Rais John Magufuli aliwavutia na kuwafurahisha wengi pindi tu alipoingia madarakani. Pamoja na mambo mengine, siku chache baada ya kukabishiwa usukani, Magufuli alianza kwa kishindo cha hali ya juu kwa kupambana na kashfa kubwa kubwa zilizokuwa zimeshindikana ukiachia mbali uoza uliokuwa umeanza kuzoelezeka. Mazoea ya kulea lea ufisadi na uoza kwa ujumla yalianza kutoweka tena ghafla. Aliwakamata watuhumiwa wa kashfa ya IPTL na kuwasweka ndani bila kuwasaza wengine wazito wazito. Kama haitoshi, aliingia kwenye taasisi mbali mbali zilizokuwa zimekithiri kwa upigaji na kuwaondoa au kuwabadili wakubwa zake. Mfano, alifumua Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bandari, Magereza, Uhamiaji, Mamlaka ya Mapato (TRA) na nyingine nyingi ambazo ima wakubwa zake waliachishwa na kushitakiwa au kuhamishiwa idara nyingine. Kwa ujasiri na kasi kubwa, Magufuli alipambana vilivyo na walioghushi vyeti vya kitaaluma pamoja na wafanyakazi hewa waliokuwa wakiliingizia taifa hasara kwa mabilioni.
Tokana na kasi na staili ya Magufuli, watanzania walijenga imani kuwa sasa nchi ilikuwa imepata kiongozi iliyomkosa kwa muda mrefu baada ya kung’atuka kwa marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere hapo mwaka 1985. Kusema ukweli, Magufuli hakuwafurahisha watanzania tu bali dunia nzima kiasi cha kuanza kusikia misamiati mipya kama vile Magufulification na kutumbua majipu. Hata hivyo, wapo waliodhani kuwa nguvu ya Magufuli ilikuwa nguvu ya soda kama siyo ya zima moto.
Hata hivyo, sijui ni kutokana na uchovu au kuzidiwa kazi, kasi ya Magufuli imeanza kupungua kiasi cha kutosikia tena majipu yakitumbuliwa kama ilivyokuwa mwanzo. Je majipu yameisha au kushindikana? Leo tutaangalia kashfa kuu mbili kati ya nyingi ambazo watanzania wanazijua fika. Hizi si nyingine bali kashfa za Lugumi na UDa. Kashfa tajwa, sawa na zile ambazo watuhumiwa wake wameishatiwa korokoroni, zililisababishia taifa hasara kubwa. Tokana na ukubwa wa kashfa hizi, wengi walidhani kuwa rais asingetoa fursa ya watuhumiwa kupumua na wengine kuendelea kufaidi fedha za umma wanazotuhumiwa kuziiba.
Kashfa ya Lugumi ilitokea baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani kutaka kufunga vifaa vya kielektroniki vya kutambua alama za vidole katika vituo vyote vya polisi nchini. Zaidi ya shilingi bilioni 30 zililipwa kwa Said Lugumi bila kanuni za utoaji tenda kufuatwa. Wapo wanaodai kuwa Lugumi, mtu ambaye anatia shaka kulhali, aliweza kupata tenda husika tokana na kuwa na mahusiano na baadhi ya wakubwa wa zama zile ima wa wizara au idara ya polisi. Kwa hiyo, wapo wanaoona kama Lugumi alitumika kama kuwadi wa wakubwa hao kupata tenda hiyo na kuishia kula fedha husika bila kutelekeza mradi husika. Sasa ni miaka zaidi ya miwili tangu Magufuli aingie madarakani. Je ni kweli kuwa ameshindwa kumshughulikia Lugumi na waliomtumia? Je kunani hapa? Je Lugumi ni Bashit mwingine ambaye haguswi hata angetenda makufuru kiasi gani tokana na sababu anazojua mshitiri wake na mhusika mwenyewe? Hakuna haja ya kuandikia mate wakati wino mpya. La kufanya hapa ni kumkumbusha Magufuli kuwa watanzania bado wanamwamini na kumetegemea ashughulikie kashfa ya Lugumi. Maana, inavyoonekana, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), polisi hata Bunge vimeshindwa kushughulikia kadhia hii.
Ushahidi uliopo ni kwamba kashfa hii ilikuwa ifikishwe mbele ya Bunge. Mwaka 2016, vyombo vya habari vilimkariri spika wa Bunge Job Ndugai akisema kuwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) alikuwa akikagua vifaa husika ili kuandaa ripoti yake. Je uchunguzi huu umefikia wapi na umegundua nini?
Mbali na kashfa ya Lugumi, ipo kashfa nyingine ya mabilioni ya uuzaji na utwaliwaji wa lililokuwa Shirika na Usafiri Dar Es Salaam (UDA). Pamoja na bunge na taasisi mbali mbali kushughulikia kashfa hii, inavyoonekana, walioko nyuma ya kashfa hii wana vifua visivyo vya kawaida. Mpaka sasa, hakuna anayeongelea kashfa hii kubwa inayoweza kuwa ilisababisha hasara kwa taifa kuliko kashfa nyingine tajwa. Kwani, tunapoandika, bado kampuni iliyouziwa na kutwaa UDA kifisadi imekabidhiwa mradi mwingine mkubwa wa Usafri wa Kasi jijini Dar Es Salaam jambo ambalo licha ya kutia shaka, linatia doa serikali ya Magufuli kuwa haikulifanyia kazi vilivyo sakata la utwaliwaji na uuzaji wa UDA kinyemela na kinyume cha sheria.
Kukondoa sintafahamu na utata ulioghubika kashfa mbili tajwa, kuna haja ya serikali kuja na maelezo yanaoingia kichwani lau watanzania wajue mbivu na mbichi. Hili litawasaidia kujua kama wamepigwa au fedha na mali zao zitaokolewa toka mikononi mwa wezi wachache wanaoonekana kutoguswa. Je ni kweli kuwa wahusika hawagusiki wakati ushahidi uko wazi? Je hapa tatizo ni utashi au ukosefu wa ushahidi wa kushughulikia kashfa husika? Je hili linatoa picha gani kwa serikali ambayo imejijingea umaarufu wa kupambana vilivyo na uoza nchini na duniani, ukiachia kasoro ndogo ndogo kama ya Bashite?
Chanzo: Tanzania Daima leo Machi 21, 2018.
No comments:
Post a Comment