Marehemu Akwiline Akwilina aliyeuawa na risasi iliyofyatuliwa na polisi wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kinondonni. |
Wahenga walinena kuwa hakuna
kisichobadilika chini ya jua. Baada ya mtindo mbovu wa siasa za kijambazi
kuanza kuzoeleka, Kijiwe kimeamua kutia guu na kukemea na kulaani mauaji ya
kisiasa yatokanayo na siasa za kijambazi kayani. Baada ya kutoka kwenye matanga
ya Daniel John aliyenyotolewa roho kwenye mazingira ya kutisha, Kijiwe kimekaa
na kudurusu nini kifanyike dhidi ya kadhia hii.
Mijjinga
aliyekuwa rafiki wa marehemu ndiye anaanzisha mada ya leo “jamani wenzangu
mnaongelaje mauaji ya vijana wawili hivi karibuni kwenye kampeni hizi
zinazoendelea kwenye uchakachuaji wa jimbo dogo la Kinondo?”
“Yakhe
wala usinkumbushe hili balaa la kujitakia litokanalo na uchumia tumbo, roho
mbaya na unyama vya kutisha wallahi. Yaani kaya ya wapendanao ya mzee Nchonga
na Karume yaweza kufikia hapa kiasi cha kutoana roho kwa sababu za ulaji wa
dezo? Nalaani sana mauaji haya. Na nasema wazi kuna nkono na ntu hapa wallahi”
analalamika Mpemba huku akionyesha wazi kuudhiwa na ujambazisiasa huu.
Mgoshi
Machungi Shekiango anaamua kumpoka mic Mpemba na kuzoza “waivyontunduisu Issu
niijua titajifunza jambo na kuanza kuheshimu haki za binadamu kumbe wapi? Hawa
waionyotoa roho za Danie na yue binti wa chuo waaaniwe siku zote. Sijui ndata
wanafanya kazi gani jamani? Mbona huko nyuma hawakuwa hivi?”
Msomi
Mkatatamaa akiwa anajiweka vizuri kwenye fomu anampoka mic Mgoshi na kudema “mie
tangu aliosokoiniwa Edward na kukolimbwa Horace, nilianza kuwasha taa nyekundu
japo mauaji haya yalisimama kidogo tokana na mzee Mchonga kutoruhusu siasa za
kijambazi na kuibia wachovu. Ila alipotundulisiwa Tundu, nilibashiri kuwa
muonja hasali hachovyi mara moja. Hivyo,
hitimisho langu ilikuwa ni kwamba siasa tulizozoea kusikia kwenye kaya ya manyang’au
zilikuwa zimepiga hodi kayani. Je wauawe wangapi ndipo tustuke kama jamii, kaya
na watu waliozoea kupendana bila kujali dini, itakadi wala mafungamano ya
kisiasa? Tulizoea kuwa mfano kwa wanaopingana kwa kuuana tokana na kupingana
bila kupigana. Inatisha; lazima tuseme kwa sauti ya juu ili wahusika wajue
tunajua kuwa wapo nyuma ya jinai hii uchwara itokanayo na siasa uchwara. Shame on
them all.”
Kabla
ya kuendelea Kanji ambaye siku hizi ametokea kuwa msemaji anakula mic “hii iko umma
sana. Moyoni yangu naona chungu sana. Kama naveza naveza toka na bundiki yangu
kwenda saka jambazi yote na kumalizia mbali. Kwanini naleta siasa ya tumboni
kwa kaya salama kama yetu? Mimi iko taka data yote fukuzwa kazini kama nakuta
inazembea na kuacha vatu nauawa kama nyama ya mwituni.”
Kapende
anaamua kutia guu na mapema “mimi sishangai haya yanayotokea hasa nikiangalia
namna ushindani wa kisiasa za ulaji ulivyogeuka mtego kwa wachovu wetu wapendao
kula dezo. Hukusikia mjalaana mmoja akikufuru kuwa anampenda mwanaume mwenzake
ni balaa asijue tafsiri itakuwa tofauti? Ukisikia siasa za kijambazi ndizo
hizi. Sijui hawa wanaotuaminisha kuwa wanataka kututumikia na si kututumia
watamuongoza nani wakati wanaanza kunyotoana roho? Je ni kwanini wanene
wamefumba macho na kuziba masikio kana kwamba wanaonyotolewa roho ni mbu au
mbwa? Baya zaidi wanatuaminisha kuwa wanatupenda wakati wanatuponda na
kutunyotoa roho tokana na kutofautiana mawazo na misimamo. Je tutaendelea
kuingizwa nkenge hivi kana kwamba sisi ni hamnazo? Napendekeza tuandamane
kwenda sentro lau wajue tunaudhiwa na ukosefu wa usalama uliotamalaki sasa.”
Mipawa
anaamua kutia guu “mna habari huyu binti aliyepigwa shaba juzi ni mtoto wa
rafiki yangu? Sasa kama mchovu anakwenda kwenye mihagaiko yake usawa huu wa
vyuma kubana anakuwa na wasi wasi kama atarudi salama, haya maendeleo
tunayoambiwa yanataka kuletwa ni kwa ajili ya nani? Kwanini tunaendekeza siasa
za chuki na woga bila sababu za msingi zaidi ya tamaa ya kutaka ulaji ili kula
dezo? Kama tunakuwa wakweli, pale Kinondo kuna sababu ya kuuana wakati wagombea
wanaotaka kuwatumikia wachovu na wanaotaka kuendekeza njaa wanajulikana?”
Kabla
ya kuendelea kudema, Mzee Maneno anakula mic “kusema ule ukweli, mauaji ya juzi
yamenitisha, kuniudhi na kunidhalilisha kama mwanakaya wa kaya hii iliyosifika
kwa amni yake ambayo sasa tunaichezea. Hivi pakichimbika bila jembe
tutakimbilia wapi wakati majirani zetu wote walishaharibikiwa?”
Kabla
ya kumaliza, Mbwamwitu anajibu kwa kebehi “huenda tutakimbilia bahari ya Hindi
ili nyangumi na papa watutafune kama zawadi ya uovu wetu. Nadhani roho za akina
Sokoine, Kolimba na Mwangosi zinatulaani na kutuandama. Maana tumejigeuza
majuha na wauaji tusijue fika kuwa matokeo ya kupanda mbigiri kuwa ni kuvuna
mbigiri hizo hizo.”
Kabla
ya Mbwamwitu kumaliza, da Sofia Lion aka Kanungaembe anajiimbia wimbo wake “amani
kaya ya amani. Mnachezea amani ili kupata shari siyo? Mnaimba amani na
kuborosha maisha wakati mkiharibu na kunyang’anya maisha. Mauaji ya kisiasa
yazuiliwe yasigeuke kansa itakayoteketeza kaya. Wanasiasa huja na kuondoka
lakini kaya siku zote itakuwapo. Wauao watauawa na wakoao wataokolewa. Kila aishie
kwa upanga ajue atakufa kwa upanga. Vibaya hivyo ndugu zangu vibaya hivyo
nasema achene kunyotoana roho kwa mambo ya muda ya kidunia.” Kabla ya kuendelea
anazidiwa uchungu na kuzimia kiasi cha Kijiwe kuishia hapa ili kumuwahisha
hospitali.
Chanzo: Tanzania Daima. Feb., 21, 2018.
No comments:
Post a Comment