Hakuna ubishi. Kila binadamu anahitaji amani katika maisha na ustawi wake kama mtu binafsi na jamii. Amani ni mtaji mkubwa wa maendeleo hasa ikizingatiwa kuwa pasipo na amani hakuna uzalishaji wala fursa za kutumia akili vizuri kwa jamii kujiletea maendeleo. Tokana na umuhimu wa amani, kila mwanasiasa anayetaka kujipatia umaarufu lazima ahimize amani. Wapo wanaotenda vitendo vya wazi wazi vya kuvunja amani kwa kisingizio cha kudumisha au kulinda amani. Huwezi kulinda amani na kuidumisha kwa fujo au ujanja ujanja.
Hata hivyo, kuna utata linapokuja suala la namna ya kuwa na amani. Mfano mzuri rais John Magufuli–akiwa mjini Chato–aliahidi kuhakikisha amani ya Tanzania haichezewi na yeyote awe adui wa ndani au nje au wa kweli au wa kufikirika. Hili ni jambo jema sana kama litafanyika bila kuingilia uhuru wa raia au kutumika vibaya. Tunajua rais Magufuli ni msikivu na ana nia nzuri na Tanzania. Hata hivyo, bila kuangalia upande wa pili, nia yake nzuri inaweza kuishia kuwa mbaya kama baadhi ya mambo ya msingi hayatazingatiwa kwa umakini mkubwa.
Magufuli aliahidi kuilinda amani ya Tanzania kulhali. Kwani, aliwaonya wale wanaotaka kuandamana kuwa watamuona. Alisema kuwa hatajali baba zao wanaowatuma. Hii kidogo, inatisha. Je hao ni akina nani na baba zao ni akina nani? Je kuandamana ni jinai chini ya sheria za Tanzania? Kwanini rais asibadili katiba na kuondoa haki ya kikatiba ya kuandamana? Kuna haja ya kumshauri na kumtahadharisha rais asiingie kwenye mtego wa maadui zake wa kisiasa kirahisi. Kwani, akiendelea kuzuia maandamano, atakuwa anavunja katiba kwa kuwanyima wananchi haki zao za msingi za kuandamana na kueleza hisia na mawazo yao bila kikwazo wala woga. Je kulinda amani kulhali kunaweza kuleta tafsiri gani? Je kunaweza kuwapo amani bila kuwapo haki? Je amani inaweza kulindwa kwa maguvu au maelewano? Je amani ya nchi ni mali ya nani kama si watanzania wote watawala na wapinzani na watawaliwa? Je amani inaweza kudumishwa na vitisho na ukosefu wa uhuru na usawa kwa kila mwananchi kufaidi haki zake za kikatiba? Je amani inaweza kudumishwa na kupiga marufuku siasa au kuminya uhuru wa baadhi ya asasi na watu? Je amani inaweza kulindwa na kudumishwa kwa mtutu wa bunduki? Maswali yana jibu moja kuwa amani haiwezi kudumishwa wala kulindwa na chochote wala lolote bali haki. Kila penye haki kuna amani; na penye dhuluma kuna vurugu au chuki kama si mazingira mazuri ya ghasia baadaye.
Kimsingi, hakuna mtanzania yeyote mwenye akili timamu anachukia amani. Nadhani kinachochukiwa na kupaswa kupigwa vita ni dhuluma. Kuzuia maandamano ni aina mojawapo ya dhuluma. Watanzania hawapaswi kuomba hisani au ruhusa kufaidi haki yao ya kuandamana kama njia ya kuelezea hisia zao. Hii ni haki yao ya kimsingi na kikatiba ambayo haipaswi kuingiliwa wala kukandamizwa bila kubadili katiba na kuiondoa kwenye katiba.
Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, Tanzania si mali ya mtu mmoja au chama kimoja; ni mali ya watanzania wote kwa usawa. Tanzania ni zaidi ya serikali, vyama na watawala. Jukumu la kulinda na kudumisha amani si la rais wala wanasiasa pekee yao. Ni jukumu la watanzania wote wake kwa waume, watoto kwa wakubwa, wanasiasa na wasio wanasiasa.
Ili kuondoa utata, tunashauri udumishaji na ulinzi wa amani ya Tanzania ufuate katiba na sheria tulizojiwekea wenyewe. Mfano, kuna madai ya wazi kuwa kuna uminywaji wa demokrasia nchini. Rejea tamko la hivi karibu la maaskofu ambao hawakumung’unya wala kupindisha maneno. Walisema wazi kuwa kuzuia maandamano na mikutano ya vyama vya siasa vinavyokidhi vigezo si chochote wala lolote bali “uvunjifu wa katiba na sheria za nchi.” uvunjaji wa katiba na sheria za nchi ni jinai kisheria bila kujali nani anafanya hivyo. Pia ni kinyume cha utawala bora na wa sheria. Na anayetenda jinai hii anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria. Je watanzania kweli wanahitaji amani inayowapa baadhi amani wakati ikiwanyima wengine haki zao? Nani anapenda amani hii ambayo kismingi ni feki na ya muda? Je rais na washauri wake wanaliona na kulijua hili na kulikubali? Amani ya Tanzania italetwa na watanzania na si yoyote wala chochote zaidi yao. Amani ya Tanzania lazima ichimbuke na kuchipuka toka kwenye utendaji wa haki bila vitisho, ubaguzi wala upendeleo.
Sitaki niamini kuwa rais Magufuli ana haja ya kuminya uhuru wa wananchi wa kikatiba ili kuwapo amani bandia. Siamini kuwa rais Magufuli anahitaji amani hii bandia na hatia. Hivyo, kuondoa shaka kama hizi, lazima rais Magufuli ajadiliane na wapinzani ambao nao–kama yeye na chama chake–wanawakilisha wananchi.
Tumalizie kwa kuwasihi watanzania waidurusu na na kuitolea ufafunizi dhana nzima ya amani faida na madhara ya kuidumisha na kuilinda bila kujali sheria na katiba na haki za watanzania ambao ni wadau wakuu.
Chanzo: Tanzania Daima leo Machi 14, 2018.
No comments:
Post a Comment