Japo kusifia au kufisiwa ni haki ya anayesifia au kusifiwa, kunapozidi au kufanyika bila sababu za msingi, huleta kero na maudhi kiasi fulani. Mfano, mtu anapokusifia lakini akachelea kukwambia ukweli au kukushauri, basi mtu huyu hakufai hata chembe. Yesu aliwahi kuonya akisema kuwa si wote wajao wakisema bwana bwana wataingia ufalme wa mbinguni; kwani wengi ni wanafiki na wachumia tumbo waliojaa uongo na ghilba. Hivi katibuni, baada ya rais John Magufuli kuingia madarakani, kumezuka magazeti yanayojikomba kwake kiasi cha kusifia kila kitu. Hii si kazi ya magazeti kama sauti ya wasio na sauti. Kazi ya msingi ya kwanza ya vyombo vya habari ni kusimamia na kutetea maslahi yake pamoja na ya wale wasio na sauti katika jamii. Hili hufanyika kwa kuibua madhira na uoza unaowanyima haki zao wasio na sauti. Pia vyombo vya habari hutumika kama jukwaa la wasio na sauti na walio na sauti kueleza mawazo na matatizo yao. Hivyo, kusifia si sehemu ya wajibu wa vyombo vya habari. Hatuna maana kuwa magazeti yamlaumu rais bila sababu. Lakini inatia kinyaa kusoma baadhi ya magazeti juu ya namna yanavyojikomba kwa rais kiasi cha kusifia kila kitu. Kazi ya magazeti ni kufikirisha, kufundisha, kuhabarisha, kukusanya na kusambaza habari na kuibua hoja na uoza na kufanya hivyo bila patilizi wala upendeleo kati ya majukumu mengi halali ya vyombo vya habari. Kwa watu wenye akili sawa sawa na wanatoka kuheshimika na kuendelea lazima wakoseane, wakosoane na kuambizana ukweli. Tusipojikosoa tutaangamia kama jamii na taifa. Hivyo, tusiogope kukosoana na kuambiana ukweli; na ikibidi kusifiana tufanye hivyo pale inapostahili bila kuzidisha wala kutia chumvi.
Kwa wanaokumbuka namna utawala uliopita ulivyokuwa ukifanya kazi, watakumbuka wazi namna baadhi ya wahariri na wenye vyombo vya habari walivyobuni mbinu ya kuihadaa serikali ili kupata upendeleo na ajira. Nadhani bado tunawakumbuka baadhi ya waandishi wa habari na wahariri waliojigeuza wasemaji wa serikali kana kwamba wao ni Habari Maelezo na kuiingiza mkenge kiasi cha wengine kuteuliwa kuwa wakuu wa wilaya mmojawapo akiambulia kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Mawasiliano Ikulu. Baada ya jinai hii kutendeka, makanjanja wengi na wenye vyombo vya habari waliona huu ndiyo mwanya wa kujiunga na ulaji wa dezo serikalini. Wengi tulidhani kuwa tabia hii chafu ya kujikomba na kujipendekeza ingeisha wakati ule. Ni bahati mbaya kuwa imeendelea. Tumekuwa tukisoma magazeti yakisema vitu vya ajabu ilmradi yawafurahishe wanaolenga kuwatapeli.
Nadhani wakati wa kuionya serikali na rais Magufuli mahsusi kuwastukia wasanii hawa ni sasa. Mwandishi wa makala hii amekuwa halalii upande. Huwa anaonya na kusema ukweli Dhahiri bila kujali atamuudhi au kumfurahisha nani. Hii ndiyo kazi adhimu ya uandishi wa habari na uchambuzi wa masuala ya kisiasa. Kwani, umma una imani kubwa na taaluma ya habari.
Wapo wasaka tumbo ambao magazeti yao yalishakufa zamani lakini yakaibuliwa na tabia hii ya kujikomba ili kupata vyeo au tenda za serikali. Hatuwezi kuendelea kunyamazia kadhia hii wakati tukijua madhara ya matumizi mabaya ya dhamana na taaluma ya habari. Tulishuhudia namna vyombo vya habari vilivyochochea mauaji ya kimbari katika nchi jirani ya Rwanda. Tutakuwa ni viumbe wa ajabu; kama hatutaghairi kujifunza tukajiruhusu kuchezewa na kutapeliwa na matapeli wachache tena wenye kutumia njia ya kijinga kama hii.
Kazi ya magazeti kama tulivyosema hapo juu si kutetea serikali au kujivisha jukumu la kuwa msemaji wake. Serikali ina watu wake tena wabobezi katika kufanya kazi hii wanaolipwa kwa kodi za hawa hawa wanaolishwa habari chafu na hawa wanaopenda kujikomba. Tuikatae, kuikemea na kuipiga vita jinai hii itokanayo na uroho, ukosefu wa sifa za kufanya kazi na kujiingiza kwenye uwindaji wa favour toka kwa wenye madaraka. Kwa wanaojua umakini wa rais Magufuli wana imani kuwa hataanguka kwenye mtego huu hasa ikizingatiwa alivyowahi kusema kuwa hakuingia madarakani kutafuta kupendwa kwani kama kupendwa mkewe anatosha. Na hii ndiyo maana juzi juzi aliwaambua baadhi ya matapeli waliotaka kupeleka mswaada wa kutaka avunje sheria kwa kubadili katiba ili kujiongezea muda wa kuwa madarakani. Hawa wote si kwamba wanampenda Magufuli bali ulaji tu. Hii inatukumbusha mwanaume mzima ambaye anajua kuwa maadili yetu hayaruhusu upuuzi aliyesema hadharani kuwa anampenda Magufuli balaa. Nadhani hili litakuwa limemchukiza Magufuli ukiachia mbali kumstua asijue wapo wengi wanaotumia njia mbali mbali kujikomba kwake ili wapate mlo au vyeo hasa wakati huu ambavyo vyuma vimebana kama anavyopenda kusema rais Magufuli. Hata watendaji au wateule wake wanaopenda kumsifia hawakosi kwenye kundi hili la waimba kwaya za sifa wakati mioyoni ni maadui na mafisi wa kawaida kama yule mchungaji wa kuchipachika aliyejaribu kupambana na mteule mmoja wa Magufuli huku akimsifia akaishia kumdharau na kumuumbua.
Tumalize kwa kumshauri Magufuli awe na macho na wale wanaomwendea wakisema bwana bwana. Si chochote bali mbwa mwitu wasaka tonge wanaoendesha na njaa na si upendo wa dhati.
Chanzo: Tanzania Daima, Feb., 21, 2018.
No comments:
Post a Comment