Baada ya
kujikita kwenye uchafuzi wa maadili wiki iliyopita na kupata muitikio wa kuua
mtu, Kijiwe leo kinarejea kujadili kadhia mojawapo ya uvunjaji maadili, yaani
uvunjaji wa amri ya sita au tuseme kwa lugha rahisi unungaembe wa kisiasa ni
aina fulani ya uchangudoa. Kwa wale wanaotoka etimolojia ya dhana nzima, unungaembe
wa kisiasa ni kitendo cha mchovu kuwa na washikaji wengi. Simpo. Hata hivyo,
leo tutaongelea uchangudoa tofauti na huu wa mwili. Tutaongelea uchangu wa
kichwani aka wa kisiasa.
Kapende
anaingia akiwa na gazeti la Danganyika Daima. Anaamkua na kulibwa mezani.
Mchunguliaji anajiwahi kama kawaida yake. Kapende anazoza “jamani mmeona
wachovu wanavyobadili vyama kama daladala. Kunani jamani mbona mwenzenu
nachanganyikiwa kiasi cha kushindwa kuelewa jinai hii ya kujitakia?”
Mzee
Meneno ambaye wiki jana hakuudhuria Ndevu anakula mic “unashangaa na kuulizia
huu ununga wa kisiasa ambao unaendeshwa na njaa ya kukosa adabu na aibu!
Nadhani kuna sababu nyingi nyuma ya uchangu huu wa kimaadili mojawapo ikiwa ni
njaa hasa iliyopanda vichwani na kuendekezwa.”
Kabla
ya kuendelea Mpemba anamnyang’anya mic na kunena “yakhe uniosema ni ya kweli
tupu. Mie naona wengine wasukumwa na
uchumia tumbo wala si njaa. Kwani wengi wanao ukwasi. Hawana njaa hata kidogo
bali tamaa na kutaka vya dezo muda wote ukiachia mbali kuishiwa kulhali.”
Msomi
Mkatatamaa anaamua kutia guu “wasemaji mliotangulia mmenena vitu vya maana sana.
Tangu siasa iwe dampo la kila anayetafuta ulaji bila kujali usomi wake
unategemea nini? kuna wachovu ambao licha ya kuwa na elimu za kuungaunga au
kughushi, hawana sifa yoyote ya kuajiriwa na kufanya chochote zaidi ya siasa
ambayo kwa kaya za uswekeni ni ubingwa wa kupiga domo na usanii usiofuata
kanuni yoyote. Hivyo, kwa wachovu kama hawa kubadilisha vyama kama nepi si
jambo geni wala la kushangaza. Wana hasara gani iwapo wanapata tonge hata kwa
kujivua nguo na kujidhalilisha kama tunavyoshuhudia? Kwangu, kinachoshangaza ni
mfumo huu unaoruhusu huu uchangudoa wa kimaadili unaoanza kuzoeleka katika anga
za ulaji wa dezo wa wachovu na raslimali zao.”
Kabla
ya kuendelea, Kanji anampoka mic “veve kumbusha mimi ile changu nasema eti
napenda kuu balaa. Yaani baba jima napenda baba nyingine balaa? Sasa kama
napenda baba nyingine balaa bibi yako tapenda wipi dugu yangu? Hata Bombei
hapana sikia kufuru kama hii dugu yangu. Sasa kama baba napenda baba nyingine
balaa nani tapenda mama na toto?”
Mijjinga
anampoka mic Kanji na kuzoza “hivi kama tutakuwa wakweli kwa nafsi zetu hii
naayo ni sera ya kutangaza majukwaani? Kweli kuna mapenzi katika sanaa za ulaji
ndugu zanguni? Ukisikia kufilisika kimaadili ndiyo huku. Jamaa mwenyewe
alishasema hatafuti kupendwa bali kuwatumikia wachovu.”
Kabla
ya Mijjinga kuendelea kudana, Kapende anaamua kumtoa wasi wasi Kanji kwa kusema
“Kanji wala huna cha kushangaa. Njaa inapopanda kichwani msaka tonge yoyote
anaweza kufanya lolote hata kama ni kujivua nguo kama hili baba lililoropoka.
Kimsingi, vyangu kama hawa wanafanya usanii ili tonge lipande kinywani. Hawana
mapenzi yoyote na wale wanaowapenda zaidi ya kupenda ulaji wa dezo utokanao na
usanii huu wa kisiasa. Hakuna zaidi ya hili ndugu yangu. Mimi nawajua nimeishi
nao tangu nikifanya kazi ya kupiga picha. Kimsingi, kinachoendelea ni
unungaembe wa kisiasa.”
Kitendo
cha kutaja unungaembe kinamuibia Da Sofia Lion aka Kanungaembe ambaye anaamua
kula mic “kama ununga wa kisiasa umeruhusiwa hivi, kwanini kuwaandama dada poa
wakati kaka poa wa kisiasa wakivumiliwa wakati hawamuuzi, kumtapeli wala
kumuumiza mchovu yoyote? Maskini kutokana na ukapa uliotamalaki wanajiuzia
miili yao sawa na hawa wasanii uchwara wanaouza roho za wenzao bila aibu wala
huruma.”
Mipawa
anaamua kula mic “hapa dada Sofia umetia na kunena neno la maana. Kimsingi, wasanii hawa njaa wanatiana aibu
bila kufikiri wakidhani wachovu ni wajinga wasioweza kuambua utapeli huu Dhahiri.
Itikadi ni imani na msimamo. Huwezi kudandia vyama kama dala dala ukabakia kuwa
na maana.”
“Nadhani
wewe bado unaota zama za maadili za mzee Mchonga. Siku hizi siasa ni ulaji hata
kama wa kula bila kunawa. Itikadi na msimamo vilikufa na mzee Mchonga kiasi cha
maadili kugeuka madili. Hata hili linakushinda?” anachomekea Mbwamwitu huku
akivuta kombe lake na kubwia kwa madaha.
Mgoshi
Machungi mwana wa Shikilango aliyekuwa akikamua kahawa yake anaamua kutia guu “sisi
kue Ushoto huita haya mnayoshangaa mambeza yaani kufanya mambo kana kwamba
anayefanya hivyo hana akii timamu kama yule kidhabu nabii Tito mjaana aiyekuwa
akihimiza dini ya mashetani ya kutenda maovu. Nashukuu Mungu amekamatwa na
kupigwa stop maa moja. Sijui tinapeekeshwa wapi jamani ambao kia mjaana
anajifanyia atakavyo?”
Kijiwe
kikiwa kinanoga si akapita msanii aliyesema anampenda Mpayukaji balaa. Acha tumzonge
lau tujue alichomaanisha ili ti-understand.
Chanzo: Tanzania Daima, Feb., 14, 2018.
No comments:
Post a Comment