatua kwa kuhofia kutopendwa au kuyashabikia kama sehemu ya kupumbaza wananchi wasiwashughulikie pale wanapowatendea maovu kama kuendeleza ufisadi na uvivu, tunamshauri waziri anayehusika na habari apeleke mswaada bungeni kuondoa vyombo vya habari vya udaku kwenye mzunguko nchini. Kwani vyombo hivi ni janga kwa taifa hasa wakati huu dunia inapokabiliwa na tishio la ukimwi, ujinga, umaskini na mabalaa mengine ambayo ni chanzo kizuri cha mapato ya magazeti ya uchafu na udaku. Mfano, ujinga unapoongezeka, wateja wa magazeti ya uchafu wanaongezeka. Umaskini kadhalika ukiachia mbali imani za kishirikina na upuuzi mwingine ambavyo ndivyo vyanzo vizuri vya habari kwa magazeti haya hatarishi kwa maadili ya taifa.
Mwandishi wa makala hii amewahi kutembelea nchi zote jirani ukiondoa Msumbiji. Katika nchi jirani zote kuanzia Burundi, Kenya, Malawi, Rwanda hadi Uganda, havina tatizo la udaku kiasi cha kuwa na magazeti ya udaku kama ilivyo kwa Tanzania.
Ni jambo la aibu kwa taifa linalosifika kwa amani na utulivu kugeuzwa la kidaku bila sababu. Nadhani kuna haja ya kufanya utafiti ili kugundua ni kwanini watu wetu wengi wanapenda udaku. Hili ni muhimu hasa ikizingatiwa kuwa kwa baadhi ya majirani zetu kama Kenya, ukitoa tangazo linalovunja maadili, hawangoji mamlaka bali hujichukulia sheria mikononi kuondoa kadhia. Nakumbuka tukio moja lilotokea mwaka 2004 jijini Nairobi karibu na chuo kikuu cha Nairobi. Shirika moja lisilo la kiserikali lilitundika bango Kenya kuonyesha dalili za ngono. Wananchi waliokuwa wakielekea makazini asubuhi walipoliona bango lile wala hawakwenda polisi zaidi ya kuanza kuliporomosha.
Je ni kwanini kwenye nchi jirani hakuna kabisa au hakuna utitiri wa magazeti na televisheni za udaku? Nchini Uganda najua kuna gazeti moja tu liitwalo Pepper. Nchini Burundi, Rwanda na Zambia sijui. Kama yapo yameanzishwa hivi karibuni. Kwanini Tanzania imekuwa kiwanda cha udaku kuanzia wa kimaadili, dini hata mambo mengine. Ukiangalia magazeti yanayojifanya ya tiba, dini na mambo mengine na mambo yanayoandika, licha ya kusikitika, unahoji mchango wa elimu yetu kwa taifa hasa kama wenye mamlaka waliosoma hawawezi kuona hatari na kitisho vitokanavyo na kuruhusu wajinga na waroho fulani waendelee kuharibu taifa na kuwaibia watu wetu kwa kuwalisha uchafu uitwao udaku na uongo kwa magazeti yanayoongelea mambo ya kitaaluma kama tiba.
Tumalizie kwa kuyataka mamlaka yanayohusika na habari na maadili kuondosha kadhia ya vyombo vya habari vya uchafu na udaku nchini haraka bila kungoja rais ang’ake wakati ana mambo mengi ya kufanya.
Chanzo: Tanzania Daima, Feb., 14, 2018.
No comments:
Post a Comment