Wakoloni walisamehe taasisi za dini kodi tokana na mchango wao mkubwa katika kueneza ukoloni Afrika kwa vile wote walikuwa ni kitu kimoja katika kuiibia na kuhujumu bara la Afrika. Hivyo, chanzo kizuri cha kusamehe taasisi za dini kodi ni dhana nzima ya ukoloni kuhakikisha zilikuwa zikiendelea kuwapeleleza waafrika na kuwafanya wawe watiifu kwa mamlaka za kikoloni zama zile.
Hata hivyo, ni bahati mbaya sana kuwa baada ya kupata uhuru, ima kutokana na kutojua au kuongozwa na wakoloni weusi, kupwakia kila kitu cha kikoloni kama vile kuwa na staili za utawala sawa na zile zilizoachwa na wakoloni, nchi za kiafrika zilirithi na kuendeleza kandokando hili la kikoloni bila kujua kuwa watatokea matapeli na wasaka tonge kuutumia udhaifu huu kuibia umma na kujipata utajiri wa dezo na haraka. Ni kutokana na dhana na tabia hii ya kikoloni, asasi za kidini ziliendelea kuwanyonya waafrika hadi leo ambapo kwa sasa zinatumiwa na baadhi ya matapeli kujitajirisha huku nchi zao zikiendelea kusamehe kodi kwa mabilioni lakini zikaendelea kutegemea kuombaomba na kukopa.
Kitendo cha kuendeleza makandokando ya ukoloni kuhusiana na ukusanyaji na ulipaji kodi kilichomotisha matapeli kila aina kuanzisha madhehebu ya dini ili kujitajirisha haraka. Tunao wengi nchini kwa sasa wanaolala maskini na kuamka matajiri. Wanakwepa kodi hata wengine kutumiwa na wafanyabiashara kukwepa kodi wakiwalipa kidogo kama ilivyowahi kutokea kwa shirika moja lililokutwa likiingiza magari ya wafanyabiashara kwa mgongo wa dini. Ni jambo la hatari, kwa mfano, kama ilivyotokea hivi karibuni ambapo dhehebu fulani lenye kutia shaka lilikutwa halina hesabu za mapato na matumizi yake na bado mamlaka, pamoja na kupata ushahidi, zilishindwa kuliadhibu kwa uvunjaji wa sheria huu wa wazi. Je yapo madhehebu mangapi ambayo, kimsingi, hayana tofauti na maduka au miradi binafsi ya viongozi wake? Je hili nalo linahitaji ugwiji wa historia au uchumi kulibaini na kulitafutia suluhu ya kudumu?
Najua wapo watakaojitokeza kutetea mfumo huu ima wanufaika au wale wanaohisi wananufaika kwa kusema kuwa madhehebu ya dini yanatoa baadhi ya huduma za jamii kama afya na elimu. Sina ugomvi na haya hasa ikizingatiwa kuwa hawatoi bure kama serikali inavyofanya. Hivyo, utoaji wa huduma kama hizi si sababu ya kusamehewa kodi. Isitoshe, kiwango cha huduma wanazotoa ni kidogo sana ikilinganishwa na kile kinachotolewa na serikali. Kwa nchi ambayo imekuwa huru kwa zaidi ya miongo mitano kuendelea kuwa maskini na kusamehe kodi ni dhambi isiyosameheka kama wananchi wangejitambua na kuhoji vilivyo. Nani anahitaji huduma ambazo zinatumika kama kisingizio cha kulipa kodi? Kwanini wahusika wasilipishwe kodi ili kuipa serikali uwezo wa kutoa hizo huduma wanazosingizia kutoa? Hali inakuwa mbaya kwa nchi ambazo hazina sheria za maadili zinazomtaka kila mwananchi na mkazi wake kutaja vyanzo vya mapato yake huku akiainisha alivyochuma na kutumia. Kwa wale waliokuwa wakihoji na kushuku utajiri wa haraka wa baadhi ya viongozi wa dini wa kujipachika, wanaweza kupata jibu tokana na hili. Je tutaendelea kuvumilia jinai hii kwa maangamizi yetu hadi lini kama taifa na watu?
Ni ajabu baadhi ya taasisi za serikali zinalipa kodi lakini madhehebu ya dini hayafanyi hivyo.
Wenye madhehebu ya dini wanaoonekana kuwa matajiri lazima watungiwe utaratibu wa kuwabana ili mapato na matumizi yao yajulikane wazi ili kuepusha kuendelea kuibiwa kwa watu wetu wasioshuku kitu. Hili lipo wazi hasa ikizingatiwa kuwa hata huyo Yesu wanayedai kumhubiri hakuwa na ukwasi wa aina yoyote na alisema wazi kuwa ufalme wa mbingu si wa matajiri. Tuwakaange kwa mafuta yao. Yesu hakuwahi kuanzisha kanisa wala kutoza sadaka na zaka. Kwani alisema wazi kuwa ni heri ngamia kupitia kwenye tundu la sindano kuliko tajiri kuuona ufalme wa mbinguni. Ajabu ya maajabu, kwa sasa, viongozi wengi feki, nyemelezi na wa kujipachika wametokea kuwa matajiri wa kuktisha na kutia kila aina ya shaka. Je hawa anamhubiri Yesu yupi wakati Yesu mwenyewe anajulikana kuwa maskini na kiongozi wa maskini aliyekuwa hata hana senti ya kulipia kodi hadi alipopewa na samaki? Yesu hakuna na mahekalu wala suti za bei mbaya ukiachia mbali kutotangaza injili yake kupitia vyombo vya habari? Wapo watanaoweza kuhoji vilikuwa wapi vyombo hivi wakati upo ushahidi kuwa kulikuwa na waandishi wa habari ukiachia mbali wakwasi kama akina Nabkadnezza waliokuwa wakilia kwenye vyombo vya dhahabu? Utajiri hakuanza jana wala juzi. Umekuwapo kadiri binadamu alivyokuwapo.
Leo imefikia mahali baadhi ya madhehebu yamegeuza makanisa maduka ya kupatia kila kitu kuanzia fedha, mazao hadi huduma. Mfano wa karibu ni kugundulika kuwa dhehebu moja lilikuwa likimjengea nyumba mke wa kiongozi wake. Kwa kazi ipi na kwanini kama siyo ufisadi wa kiroho utokanao na uroho uliojificha nyuma ya kuhubiri neno la Bwana? Jina la Bwana limegeuka biashara inayolipa haraka huku umma ukiendelea kuibiwa na kutopea kwenye umaskini utokanao na ujinga huku mamlaka zikishuhudia na kusamehe kodi. Umefika wakati wa kuzitoza kodi taasisi za kidini.
Chanzo: Tanzania Daima, Feb., 28, 2018.
No comments:
Post a Comment